HALI si shwari ndani ya Umoja wa Vijana Mkoa wa Arusha (UVCCM) kwa kuwa jana kundi lingine la umoja huo liliibuka na kumtaka Mwenyekiti wa umoja huo Mkoa wa Arusha, James Ole Millya aache kufikiria kwa kutumia tumbo na badala yake atumie kichwa.
Wiki iliyopita, kundi lingine linaloonekana linamuunga mkono Millya, lilifanya maandamano hadi katika ofisi za Mkoa za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kumtaka Katibu wa CCM Mkoa, Mary Chatanda kuachia ngazi kwa kumtuhumu kuwa alisababisha Jimbo la Arusha kwenda upinzani na vurugu za umeya wa Jiji la Arusha.
Akisoma tamko la UVCCM Mkoa wa Arusha mbele ya wajumbe zaidi ya 40 wa umoja huo kutoka wilaya za Arusha, Ally Said maarufu kwa jina la Babu, alidai Millya ameshindwa kuitumikia jumuiya, hivyo afukuzwe ama ajiuzulu mwenyewe kwa kukosa sifa.
Said katika tamko hilo ambalo gazeti hili ina nakala, alidai Millya ameshindwa kuwajibika ndani ya UVCCM mkoa na badala yake anagawa vijana kwa kutumiwa na mafisadi, hatua aliyodai ni hatari hapo baadaye.
Saidi ambaye ni Mjumbe wa Baraza la UVCCM Wilaya ya Arusha Mjini, alidai Ally Bananga anayedaiwa kuwa kibaraka wa Millya anayetumiwa na Mwenyekiti huyo kutoa matamko, si kiongozi wa jumuiya hiyo kuanzia ngazi ya tawi hadi Taifa hivyo kumtaka akae kimya kwani anatumia mdomo kuganga njaa yake.
Tamko hilo pia lilimuonya Mbunge wa Viti Maalumu kupitia UVCCM Mkoa wa Arusha, Catherine Maige aache mara moja kutumia fedha za mafisadi kuwagawa vijana wa Arusha kabla ya haijatumika haki ya kikanuni ya kumsimamisha ubunge.
Said alisema, maamuzi ya kujivua gamba kwa watu walioamriwa na NEC ni lazima yatekelezwe ili kukisafisha chama kwa wananchi.
Akizungumzia tamko hilo, Millya alisema hao ni vijana kutoka katika kata mbili za mjini Arusha na ni vijana wanaoshinda katika vijiwe vya kahawa na sio wajumbe kutoka katika wilaya za Mkoa wa Arusha.
Huku akikanusha kutumiwa na mafisadi, Millya alisisitiza kuwa msimamo wake ni kutaka Chatanda kuachia ngazi kwani anakula mishahara miwili kinyume cha taratibu za kikazi na hawezi kuwajibika katika Mkoa wa Arusha kama katibu wa chama.
Kwa upande wake, Magige alipoulizwa kwa simu juu ya madai ya kutumia fedha za mafisadi kuigawa UVCCM Mkoa wa Arusha, alisema sio kweli, bali anasaidia vijana kujikomboa na kugawa misaada sehemu mbalimbali za mkoa huo.
No comments:
Post a Comment