-Kigogo ahamishwa kufunika ulaji wa mabilioni
-Kauli ya Ngeleja bungeni utata mtupu
KASHFA mpya inayohusisha mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imepamba moto na sasa Msimamizi rasmi wa kampuni hiyo, Teophili Rugonzibwa, amehamishwa, Raia Mwema imeelezwa.
Kuhamishwa kwa Rugonzibwa, ambaye ni mteule wa Mahakama aliyekabidhiwa jukumu la kusimamia mali na madeni ya IPTL, kunahofiwa kuwa na malengo ya kufunika tuhuma za ulaji wa mabilioni ya fedha katika tenda za mafuta na kuvuruga kesi iliyorindima kwa miaka tisa ambayo nayo inahusisha mabilioni.
Rugonzibwa, ndiye ambaye amekuwa akiendesha kesi kati ya Mechmar - kampuni ya Malyasia iliyoingia ubia na VIP ya mfanyabiashara Mtanzania, James Rugemalila kuanzisha IPTL kabla ya pande hizo mbili kutofautiana na VIP kuiomba Mahakama kuingilia kati na kisha Mahakama kumteua yeye kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kuwa msimamizi wa IPTL.
Pamoja na kuendesha kesi hiyo, Rugonzibwa akiwa mfilisi, ndiye ambaye amekuwa akisimamia shughuli karibu zote za IPTL akiiwakilisha Serikali katika shauri la ufilisi ambalo linaendelea kusikilizwa Mahakama Kuu, sasa likiwa limeahirishwa bila kupangiwa tarehe maalumu.
Kauli ya Rugonzibwa
Wiki hii, Rugonzibwa - wakili mwandamizi wa Serikali daraja la kwanza, akizungumza katika mahojiano ya simu, aliiambia Raia Mwema kwamba ni kweli alikuwa amepewa uhamisho kutoka RITA kwenda Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ambako alisema hajajua atapangiwa kazi gani.
“Ni kweli siku ya Ijumaa (Mei 6, 2011) Mtendaji Mkuu wa RITA , Philipo Saliboko, aliniita ofisini kwake kama saa 10 hivi jioni na kunipa barua ya uhamisho kwenda Wizara ya Ardhi. Hivi ninavyozungumza na wewe nimeambiwa nikabidhi ofisi na nyaraka zote ndani ya wiki mbili,”alisema Rugonzibwa akikataa kueleza nani atasimamia shughuli za IPTL.
Baada ya uhamisho huo IPTL sasa itaongozwa na raia wa Malaysia, mhasibu kwa taaluma na mwakilishi wa Standard Chartered Bank ya Hong Kong, Magesvaran Subramaniam, ambaye alikuja nchini kama mwajiriwa wa Mechmar mwaka 1998.
Tuhuma za rushwa
Uhamisho wa Rugonzibwa umekuja huku kukiwa na tuhuma za ufujaji mkubwa wa fedha za mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL kwa kipindi cha kuanzia Novemba mwaka jana hadi Februari mwaka huu, ambazo zilitajwa bungeni na Waziri William Ngeleja kuwa ni karibu shilingi bilioni 15 kila mwezi.
Taarifa zinasema kwamba mtandao wa ulaji fedha hizo ni mpana ukigusa uongozi wa juu wa RITA, wafanyakazi wageni wa IPTL na wakubwa ndani ya Wizara ya Nishati na Madini na wizara nyingine kadhaa, ambao kwa sasa hatutawataja kwa sababu za kitaaluma.
Taarifa zinasema wakubwa ndani ya Wizara ya Nishati na Madini wamekuwa wakihusika kikamilifu katika mchakato wa uagizaji mafuta ya IPTL na malipo yake kwa kampuni za Oryx na Total ambazo ndizo pekee zilizopitishwa katika tenda ya mafuta hayo.
Gazeti hili likikariri habari za uhakika kutoka vyanzo mbalimbali vya habari, liliandika wiki iliyopita, kwamba tayari vyombo vya dola vimeanza kufuatilia matumizi ya fedha hizo zinazotolewa serikalini kabla ya kuingia katika mfuko mkuu wa Hazina.
Ni utata wa matumizi ya fedha hizo ambao ulimsukuma hivi karibuni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) Zitto Kabwe, kuliomba Bunge kupitia Kamati ya Nishati na Madini, kufanya uchunguzi wa matumizi ya fedha hizo kwa kushirikiana na vyombo vya dola na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
TAKUKURU kuchunguza
Kuna taarifa pia kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nayo imekuwa ikichunguza matumizi ya fedha hizo. Raia Mwema imethibitishiwa ya kuwa maofisa wa TAKUKURU walifika RITA katikati ya wiki iliyopita, mara ya mwisho ikiwa mwanzoni mwa wiki hii, pamoja na mambo mengine, wakihoji uhamisho wa Rugonzibwa katikati ya mchakato wa uchunguzi.
Kinachogomba katika suala hilo ni wingi wa fedha zinazoelezwa kuwa zimetumika katika miezi hiyo kama alivyoeleza katika majibu ya Waziri Ngeleja bungeni, wakati wa Mkutano wa tatu, Aprili 6, 2011, kuwa Serikali ilitumia zaidi ya shilingi bilioni 46 kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL tangu Novemba 2010 hadi Februari 2011.
Maelezo ya Ngeleja Bungeni
Katika maelezo yake bungeni, Waziri Ngeleja alisema shilingi bilioni 46.4 au wastani wa shilingi bilioni 15.62 kwa kila mwezi zilihitajika kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa tani 36,800 za mafuta mazito kwa kipindi cha miezi mitatu, kuanzia 15 Novemba, 2010 hadi 14 Februari, 2011 sawa na tani 400 kwa siku.
Alisema kampuni mbili za Oryx na Total ndizo pekee zinazofanya biashara ya mafuta mazito nchini (Raia Mwema imearifiwa kuwa zipo kampuni nyingine zenye uwezo wa kufanya biashara hiyo) na ndizo zilizoombwa kushiriki katika mchakato wa ununuzi wa mafuta hayo.
“Utaratibu uliotumika kupata kampuni za Oryx na Total ni kwa restricted tendering ambapo, kampuni za mafuta zilitakiwa kufikisha mafuta katika maghala ya IPTL mwezi Novemba, 2010. Katika hali ngumu kama hiyo, maamuzi ya Serikali yalihitajika kufanyika haraka ili kupunguza ukali wa mgawo wa umeme kwenye mfumo wa grid ya Taifa. Fedha za kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL zimetoka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali,” alisema Ngeleja.
Lakini taarifa ambazo Raia Mwema inazo na takwimu za jinsi mafuta yalivyokuwa yakitumika IPTL na umeme uliokuwa unafuliwa katika miezi hiyo yote, zinaonyesha kuwa gharama yake ni karibu nusu ya shilingi bilioni zaidi ya 46 alizotaja bungeni Waziri Ngeleja.
Utata wa gharama za mafuta
Kwa mujibu wa takwimu hizo, kwa Novemba mafuta yaliyotumika IPTL ni meta za ujazo 3,670.09 ambazo ni sawa na lita za ujazo 3,670,090 ambazo kwa mauzo ya fedha za kigeni wakati huo yanaweza kufikia gharama ya shilingi 3,934,336,480 (Tsh. bilioni 3.9).
Takwimu zinaonyesha pia kwamba kutokana na mgao kuwa mkali sana Desemba mwaka jana, IPTL ilizalisha zaidi umeme na hivyo kutumia mafuta mengi zaidi yaliyofikia meta za ujazo 8,146.80 sawa na lita 8,146,800 zenye gharama ya shilingi 8,733,369,600 (sh. bilioni 8.7).
Matumizi ya Januari 2011 hayakuwa makubwa sana na takwimu zinaonyesha kwamba mafuta yaliyotumika IPTL yalikuwa ya meta za ujazo 2,021.43 sawa na lita 2,021,430 ambazo gharama yake iliyoko katika nyaraka ni karibu shilingi 2,166,972,960 (Sh.bilioni 2.1).
Huku mgao ukiendelea kupungua na sababu nyingine, ikiwamo ya Subramaniam kuzima mitambo katikati ya mgao ili kushinikiza apewe mkataba mpya baada ya mkataba wake wa awali kwisha (alikwishakuandika notisi ya miezi mitatu ya kuacha kazi) uzalishaji mwezi Februari ulishuka, IPTL ikiwa imetumia mafuta ya meta za ujazo 1,876.94 ambayo ni sawa na lita 1,876,940 kwa gharama ya shilingi karibu 2,012,079,680 (Sh.bilioni 2.0).
Kwa mujibu wa Waziri Ngeleja bungeni, jumla ya shilingi bilioni 46.4 zilitumika kununuliwa mafuta ya mitambo ya IPTL kwa miezi mitatu kati ya Novemba 15 2010 na Februari 2011, takwimu ambazo ziko juu mno kulinganisha na hali halisi kwani kwa miezi hiyo mitatu takwimu za matumizi ya mafuta IPTL zinaonyesha kwamba mafuta yaliyotumika ni lita 15,715,260 sawa na shilingi 16,846,758,720 (Sh.bilioni 16.8).
Taarifa zinasema hata kama Waziri Ngeleja angezungumzia IPTL kuendelea kutumia mafuta hadi Machi 2011 na Aprili 2011 bado kwa mujibu wa takwimu za kweli ambazo Raia Mwema imefanikiwa kuziona mafuta hayo yasingefikia gharama ya shilingi bilioni 46.4.
Raia Mwema imefahamishwa kwamba kwa Machi, IPTL ilitumia mafuta ya meta za ujazo 4,368.08 ambazo ni sawa na lita 4,368,000 zenye gharama ya shilingi 4,642,496,000 (Sh.bilioni 4.6).
Aidha, imefahamika kwamba kwa Aprili, mafuta yaliyotumika IPTL ni meta za ujazo 2,818.20 ambazo ni sawa na lita 2,818,200 zenye gharama ya shilingi 3,021,110,400 (Sh.bilioni 3.0).
Ukiongeza gharama hizo za Machi na Aprili katika jumla ya miezi mitatu ya mwanzo hesabu ya miezi yote inafika shilingi bilioni 24,510,365,120 ambayo dhahiri ni pungufu chini ya nusu kwa hesabu aliyotoa Waziri Ngeleja katika Bunge.
Mgawo wa fedha
Taarifa za uchunguzi zinaonyesha kuwa mpango wa ulaji ukubwa kiasi hicho, unaoweza kuingiza fedha nyingi kiasi hicho katika mifuko binafsi unaweza tu kufanikishwa na ushiriki mkubwa wa wakubwa, tena katika ngazi ya watendaji wakuu au makatibu wakuu.
“Mnajisumbua bure. Huo ni mpango wa wakubwa. Na si unaona hizo ni fedha nyingi. Ni mabilioni. Hata hizo takwimu mlizonazo watazibadili, si tayari aliyekuwa akizitunza amehamishwa,” alisema ofisa mmoja katika Wizara ya Nishati na Madini ambaye aliomba jina lake lisitajwe.
Ajira tata ya Meneja IPTL
Hali ya utata anayoizungumzia ofisa huyo wa Wizara ya Nishati na Madini inachangiwa zaidi na hatua ya Mtendaji Mkuu wa RITA, Philipo Saliboko kuongeza mkataba wa kazi wa Subramaniam, ambaye sasa ni Kaimu Meneja Mkuu wa IPTL pamoja na ukweli kwamba ni mwakilishi wa Standard Chartered Bank ya Hong Kong iliyoishitaki Serikali ya Tanzania na ambaye kibali chake cha kuishi nchini, cha daraja la B, kiliisha tangu Februari 19, 2011.
Taarifa zinasema hata mkataba wake wa kufanya kazi IPTL ulikwisha Januari 31, 2011 na kwa karibu miezi mitatu, mpaka alipopewa mkataba mpya na Saliboko alikuwa hafanyi kazi kutokana na notisi yake ya miezi mitatu ya Novemba mwaka jana ambayo ingemfikisha katika kuacha kazi Februari 2011.
Imeelezwa kwamba baada ya Saliboko kumpa mkataba, sasa RITA inamtafutia kibali cha kuishi nchini kupitia Kituo cha Uwekzaji (TIC).
Kwa kupata mkataba mpya, na baada ya mfilisi wa IPTL Rugonzibwa kutimuliwa, sasa Subramaniam ni kati ya wahasibu wanaolipwa vizuri sana nchini.
Taarifa zinaonyesha kwamba anapata dola za Marekani 10,500 (karibu sh. Milioni 15) kwa mwezi kama mshahara baada ya makato; ana gari la kisasa kabisa GX Landcruiser analowekewa mafuta kila mwezi; ana dereva wa kuhudumia familia, analipiwa gharama za simu, maji, intaneti, umeme, gesi, na watoto wake wanasomeshwa kwa gharama zaidi ya dola za Marekani 10,000 (Sh.milioni 15) katika shule za kimataifa, na amepewa nyumba ya IPTL yenye samani.
Taarifa zinasema ni fedha hizo nyingi zinazomfanya kuwa karibu sana na uongozi wa juu wa RITA, Wizara ya Nishati na Madini na benki ya Standard Chartered ambayo imekuwa ikifanya jitihada kutaka ilipwe zaidi ya dola za Marekani 117,000 katika shauri lililoko Mahakamani lililokuwa likisimamiwa na Rugonzibwa ambaye habari zinasema Mahakama ilimteua binafsi.
Pengo la Rugonzibwa RITA
Taarifa za ndani ya RITA zinasema kuondoka kwa Rugonzibwa, ambaye uhamisho wake unaelezwa kuwa wa aina yake wa kutoka katika Mamlaka kwenda Serikali Kuu, kutaiacha kesi iliyoko Mahakamani wazi kwa vile ndani ya RITA si Mtendaji Mkuu, Saliboko au wafanyakazi wengine waliobaki, mwenye uwezo wa kusimamia kesi hiyo mahakamani.
Sifa za kazi ya ufilisi kwa mujibu wa Sheria ya Kabidhi Wasii Mkuu sura ya 27 na Sheria ya Mawakili sura ya 341, zinamhitaji mfilisi kuwa si tu mwanasheria, bali awe pia wakili, sifa ambazo Saliboko na timu yake iliyobaki haina.
Wiki iliyopita Saliboko aliliambia Raia Mwema kwamba hakuwa na taarifa za uchunguzi unaofanywa na TAKUKURU ofisini kwake kuhusu ununuzi wa mafuta ya IPTL.
Alisema pamoja na RITA kusimamia IPTL, haina mamlaka na wala fedha zinazotolewa na Serikali hazipitii ofisini kwake na kwamba hata taratibu za ununuzi na maamuzi yote mazito hufanywa na Serikali kuu moja kwa moja baada ya ofisi yake kutoa taarifa za upungufu wa mafuta katika mitambo ya kuzalisha umeme.
Sakata la IPTL limekuwa la kihistoria tokea kuingia kwa kampuni hiyo nchini, ikihusishwa na ulaji rushwa wa kutisha ambao hadi sasa hakuna hatua zozote za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya wahusika pamoja na kuwapo kiapo cha Patrick Rutabanzibwa, ambaye wakati huo alikuwa Kamishna Nishati. Rutabanzibwa sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, anakopelekwa Rugonzibwa.
Bilioni 160 za ESCROW Account
Wakati hayo yakiendelea, bado kuna taarifa za kuwapo wanasiasa na watendaji ambao wanazinyemelea fedha ambazo zinawekwa kwenye akaunti maalumu Benki Kuu ya Tanzania (ESCROW Account) ambapo zimefikia zaidi ya Shilingi bilioni 160, fedha zinazosubiri uamuzi wa kisheria wa masharuri yanayoendelea kuhusiana na IPTL.
Hivi karibunini katika kikao cha Bunge, Zitto alisema TANESCO wanalipa capacity charge ya zaidi ya shilingi bilioni 3.6 kwa IPTL, na kuhoji zinakotoka fedha za kuilipa IPTL kutokana na kutokuwapo bajeti ya fedha hizo, swali ambalo Waziri Ngeleja alilikwepa kwa kutoa majibu ya jumla jumla.
Katika swali lake Zitto alihoji akianza kwa kusema;
“Ni dhahiri kwamba shilingi bilioni 15 kwa mwezi ni fedha nyingi sana. Wakati tunapitisha bajeti ya Serikali mwaka 2010/2011 hapakuwa na provision yoyote ya bajeti kwa ajili ya mafuta kwa mitambo hii. Waziri alithibitishie Bunge ni katika vote gani na kama ni ya Wizara yake au Wizara nyingine yoyote ambayo tunapata fedha (mabilioni) haya kwa ajili ya kulipia mafuta haya?”
“Kumekuwa na malalamiko na maombi na hoja mbalimbali za kutaka mitambo hii igeuzwe kuwa gas na imilikiwe na Serikali. Lakini mpaka sasa hakuna lolote ambalo limefanyika. Waziri haoni kwamba kuendelea mitambo hii kutumia mafuta kama hivi na bila utaratibu ambao labda mitambo hii imilikiwa na Serikali ni kuwa ni mradi wa watu wachache ambao wanafaidika na mafuta haya?”
Katika majibu yake, Waziri Ngeleja hakuwa na maelezo ya kutosha kuhusu zinakotoka fedha hizo na badala yake alisema, “nimuombe Zitto Kabwe kama anavyofahamu vizuri ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge suala hili ni la takwimu tunayo ofisi inayosimamia mambo yote ya Fedha, chini ya Wizara ya Fedha mimi na yeye tukutane baada ya kikao hiki ili tupeane taarifa kupitia Wizara ya Fedha.”
Ngeleja alisema kwa utaratibu uliopo fedha inayopaswa kulipwa kwa IPTL inalipwa kwenye akaunti maalum ESCROW kwa sababu ya kuwapo mgogoro wa kisheria mahakamani na kwamba ni lazima kuwe na utaratibu maalum hadi hapo mgogoro utakapokuwa umekwisha.
“Kwa nini hatujaweza kufanikisha azma ya Serikali ya kubadili ile mitambo kutoka kwa kutumia mafuta mazito kutumia gesi asili kilichotuchelewesha hapa ni huo mgogoro ulioko mahakamani kwa sababu ya mgogoro hatuwezi kuendelea zoezi hilo linahitaji kufanywa baada ya kupatikana hatma ya mambo ambayo yanabishaniwa mahakamani,” alisema Ngeleja.
Sekta ya nishati nchini imeendelea kugubikwa na kashfa na baada ya IPTL iliibuka kashfa nyingine katika miradi kama hiyo ikihusisha kampuni za Richmond Development LLC na Dowans Holding Limited, kashfa ambazo ziliwagharimu wanasiasa kadhaa akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wawili, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, ambao wote waliwahi kuongoza Wizara ya Nishati na Madini.
No comments:
Post a Comment