Monday, May 9, 2011

Wajawazito kupatiwa vifaa vya kisasa

Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donan Mmbando, amesema serikali imeandaa mkakati mpya kwa ajili ya kuwahudumia akina mama wajawazito ili kupungaza tatizo la vifo kwa wajawazito.

Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, wakati alipokuwa akisoma hotuba yake katika maadhimisho ya siku ya wakunga duniani yaliyokuwa na kauli mbiu ‘Dunia inahitaji wakunga sasa kuliko wakati wowote’ ambayo yalitanguliwa na maandamano yaliyoanzia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii hadi Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Alisema mkakati huo unalenga kuwapatia wajawazito mikoba pamoja na makasha maalum yenye vifaa vya kutoa huduma ya uzazi.

Dk. Mmbando alisema vifaa hivyo vitawasaidia akinamama wajawazito kupata huduma bora na hata kama watajifungulia majumbani itawasaidia.

Alisema mikoba hiyo itasambazwa katika vituo mbalimbali vya afya nchini na kwamba mpango huo umepangwa kutekelezwa katika bajeti ijayo ya serikali.

Alifafanua kwamba serikali imepanga kutoa bure vifaa hivyo ili kila mmoja aweze kunufaika na mpango huo katika maeneo yote nchini.

Kwa upande mwingine, Dk. Mmbando alisema pamoja na matatizo yanayowakabili wajawazito, serikali imefanikiwa kupunguza vifo ambapo utafiti wa mwaka 2005 unaonyesha kuwa kati ya wanaojifungua 100,000 wanaopoteza maisha ni 578. Aidha, alisema utafiti wa mwaka 2010 umeonyesha kuwa kati ya akinamama wanaojifungua 100,000 ni 454 wanaopoteza maisha hivyo idadi imeshaanza kupungua.

Naye Makamu Rais wa Chama cha Wakunga (Tama), Feddy Mwanga, alisisitiza kuwa pamoja na wakunga nchini kukabiliwa na changamoto mbalimbali wanatakiwa kufanya kazi kwa kufuata maadili.

Alisema endapo mkunga atakuwa hana maadili kwa mgonjwa anatakiwa kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria la sivyo atakuwa akiharibu taaluma ya ukunga katika jamii.

No comments: