Wednesday, May 11, 2011

Wanajeshi, raia wapambana Dar es Salaam, Mwanamke mjamzito ajeruhiwa

ASKARI wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kambi ya Kunduchi, Dar es Salaam wanadaiwa kuvamia makazi ya wananchi na kuwapiga na kuwajeruhi vibaya baadhi ya watu, mmoja wa majeruhi hao ni mwanamke mjamzito.

Mwanamke huyo kwa sasa amelazwa katika hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam, majeruhi mwingine amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Chanzo cha vurugu hizo hakijawekwa bayana kwa kuwa wanajeshi wanadai kuwa wananchi ndiyo walioanza kupanga mipango ya kuwavamia askari waliokuwa doria eneo hilo la machimbo ambalo wananchi wamepigwa marufuku wasiendele na uchimbaji.

Lakini wananchi wamekanusha madai ya askari hao na kudai kuwa, wanajeshi waliwavamia kwenye makazi yao baada ya kuzozana na baadhi ya wachimbaji ambao walikuwa wanachimba kokoto eneo ambalo si la jeshi.

Tukio hilo lilitokea Jumapili saa nne asubuhi Kunduchi wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

Katika eneo hilo la machimbo ya kokoto kwa sasa baadhi ya watu wameligeuza makazi yao, lakini pia eneo hilo liko liko karibu na Kambi ya JWTZ Kunduchi.

Kwa muda mrefu kumekuwa na mvutano kati ya wachimbaji na wanajeshi kuhusu uchimbaji wa kokoto unaofanywa eneo hilo.

Uchimbaji kwa kutumia baruti ulikatazwa na jeshi na kuwataka wananchi wafanye shughuli zao nje ya mita 500 kutoka kambi ya JWTZ.

Mmoja wa majeruhi, John Kadengu aliliambia gazeti hili kuwa wakati tukio hilo linatokea, alikuwa nyumbani kwake mara akavamiwa na kundi la wanajeshi na ndipo akashitukia anapigwa kirungu begani na baadaye akapigwa ngwala na kuanguka chini.

“Mimi nimeumia na hivi natoka hospitali Muhimbili wameniambia kuwa bega langu limeteguka,” alisema Kadengu aliyedai wanajeshi waliwatesa kwa kuwarusha kichura kwenye matope na pia kuwaamuru wapande kilima huku wakiruka kichura.

Alidai kuwa, wakati anaruka kichura kwa vile alishapigwa, alijisikia vibaya akawaomba wanajeshi wampumzishe; lakini wakaendelea kumtaka aruke kichura na baadaye hali yake ikawa mbaya akakimbizwa kwenye zahanati ya kijeshi kabla ya kupelekwa Muhimbili.

Diwani wa Kata ya Kunduchi, Janet Rithe alisema, yeye alipigiwa simu wakati tafrani hiyo inaanza na alipoenda eneo la tukio alishuhudia wanajeshi wakivamia makazi ya wananchi na kuwapiga virugu na mikanda hali iliyomfanya akimbilie kambini ili kutoa taarifa kwa mkuu wa kambi.

“Nilishuhudia kwa macho yangu wakiingia kwenye nyumba moja iliyoko eneo hilo la machimbo wakampiga mwanamke mjamzito ambaye baadaye tulimkimbiza Hospitali ya Mwanyamala; lakini bahati mbaya ile mimba imetoka,” alisema Janet.

Alidai alipofika kambini alipokewa kwa lugha za kejeli kutoka kwa wanajeshi waliokuwa getini. “Waliniambia usilete siasa hapa au wewe ndio unaowatuma watu wako waje kutufanyia fujo,” alidai diwani huyo.

Alisema, alikuta watu 32 wanashikiliwa na baada ya kuruhusiwa kuonana na mkuu wa kambi, aliwasihi wawaachie wananchi waliokuwa wanashikiliwa ili zifanywe taratibu za kuwashitaki kiraia.

Alisema baada ya kuwaachia na kupelekwa ofisi ya kata ndipo walipowakimbiza watu wanne ambao walijeruhiwa vibaya hospitalini ambako wawili wameruhusiwa kutoka; lakini wengine wawili akiwemo mama huyo mjamzito bado wamelazwa.

Ofisa Habari wa JWTZ, Meja Joseph Masanja alikanusha wanajeshi kuwapiga raia na akasisitiza kuwa, walioumia ni waliojaribu kukimbia kwa hofu baada ya kuwaona wanajeshi wakienda eneo hilo.

Akielezea tukio hilo kwa kina, Masanja alisema, wananchi waliokutwa katika eneo hilo hawakuumizwa wala kupigwa na askari wao.

Alisema siku hiyo, wanajeshi waliokuwa doria katika eneo hilo waliwakamata baadhi ya watu wakiwa wanachimba kokoto. Alisema wakati wakiwahoji, walijitokeza kundi la wananchi ambao waliwaambia wanajeshi hao kuwa hawawezi kuliachia eneo hilo.

Alisema wananchi hao huku wakiwa wamebeba silaha waliwazingira askari hao wawili waliokuwa doria tayari kuwazuru wanajeshi hao.“Baada ya kuona hivyo wale wanajeshi hawakuwa na namna ya kufanya hivyo wakaomba msaada kwa wenzao waliokuwa kambini.”

Masanja alisema, kundi hilo la wanajeshi walipofika eneo hilo walitumia mbinu za kijeshi za kuwaokoa wenzao; hivyo wananchi baada ya kuliona kundi hilo walikimbia ovyo na wengine wakaumia.

Alisema, baadhi ya wananchi walikamatwa na kupelekwa kambini na wakati huo tayari viongozi wa wananchi hao akiwemo diwani walikuwa tayari wameshafika kambini hapo kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa kambi.

“Uongozi wa kambi ulifanya mashauriano na diwani na kuamriwa kuwa wahusika waliokamatwa wapelekwe kwenye vyombo vya sheria kupitia ofisi za serikali za mitaa,” alisema Meja Masanja.

Alisema wananchi hao walikamatwa na vifaa vya kuchimbia kokoto pamoja na malori mawili . Alisema eneo hilo ni la jeshi kwani liko ndani ya mita 500 kutoka kambi ya jeshi.

No comments: