Wanafunzi 126 wa shule za msingi na sekondari Wilaya ya Tandahimba mkoani hapa, wamekatisha masomo kwa kupata mimba katika kipindi cha kuanzia mwaka jana hadi kufikia Machi mwaka huu.
Kwa mujibu wa Ofisa Elimu Taaluma wa Wilaya, Mayloce Nswila, tatizo la mimba kwa wanafunzi wilayani humo bado linasumbua. Nswila alifafanua kuwa kati ya mimba hizo, 78 ni kwa wanafunzi wa shule za msingi wakati 48 ni kwa wanafunzi za sekondari, hali aliyosema inachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya elimu wilayani humo.
“Bado tuna tatizo la mimba za wanafunzi, pamoja na jitihada kubwa tunazozifanya kwa kushirikiana na wadau wengine wa elimu katika kuelimisha jamii ili itambue umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike, lakini bado hali si nzuri sana…..tunaweza kusema walau idadi inapungua ukilinganisha na hapo awali,” alisema Ofisa Elimu Taaluma.
Alisema tatizo kubwa ni mwamko mdogo wa jamii wilayani humo kusomesha watoto wa kike, kwa kuwa wazazi wamekuwa wakiwachukulia kama watu wanaopaswa kuolewa huku wakihusisha msimamo huo na imani za kidini.
Alisema Wilaya ya Tandahimba yenye shule za msingi 111 zenye wanafunzi 45,124 na shule za sekondari 26 zenye wanafunzi 7,345, zimekuwa zikikabiliwa na tatizo hilo kwa muda mrefu sasa na kwamba limesababisha watoto wengi wa kike kupoteza fursa yao ya kupata elimu.
“Hata vyombo vya sheria hawapati ushirikiano mzuri kutoka kwa wazazi wa wanafunzi ambao watoto wao wamepewa mimba, wengi wa watuhumiwa wanakimbilia nchi jirani ya Msumbiji na wale wanaofikishwa mahakamani, basi njama zinafanywa na wazazi za kuharibu ushahidi,” alisema. Tatizo la mimba kwa wanafunzi limekuwa moja ya kikwazo kinachoutia doa katika elimu Mkoa wa Mtwara kutokana na watoto wengi wa kike kukatisha ndoto za maisha yao kwa kupata mimba shuleni.
Serikali na jamii tufanye nini?
No comments:
Post a Comment