Friday, May 6, 2011

Vigogo wabanwa ufisadi mpya IPTL

-Zitto awatuhumu kupata mabilioni
-TAKUKURU yaanza kuchunguza

KUNA taarifa ya kuwa kuna kashfa mpya ya ufisadi inayonukia kuhusu mafuta ya mitambo ya umeme ya kampuni ya Independent Power Limited (IPTL) inayoweza kuwa inawahusisha vigogo serikalini.

Kashfa hiyo ambayo tayari vyombo vya dola vimeanza kufuatilia kwa karibu, inahusisha matumizi yenye utata ya Sh bilioni 15 kila mwezi, fedha zinazotolewa serikalini kabla ya kuingia katika mfuko mkuu wa Hazina.

Tayari Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) Zitto Kabwe, ameliomba Bunge kupitia Kamati ya Nishati na Madini, kufanya uchunguzi wa kashfa hiyo kwa kushirikiana na vyombo vya dola na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG).

Wakati Zitto akitaka Bunge liunde kamati ya kuchunguza suala hilo, Raia Mwema limefahamishwa kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekwisha kuanza kuchunguza suala hilo kwa kina.

Imeelezwa kwamba TAKUKURU inachunguza taarifa za kwamba baadhi ya vigogo wakiwamo wanasiasa na watendaji serikalini wananufaika na mradi huo ambapo baadhi wanatajwa kupata bakshish ya fedha zinazotolewa kila mwezi na serikali kwenda IPTL.

Vyanzo vya habari ndani ya Bunge vimeliambia Raia Mwema kwamba Zitto ameandika barua hiyo Aprili 11 mwaka huu, kwenda kwa Spika akipendekeza Bunge kuunda kamati teule kuchunguza suala hilo.

Kumbukumbu za Bunge (Hansard) zinaonyesha kwamba suala hilo lilianzia Bungeni ambapo katika Mkutano wa tatu wa Bunge, Aprili 6, 2011, Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja alilithibitishia Bunge kwamba Serikali ilitumia zaidi ya Shilingi Bilioni 46 kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL tangu Novemba 2010 hadi Februari 2011.

Katika barua yake kwa Spika Zitto alisema;

“Waziri alikiri kwamba serikali ilitumia mfumo wa zabuni dharura na hivyo kuyapa makumpuni mawili ya
Oryx na Total Zabuni ya kuagiza Mafuta mazito kwa ajili ya kuendesha mitambo ya IPTL. Fedha hii ni wastani wa Tsh 15bn kila Mwezi.

“Kumekuwa na Manung’uniko kuhusiana na zabuni hii na hata kuletea hisia za rushwa miongoni mwa Maafisa wa Wizara ya Nishati na Madini na Kabidhi wasii Mkuu aliyeko Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) ambaye ndiye msimamizi wa IPTL kwa sasa
kufuatia amri ya Mahakama. Inawezekana kabisa kwamba kuna watumishi wa Umma ambao wanafaidika na tatizo la mgawo wa umeme kwa kuhongwa kutokana na zabuni hii ya mafuta mazito kwa ajili ya mitambo ya IPTL.”

Mtendaji Mkuu wa RITA Philip Saliboko, ameliambia Raia Mwema jana kwamba hana taarifa za kuwapo uchunguzi unaofanywa na TAKUKURU, pamoja na kuwa wakala unahusika katika mchakato wa kuisimamia IPTL.

Saliboko alisema pamoja na RITA kusimamia IPTL, hawana mamlaka na wala fedha zinazotolewa na serikali hazipitii katika kwao na kwamba hata taratibu za ununuzi na maamuzi yote mazito hufanywa na serikali kuu moja kwa moja baada ya wao kutoa taarifa za upungufu wa mafuta katika mitambo ya kuzalisha umeme.

Katika maelezo yake Zitto alisema kuna mashaka kuhusiana na utaratibu wa zabuni kama ulifuata sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.

“Ninaleta kwako ombi kwamba Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ifanye uchunguzi maalumu kuhusu zabuni ya uagizaji mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL. Uchunguzi huo, pamoja na mambo mengine, uzingatie malipo yote ambayo Kampuni za Oryx na Total zinafanya kwa watu mbalimbali kuhusiana na biashara hii. Malipo yote ya Kampuni hizi ya ndani ya nchi na nje ya nchi yachunguzwe na Maafisa wa TRA na CAG wakisaidiwa na PCCB (TAKUKURU),” inaeleza sehemu ya barua ya Zitto kwa Spika wa Bunge.

Katika maelezo yake bungeni, Waziri Ngeleja alisema shilingi bilioni 46.4 au wastani wa shilingi bilioni 15.62 kwa kila mwezi zilihitajika kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa tani 36,800 za mafuta mazito kwa kipindi cha miezi mitatu, kuanzia 15 Novemba, 2010 hadi 14 Februari, 2011 sawa na tani 400 kwa siku.

Alisema kampuni mbili za Oryx na Total ndizo pekee zinazofanya biashara ya mafuta mazito nchini na ndizo zilizoombwa kushiriki katika mchakato wa ununuzi wa mafuta hayo, kauli ambayo imepingwa na baadhin ya wadau wa mafuta wakizitaja kampuni nyinginezo zinazofanya biashara ya mafuta hayo na kampuni za madini zinazoendesha mitambo ya umeme wa mafuta.

“Utaratibu uliotumika kupata kampuni za Oryx na Total ni kwa restricted tendering ambapo, kampuni za mafuta zilitakiwa kufikisha mafuta katika maghala ya IPTL mwezi Novemba, 2010. katika hali ngumu kama hiyo, maamuzi ya Serikali yalihitajia kufanyika haraka ili kupunguza ukali wa mgawo wa umeme kwenye mfumo wa grid ya TAIFA. Fedha za kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL zimetoka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali,” alisema Ngeleja.

Hata hivyo, Raia Mwema limethibitishiwa kwamba fedha hizo hutolewa katika akaunti ya makusanyo hata kabla ya kuingia katika mfuko mkuu, jambo ambalo linazidi kuibua utata kutokana na fedha hizo kutofuata taratibu za fedha za serikali na kuwapo ugumu wa kufanyiwa ukaguzi.

Katika swali la nyongeza, Zitto alihoji; “Ni dhahiri kwamba shilingi bilioni 15 kwa mwezi ni fedha nyingi sana. Wakati tunapitisha bajeti ya Serikali mwaka 2010/2011 hapakuwa na provision yoyote ya bajeti kwa ajili ya mafuta kwa mitambo hii. Waziri alithibitishie Bunge ni katika vote gani na kama ni ya Wizara yake au Wizara nyingine yoyote ambayo tunapata fedha (mabilioni) haya kwa ajili ya kulipia mafuta haya?”

Zitto alisema kila mwezi Tanesco wanalipa capacity charge ya zaidi ya shilingi bilioni 3.6 kwa IPTL, fedha ambazo zinawekwa kwenye ESCO Account ambapo zimefikia zaidi ya shilingi bilioni 160.

“Kumekuwa na malalamiko na maombi na hoja mbalimbali za kutaka mitambo hii igeuzwe kuwa gas na imilikiwe na Serikali. Lakini mpaka sasa hakuna lolote ambalo limefanyika. Waziri haoni kwamba kuendelea mitambo hii kutumia mafuta kama hivi na bila utaratibu ambao labda mitambo hii imilikiwa na Serikali ni kuwa ni mradi wa watu wachache ambao wanafaidika na mafuta haya?” alihoji Zitto.

Katika majibu yake, Waziri Ngeleja hakuwa na maelezo ya kutosha kuhusu zinakotoka fedha hizo na badala yake alisema, “nimuombe Zitto Kabwe kama anavyofahamu vizuri ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge suala hili ni la takwimu tunayo ofisi inayosimamia mambo yote ya Fedha, chini ya Wizara ya Fedha mimi na yeye tukutane baada ya kikao hiki ili tupeane taarifa kupitia Wizara ya Fedha.”

Ngeleja alisema kwa utaratibu uliopo fedha inayopaswa kulipwa kwa IPTL inalipwa kwenye akaunti maalum ESCO kwa sababu ya kuwapo mgogoro wa kisheria mahakamani na kwamba ni lazima kuwe na utaratibu maalum hadi hapo mgogoro utakapokuwa umekwisha.

“Kwa nini hatujaweza kufanikisha azma ya Serikali ya kubadili ile mitambo kutoka kwa kutumia mafuta mazito kutumia gesi asili kilichotuchelewesha hapa ni huo mgogoro ulioko mahakamani kwa sababu ya mgogoro hatuwezi kuendelea zoezi hilo linahitaji kufanywa baada ya kupatikana hatma ya mambo ambayo yanabishaniwa mahakamani,” alisema Ngeleja.

Sekta ya nishati nchini imekuwa ikigubikwa na kashfa za mara kwa mara na mradi wa IPTL ndio mkubwa wa kwanza kuhusishwa na ufisadi ambao hadi sasa hakuna maelezo wala hatua zilizowahi kuchukuliwa dhidi ya wahusika kabla ya kuibuka kashfa nyingine katika miradi kama hiyo ikihusisha kampuni za Richmond Develepoment LLC na Dowans Holding Limited.

No comments: