RAIS Jakaya Kikwete amewataka viongozi na hasa mawaziri wasiowajibika kwa pamoja katika Baraza la Mawaziri na Bungeni, kujiondoa ili watakaobakia wajenge umoja katika kuwatumikia wananchi.
Rais Kikwete alisema , bila umoja katika Wizara au Serikali, kutakuwa na udhaifu mkubwa na viongozi watapingana tena mbele ya watumishi wa Serikali na huwa mbaya zaidi wakipingana katika vyombo vya habari.
Alikuwa akifungua semina elekezi kwa viongozi na watendaji wakuu wa Serikali mjini Dodoma jana.
"Tuepuke kauli za kuchonganisha mawaziri...wakati wote tuzingatie wizara ni moja, Serikali ni moja hivyo tuwe na kauli moja na lengo moja...si vizuri kuona Waziri na Waziri, Waziri na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, wanasemana, wanapingana.
"Si maadili mema katika Wizara wala taasisi yoyote, hata katika kampuni yako binafsi wewe na msaidizi wako mkishindana hadharani, kuna kampuni hapo?" Alihoji katika semina hiyo ya siku nne.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, uzoefu umeonesha kuwa hali ya kupingana kwa mawaziri na viongozi wengine huchangiwa na kuingiliana majukumu ya kazi na kutokuwepo kwa maadili ya utendaji kazi.
"Lazima ikubalike, tukishaamua katika Baraza la Mawaziri, ni uamuzi wetu sote, tunawajibika kuunga mkono na kuutetea, kama unaona huwezi kuwajibika, hapo si mahali pako, toka utatupunguzia mzigo wa kukutetea," alionya Rais Kikwete.
Aliwataka mawaziri pia kuacha utoro katika vikao vya Baraza la Mawaziri na vya Bunge na kwa pamoja waunge mkono miswada inayopelekwa bungeni kwa kuwa huo ndiyo utaratibu wa uendeshaji wa Serikali.
“Muswada wa Sheria ukiletwa na Waziri mmoja, kila Waziri anao wajibu wa kuunga mkono na kuutetea. Haitegemewi na ni kinyume cha maadili cha hali juu kwa Waziri kupinga muswada wa Waziri mwenzake. Kwa kweli, tabia hii haivumiliki na anayetenda hayo amejitenga mwenyewe na Serikali,” alisema na kuongeza:
“Jambo lingine muhimu kwa Mawaziri ni kutambua kuwa kuhudhuria vikao vya Bunge ni jambo la lazima kama ilivyo kwa vikao vya Baraza la Mawaziri. Si jambo la hiyari. Ni lazima Waziri ahudhurie vikao vya Bunge bila ya kukosa labda awe na sababu kubwa inayoelezeka na kukubalika.
“Kutembelea jimbo lako la uchaguzi ni jambo la lazima, lakini siyo sababu ya kukufanya ukose vikao vya Bunge au Baraza la Mawaziri.”
Rais Kikwete pia aliwataka mawaziri na makatibu wakuu kuwapangia kazi na kushirikisha naibu mawaziri na naibu makatibu wakuu katika shughuli za wizara ili wote wajue kinachoendelea na pasitokee atakayekosa kazi.
Aliwataka kutonuniana ikiwa atatokea mwananchi kwenda kumuona Naibu Waziri au Naibu Katibu Mkuu, badala yake wapeane habari kila mara na ikibidi hata kutengeneza sehemu ya kunywa chai pamoja na kupeana habari za utendaji kazi.
"Sio unasikia mtu kaenda kwa Naibu Waziri unasema kwa nini asije kwangu, au yuko ziarani unasema nani kamtuma huko... kumbukeni aliyekuteua kuwa Waziri au Katibu Mkuu ndiye aliyemteua Naibu," alisema.
Katika hilo, alisema Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya na Spika mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa watatoa mada kwao kwa kuwa wana uzoefu wa uofisa wa Serikali, ukatibu mkuu, uwaziri mkuu, uspika na umakamu wa Rais.
Pia aliwataka wajumbe wa semina hiyo ambao ni mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu kuwa mfano mwema kwa jamii inayowazunguka katika kuchapa kazi na maadili, ili watu watamani kufanikiwa kama wao na kuishi kama wao.
"Waziri na Naibu Waziri usinyooshewe vidole vya uvivu, unafika saa tano, unatoka saa saba unaenda kulala...kazi yako uzembe, wizi, kuchonga laini, kutumia ofisi kujinufaisha," alionya Rais Kikwete.
Aliwataka kuheshimiana kwa cheo na umri na kushirikiana kutimiza wajibu wao uliopo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010-2015 huku akisisitiza zaidi maadili.
"Nafasi hizi kuna vitu utavikosa kutokana na maadili ya viongozi... hupaswi kuonekana mbabe, muonevu, mdhulumaji, mzinzi, mlevi kupindukia.
"Hizi si sifa za uwaziri, haiwezekani unaenda baa unakunywa mpaka chupa ya mwisho, wakisema tunataka kufunga, unasema hujui mimi ni Waziri," alisema Rais Kikwete.
Aliwataka viongozi hao kukubaliana na ukweli kuwa katika nafasi walizokabidhiwa, kuna vitu watavikosa na wakitaka vyote, kuna moja litawaponyoka na hasa la uongozi.
Kuhusu kuwatumia wananchi, Rais Kikwete, alisema “Lazima tukumbuke kwamba Serikali yetu imewekwa madarakani na wananchi kwa ajili yao na siyo kwa ajili ya viongozi tuliopo madarakani. Serikali ipo kwa ajili ya kuwahudumia na kutatua matatizo yanayowakabili wananchi na kuwaletea maendeleo.
“Wananchi wanapenda kuona Serikali yao ina viongozi na watumishi waadilifu, wachapakazi hodari, wanaowasikiliza, wanaojali shida zao na wepesi wa kushughulikia na kutekeleza maamuzi mbalimbali ya Serikali. Ni wajibu wetu kama viongozi wakuu na watendaji wakuu kutimiza matarajio hayo ya wananchi.”
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, Rais Kikwete alisema, “Tuliazimia pia kuwa tuanzishe mchakato wa kuipitia Katiba yetu. Tumeanza, lakini kuna upotoshaji mkubwa, lakini wajibu wetu sote tuliopo hapa kukabili hila na njama hizo chafu. Naamini tutafika salama. Kinachotakiwa ni mshikamano na umoja miongini mwetu.”
Mbali na Msuya na Msekwa, pia viongozi wa ulinzi na usalama, wawakilishi wa Benki ya Dunia, CAG na wataalamu wengine wa ndani na nje ya nchi watatoa mada na kujadiliwa.
No comments:
Post a Comment