Monday, May 30, 2011

Askofu amtaka Kikwete kutowavumilia wazembe

MWENYEKITI wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Mennonite Tanzania (KMT), Askofu Steven Mang’ana amemtaka Rais Jakaya Kikwete kutokuwa tayari kuwavumilia viongozi wazembe serikalini ambao hawatekelezi na kutimiza wajibu wao kwa wananchi.

Askofu Mang’ana aliyasema hayo jijini hapa wakati wa sherehe za kusimikwa kwa Askofu Mteule Albert Randa kuwa Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Mwanza, ambazo Rais Kikwete alikuwa mgeni rasmi.

Alisema ifike wakati kila mtendaji serikalini aone kuwa ana jukumu kubwa la kutanguliza uzalendo na mapenzi ya nchi yake kwa kutumia nafasi aliyonayo, ashughulike na changamoto lukuki zinazowakabili wananchi, zikiwemo zile za huduma muhimu za kijamii.

Alisema wapo viongozi walioteuliwa na Rais katika nafasi nyeti serikalini, lakini utendaji wake umekuwa sio wa kuridhisha na kumtaka Rais Kikwete achukue hatua mara moja za kuwawajibisha.

“Mheshimiwa Rais anamteua mtu kushika nafasi nyeti serikalini na badala ya yeye kuwajibika na kumsaidia, anabaki kucheza tu, Rais nakuomba uwaondoe viongozi wa aina hii…wapo wengi na wenye uwezo wa kufanya kazi, viongozi wa aina hii hawakusaidii,” alisema.

Aliwataka viongozi wa madhehebu ya dini kutokuwa mahiri katika kukosoa serikali, bali waipe ushirikiano wa kutosha.

“Viongozi wa dini msiwe wepesi katika kuilaumu na kuikosoa serikali, tambueni kuwa Mungu anawapeni nafasi hiyo ili kusaidia taifa letu na Rais wetu ni msikivu ana hekima, busara na upendo hivyo mpeni ushirikiano,” alisema Askofu Mang’ana na kuongeza: “Katika nchi yetu, tunawataka viongozi wawajibikaji walio na uchungu na nchi, wanaomsaidia Rais wetu katika kutekeleza majukumu ya msingi ya kulihudumia taifa, sio Rais wetu aende kushughulikia tatizo dogo la ukosefu wa maji Ubungo, ilihali wasaidizi wake wapo.

“Tunawataka watendaji wa mitaa, serikali za vijiji, wabunge na mawaziri wawajibike kwa wananchi.”

Aidha, aliwataka baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini kuacha tabia ya kushiriki kwenye maandamano kwa lengo la kujipatia umaarufu wa kisiasa na kusema kuwa kufanya hivyo ni kuingiza nchi katika machafuko na kusababisha kupotea kwa amani nchini kama hali ilivyo katika nchi za Libya na Misri.

“Viongozi wetu lazima wawe tayari katika kuilinda amani iliyopo nchini, kushiriki katika maandamano kama njia ya kuishinikiza serikali ili kudai haki sio sawa, hivi hakuna njia nyingine ya kudai haki, sharti watu washiriki kwenye maandamano tu?” Alihoji askofu huyo.

Kwa upande wake, Rais Kikwete aliwataka viongozi wa dini nchini kuwapatia fursa za nafasi za kusoma kwenye shule zao vijana watakaokuwa wanajiunga na shule za sekondari za kidato cha tano na sita kwa kuwa mahitaji ya shule hizo kwa sasa yatakuwa makubwa kwa miaka ijayo kutokana na wingi wa wanafunzi wanaofaulu kutoka katika sekondari za kata nchini.

“Niwaombe viongozi wa madhehebu ya dini na shule zenu muwapatie fursa vijana wetu wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na sita kwa miaka ijayo ili waweze kusoma maana mahitaji ya nafasi hizo ni makubwa na serikali peke yake haiwezi, maana nikiri kuwa tulijenga sekondari za kata bila ya kuwa na maandalizi ya nafasi za shule kwa ajili ya kidato cha tano na sita,” alisema Rais Kikwete.

Kuhusu udhibiti wa dawa ya kulevya nchini, aliyaomba madhehebu ya dini nchini kwa kushirikiana na wananchi kuongeza udhibiti wa vitendo vya dawa za kulevya, kwani alisema hali sio nzuri kwa sasa.

Alisema mwaka jana, watu 12,119 walifikishwa mahakamani kutokana na kupatikana na dawa za kulevya, ambapo kiasi cha kilo 190 na gramu 780 za heroini zilikamatwa, kilo 65 za kokeini na kilo 27,9520 za bangi na mirungi kilo 10,310 ilikamatwa.

“Hali sio nzuri kwa Mkoa wa Mwanza juu ya kuwa na wingi wa dawa ya kulevya, naomba kwa pamoja viongozi wa dini na serikali tushirikiane katika kuidhibiti hali hiyo,” alisema Rais Kikwete.

No comments: