Monday, May 16, 2011

Mkurugenzi Mkuu IMF adaiwa kubaka

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Dominique Strauss-Kahn amefunguliwa mashitaka na Polisi wa New York nchini Marekani kwa tuhuma za kumshambulia na kutaka kumbaka mhudumu wa hoteli jijini humo.

Strauss-Kahn (62) alishushwa ndani ya ndege ya Air France kwenye Uwanja wa Ndege wa John F. Kennedy (JFK) dakika chache kabla ya ndege hiyo kuondoka kwenda Paris, Ufaransa.

Polisi wamesema, kiongozi huyo anakabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kutaka kubaka.

Wakili wake ameliambia Shirika la Habari la Uingereza (Reuters) kuwa kiongozi huyo atakana mashitaka hayo.

Bosi huyo wa IMF mwenye mke na watoto ambaye amewahi kuwa Waziri wa Fedha wa Ufaransa, alikuwa pia akitajwa kuwa mmoja wa wagombea urais nchini kwake mwenye mvuto mkubwa kupitia chama cha Socialist.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza ( BBC) Paris, Strauss-Khan alikuwa akiongoza kwenye kura za maoni na alikuwa akionekana kuwa nafasi kubwa ya kumshinda Rais Nicolas Sarkozy.

Kiongozi wa chama cha Socialist nchini Ufaransa, Martine Aubry, alielezea habari za kutiwa nguvuni kwa bosi huyo wa IMF kuwa ni kama “radi” iliyomwacha katika “mshangao” mkubwa.

Strauss-Khan alitarajiwa kupanda kizimbani katika mahakama moja ya New York jana, kwa mujibu wa mtandao. Alikuwa amepanga kukutana na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel jana, lakini mkutano huo ulifutwa.

Katika taarifa yake fupi jana kwenye tovuti yake, msemaji wa IMF, alithibitisha kutiwa nguvuni kwa bosi wao, na kueleza kuwa taasisi hiyo haitaeleza lolote kuhusu kesi hiyo.

“IMF iko imara kiutendaji na katika operesheni zake,” ilieleza IMF. Kabla ya kushushwa kwenye ndege hiyo, alikuwa safarini kwenda katika mkutano wa Mawaziri wa Fedha wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) jijini Brussels, Ubelgiji unaotarajiwa kuanza .

Msemaji wa Kitengo cha Polisi cha uwanja huo wa ndege, alisema Strauss-Kahn aliweka chini ya ulinzi kutokana na ombi la polisi wa New York (NYPD) ambapo baada ya kukamatwa, alihojiwa na polisi hao na alielezwa aliwapatia ushirikiano mkubwa.

Msemaji wa NYPD, Paul Browne alisema kiongozi huyo amefunguliwa mashtaka ya kutaka kubaka, kukiuka sheria dhidi ya ubakaji katika tukio lililomhusisha mwanamke mwenye umri wa miaka 32 katika Hoteli ya Manhattan.

Alisema tuhuma dhidi ya Strauss-Kahn zilitolewa na mwanamke huyo ambaye alikuwa mfanyakazi katika hoteli hiyo.

“Tulipokea simu kutoka eneo la wahudumu wa Hoteli ya Manhattan kuwa ametendewa vibaya na mtu aliyekuwa amekodisha chumba cha kifahari ndani ya hoteli hiyo na baada ya hapo mtu huyo alikimbia,” alieleza ofisa huyo wa Polisi.

Mhudumu huyo alieleza kuwa alilazimishwa kwa kufungiwa ndani ya chumba hicho na kutaka kubakwa.

Akizungumza na Reuters, Browne alitoa maelezo zaidi ya kina juu ya tuhuma zinazomkabili Strauss-Khan.

“Aliwaeleza wapelelezi kwamba (Strauss-Khan) alitoka bafuni akiwa uchi, alikimbilia katika kibaraza cha hoteli ambako alikuwapo mwanamke huyo, alimsukumiza chumbani na kuanza kumfanyia shambulio la kumtaka kimapenzi, kulingana na mwanamke huyo.”

Baada ya kuripoti tukio hilo polisi walijaribu kumtafuta aliyekodisha chumba hicho chenye kugharimu Dola za Marekani 3,000 (takriban Sh milioni 4.5) kwa siku na kubaini kuwa ni kiongozi huyo wa IMF.

“Tulibaini kuwa wakati huo alikuwa tayari Uwanja wa Ndege wa JFK na tuliwasiliana na mamlaka za uwanja huo na ndege aliyopanda ilizuiwa na kiongozi huyo alitiwa nguvuni, wakati huyo yule mhudumu alipelekwa hospitali kwa matibabu,” alisema Brown.

Inadaiwa kuwa kiongozi huyo wa IMF aliondoka hotelini hapo kwa haraka na kusahau simu yake ya mkononi na vitu vyake vingine binafsi.

Hadi sasa IMF haijatoa tamko lolote kuhusu tukio hilo. Mwaka 2008, kiongozi huyo alikuwa akichunguzwa na shirika hilo juu ya uhusiano wake wa kimapenzi na mfanyakazi mwenzake ambapo alikutwa na hatia na kuomba msamaha kwa Bodi ya shirika hilo.

No comments: