Thursday, May 19, 2011

Ufisadi Maliasili

-Wanyamapori watoroshewa nje
-Wapelekwa Doha usiku wa manane
-Mlango wa dharura KIA watumika kuwapitisha


NOVEMBA 26, 2010, saa saba usiku, wakati idadi kubwa ya Watanzania wakiwa usingizini, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kulikuwa na pilikapilika kubwa ya kupakia mizigo kwenye ndege ya jeshi la anga la Qatar (Qatar Emir Air Force).

Mizigo iliyokuwa inapakiwa usiku huo mkubwa katika ndege hiyo haikuwa ya kawaida. Wahudumu walikuwa wanapakia wanyamapori hai 130 wa aina 14 tofauti na shehena kubwa ya nyamapori iliyokaushwa, mizigo hiyo yote ni inayotambuliwa kuwa kati ya rasilimali muhimu za Taifa.

Kwa mujibu wa wafanyakazi wa uwanja huo na raia wema kadhaa, wanyama hao hai 130 pamoja na shehena ya nyama zilizokaushwa vilikuwa vinatoroshwa kwenda Doha, Qatar.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mizigo hiyo ilikuwa inaondoka nchini kinyume cha sheria kwa kuwa haikuwa na kibali wala nyaraka sahihi za kiserikali na walioshiriki katika kuratibu na hatimaye kusafirisha mizigo hiyo nao walifanya makosa ya kuhujumu Taifa.

Kati ya wanyamapori hai 130 wakiwa wa aina 14 tofauti, walikuwamo twiga wanne. Twiga hutambuliwa kama alama ya Taifa, sheria za Tanzania zinaharamisha mnyama huyo mpole kuuawa au kusafirishwa kibiashara nje ya nchi.

Shehena ya viroba vya nyamapori zilizokaushwa inaelezwa kuwa ni ya wanyama wengi waliouawa “kijangili” na mtandao wa watu wanaoendesha biashara haramu ya nyamapori.

Ndege hiyo ya Jeshi la Qatar iliwasili KIA Novemba 24, mwanzo ikionekana kama ndege iliyokuwa katika safari za kawaida hadi Novemba 26 usiku wafanyakazi uwanjani hapo waliposhuhudia ikipakia mizigo wakiwamo wanyama hai.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baada ya kuwasili kwa ndege hiyo wafanyakazi wake na marubani walikwenda kupumzika kwa siku mbili katika hoteli ya Naura Springs ya mjini Arusha.

Vinara wa uporaji huo wa wanyama hai wanatajwa kuwa ni raia wawili wa kigeni ambao wameshirikiana na Watanzania wanne ambao walifanikisha kuwatorosha wanyama hao wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 170.

Kati ya vinara hao mmoja ni raia wa Pakistan, Ahmed Kamran, mkazi wa Arusha na mwingine ni mwanamke, raia wa Kenya, Jane Mbogo, mfanyakazi katika kampuni ya Equity Aviation Service inayotoa huduma katika Uwanja wa KIA ambaye anaishi katika nyumba za uwanja huo.

Raia Mwema limefanikiwa kupata majina ya wahusika wengine, lakini haitayataja sasa kwa kuwa haikuweza kuwasiliana nao.

Raia Mwema imefahamishwa pia kwamba washiriki wengine wa mpango huo wa uhujumu ni Watanzania wanne, ambao taarifa zisizotia shaka zilizokusanywa na gazeti hili kwa muda zinaonyesha kuwa ndio waliofanikisha mkakati wa kuwasadia wageni hao kutorosha wanyama hai hao pamoja na shehena ya nyama zilizokaushwa.

Kati yao ni mwanamke mmoja mkazi wa Dar es Salaam ambaye anamiliki kampuni ya kukamata na kumiliki wanyamapori, mtumishi mmoja mwanamke wa idara ya ulinzi ya kampuni ya KADCO inayosimamia shughuli zote za uwanjani KIA, mtumishi wa Serikali katika Idara ya Mifugo KIA na mtumishi mmoja mstaafu wa Idara ya Ushuru wa Forodha.

Wanyama hao walitoroshwaje?

Duru na taarifa zilizokusanywa na Raia Mwema zinaonyesha kuwa kinara wa usafirishaji wa wanyamapori hao ni Kamran ambaye amekuwa akifanya kazi hiyo kwa kutumia leseni ya kuwakamata wanyamapori hai ya kampuni ya mwanamke mmoja wa Dar es Salaam.

Taarifa hizo zinasema wanyamapori waliotoroshwa walikamatwa katika mapori ya akiba na sehemu mbalimbali za mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na kuhifadhiwa katika nyumba anayoishi Mpakistan huyo katika eneo la Baraa, Manispaa ya Arusha.

Taarifa zinaeleza kuwa Mpakistan huyo amekuwa akiwahifadhi wanyama wa aina mbalimbali kwa muda mrefu katika nyumba hiyo ambayo imejengewa ukuta mrefu unaokadiriwa kufikia futi tisa, na kwamba ndani ya nyumba hiyo kuna zizi kubwa la kuhifadhi wanyama na ndege pori.

Ni kutoka ndani ya nyumba hiyo, Novemba 26, mwaka jana, usiku wa saa tatu, malori matatu aina ya Fuso yaliyokuwa yamesheheni wanyamapori hao hai na viroba vya nyamapori zilizokaushwa, yalisafirisha shehena hiyo hadi uwanja wa ndege wa KIA kabla ya kusafirishwa kwenda Doha, Qatar.

Katika uwanja huo, magari hayo yaliyokuwa na wanyama hao yalipitia lango namba 5B ambalo kwa kawaida hutumika kama lango la dharura, hadi ndani ya uwanja ambamo kazi ya kuwapakia ilianza bila vibali kutoka mamlaka za kiserikali zinazohusika.

Kwa utaratibu, wanyama hao walipaswa kupitishwa kupitia lango namba 5A ambako kuna wakaguzi wa Idara za Ushuru wa Forodha, na idara nyingine za kiserikali ambako vibali vyote vingekaguliwa na kupigwa mihuri kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

Wakati magari hayo yalipowasili, Jane Mbogo, kwa makusudi, hakuwa ameandaa taarifa za mzigo huo (cargo manifest) kwa kuwa kampuni yake hairuhusiwi kisheria kuhudumia ndege inayozidi tani 40, badala yake alitumia vifaa vya kuazima kutoka kampuni ya kuhudumia ndege ya Swissport kufanikisha kazi hiyo.

“Hawa Equity Aviation Serevice kisheria wanaruhusiwa kuhudumia mizigo ya ndege ndogondogo, na kwa kufahamu hilo, mtuhumiwa alifanya mipango ya kuazima vifaa vya kampuni ya Swissport ili kuwapakia wanyama hao lakini pia alikacha makusudi kuanisha aina ya mizigo iliyokuwa inasafirishwa ili kuharibu kumbukumbu,” alieleza mtoa taarifa wetu.

Aidha, taarifa zinaeleza zaidi kuwa yule mtumishi wa Serikali wa Idara ya Mifugo naye akifahamu fika kuwa wanyamapori hao hawakuwa na vibali na walikuwa wanatoroshwa nje ya nchi, hakukagua vibali vinavyotakiwa katika usafirishaji.

“Kwa kawaida mizigo inayosafirishwa kwenda nje ya nchi, hasa wanyama hai, lazima wawe na nyaraka zote sahihi za kiserikali na nyaraka hizo hukaguliwa na mamlaka zote zinazohusika na usalama na mambo mengine muhimu katika uwanja lakini wakati wanyama hao wakipakiwa mambo hayo muhimu hayakuzingatiwa,” alieleza mtoa taarifa wetu aliyeshuhudia tukio hilo.

Taarifa zinasema kuwa wakati watu hao wakifanikisha mpango huo, askari mmoja aliwasili uwanjani hapo na kuhoji akitaka kuona vibali vya kusafirisha wanyama hao, lakini wahusika walimweleza kuwa “mzigo unaosafirishwa ulikuwa wa kiserikali”.

Mtoa taarifa wetu anaeleza zaidi kuwa juhudi za askari huyo kutimiza wajibu wake ziligonga ukuta baada ya kujibiwa kwa ukali na afisa wa mifugo, ambaye ni afisa mwenzake serikalini, aliyekuwa akisimamia zoezi hilo kuwa “asiingilie kazi zisizomhusu”; huku pia akimtukana matusi ya nguoni.

Akimkariri afisa huyo mtoa habari wetu alieleza: “Wewe mpumbavu? Una akili? Unaingilia kazi zisizo zako na hivi nakuambia kuwa nitakufukuzisha kazi. Huu ni ugeni wa Serikali usipende kuhoji kitu kisichokuhusu na kama hunielewi mfuate huyo Mhindi (Kamran) hapo akupatie vibali.”

Taarifa zinasema askari polisi huyo alipomwuliza mtuhumiwa huyo kuhusu vibali vya kusafirisha wanyama alidai kuwa asingeweza kudurufu (kutoa kopi) vibali hivyo kwa kuwa ni usiku wa manane na kuahidi kuwa angempatia asubuhi yake, lakini hata hivyo vibali hivyo havikuwahi kuwasilishwa hadi leo.

kwa mujibu wa taarifa hizo, askari huyo alikwenda kutoa taarifa kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha KIA, lakini kwa muda huo tayari ndege hiyo ilikuwa imekwishakuondoka na hakukuwa na hatua zilizoweza kuchukuliwa kuzuia mpango huo.

Habari zaidi zinasema ya kuwa baada ya kukamilika kwa kazi ya kuwapakia wanyamapori hao, wahusika waliwapatia wafanyakazi walioshiriki kupakia mzigo kiasi cha shilingi 150,000 za Kitanzania ili wagawane, mgawo huo ukifanyakia uwanjani hapohapo.

Taarfa za karibuni zaidi kuhusu suala hilo zinasema tayari Polisi walikuwa wamefungua jalada la upelelezi wa shauri hilo na kupendekeza watuhumiwa wote waliotajwa wafikishwe mahakamani, lakini katika mazingira yanayotia shaka hadi sasa suala hilo limekaliwa. Miezi mitano baada ya tukio hilo, hakuna hatua zilizochukuliwa.

Kauli za watuhumiwa

Rai Mwema wiki hii ilizungumza na Kamran kwa njia ya simu ikimtaka kuzungumzia suala hilo, lakini alikana kuhusika na akaongeza kuwa hafanyi biashara hiyo.

“Sihusiki na jambo unaloniuliza. Nafikiri umepiga namba isiyo sahihi (wrong number). Si mimi,”alisema na kisha kukata simu yake.

Kwa upande wake, Jane Mbogo alidai kuwa yeye ni mtumishi wa kampuni ya Equity Aviation Services; hivyo masuala yote hayo aulizwe Mkurugenzi wake na akatoa namba ya simu ambayo hata hivyo, ilipopigwa ilionyesha ya kuwa haitumiki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Swissport, Gaudance Temu, alithibitisha vifaa vya kampuni yake kutumika kupakia mzigo huo na kuongeza kuwa walifanya hivyo baada ya kukodishwa na kampuni ya Equity Aviation Service na walilipwa fedha kiasi cha dola 3,000 za Kimarekani kwa kazi hiyo.

Alisema Temu kuhusu suala hilo: “ Ndiyo, nakumbuka Polisi walikuja kuhoji kuhusu ushiriki wetu katika madai ya kutoroshwa kwa wanyama hao. Lakini tumewaeleza kuwa hatuhusiki, ila vifaa vyetu vilikodishwa na wenzetu wa Equity na walitulipa kwa kazi hiyo. Nafikiri ukienda ofisi yetu ya KIA pale kuna risiti ya malipo hayo kuthibitisha”.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya KADCO ambayo ndiyo inayoendesha Menejimenti ya KIA, Marcus Van De Kreeke, alithibitisha madai ya kutoroshwa kwa wanyamapori hao na kuongeza kuwa hata hivyo menejimenti haihusiki na suala hilo.

“Kazi yetu kama KADCO ni kulinda usalama wa abiria na ndege zinazotumia uwanja huu kwa safari zao, lakini sisi hatuhusiki na usafirishaji wa mizigo inayopita katika uwanja. Hiyo ni kazi ya mamlaka nyingine,” alisema Van De Kreeke.

Aliongeza: “Polisi tayari wameanzisha uchunguzi. Nafikiri tuwaache wafanye kazi yao na tuone uchunguzi wao utaleta majibu gani. Ila kwa upande wetu hatuna tatizo. Tutawapa ushirikiano wa kutosha.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Lukas Ng’omboko naye alithibitishia Raia Mwema kuwapo kwa tukio hilo, na kufafanua kuwa upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendeshwa na maafisa wa timu maalumu ya Polisi kutoka Makao Makuu ya jeshi hilo.

“Tukio hilo ni la kweli lakini tafadhali wasiliana na Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam. Wao ndio waliounda timu maalumu ya askari wa upelelezi na kwa ufahamu wangu walikuwa wameanza kazi ya kuwahoji watuhumiwa,”alisema Kamanda huyo.

Raia Mwema haikufanikiwa kumpata Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba kuelezea hatua walizofikia katika upelelezi wa tukio hilo.

Utorashaji wa raslimali za nchi katika sekta za madini na maliasili umekuwa moja ya matatizo sugu ambayo Tanzania inakabiliana nayo na sababu kubwa inaelezwa kuwa ni kushamiri kwa vitendo vya kifisadi miongoni mwa maafisa wa serikali waliopewa mamlaka ya kusimamia rasilimali hizo kwa niaba ya wananchi.

Chanzo: Raiamwema

No comments: