Tuesday, May 3, 2011

Kikwete atoa ahadi nzito kwa watoto, wajawazito


RAIS Jakaya Kikwete amesema atahakikisha vifo vya watoto chini ya miaka mitano na wajawazito vinapungua mpaka asilimia sifuri ifikapo mwaka 2015.

Alielezea nia hiyo katika mkutano wa waandishi wa habari uliohusu maazimio ya Tume ya Umoja wa Mataifa ya Habari na Uwajibikaji wa Afya ya Wanawake na Watoto, iliyomaliza kikao chake cha pili na cha mwisho Dar es Salaam Jumatatu.

“Kwa Tanzania tumepiga hatua kidogo katika kupunguza vifo vya watoto na wajawazito...lakini tunataka tufikie chini ya moja, maana yake tunataka tufikie vifo sifuri,” alisema Rais Kikwete anayeongoza tume hiyo na Mwenyekiti mwenza, Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harper.

Akifafanua mafanikio yaliyopatikana Tanzania ambayo yamepongezwa na Tume hiyo, Rais Kikwete alisema mwaka 2000, kati ya wajawazito 100,000, wajawazito 578 walikufa wakati wakijifungua ambao kwa mwaka ilikuwa ni sawa na vifo vya wajawazito 8,000.

Lakini kufikia 2010, baada ya Serikali kufanya juhudi za makusudi kukabiliana na hali hiyo, vifo hivyo vya wajawazito vilipungua na kufikia 454 kati ya wajawazito 100,000 sawa na vifo vya wajawazito 6,800 kwa mwaka.

Kwa watoto, Rais Kikwete alisema, katika vizazi 100,000, walikufa watoto 81 mwaka 2000, lakini juhudi za Serikali zilisaidia kupunguza vifo hivyo na kufikia watoto 51 mwaka 2010.

“Mtu anaweza kufikiri kuwa ni vifo vichache kwa nchi yenye watu milioni 40, lakini ujauzito si maradhi, ni utaratibu tu wa Mungu kuendeleza vizazi hatutaki afe hata mmoja,” alisema Rais Kikwete.

Katika mkutano huo, waliazimia kuhakikisha habari za wanaozaliwa na vifo zinapatikana haraka ili hatua stahiki zichukuliwe katika eneo husika hasa katika nchi 74 zinazoendelea ambako zaidi ya asilimia 92 ya vifo hivyo duniani hutokea huko.

Pia wamekubaliana kutengeza utaratibu wa kufuatilia rasilimali fedha zilizoahidiwa na mataifa tajiri zaidi ya Doloa za Marekani bilioni 40 kwa ajili ya kupunguza vifo hivyo na kuhakiki matumizi yake katika nchi zitakakopelekwa.

No comments: