KATIKA kipindi hiki ambacho jamii imelemewa na ugumu wa maisha kisiasa, kiuchumi na kijamii, na kwa maumivu na huzuni ikipiga kite,wasomi wameamua kutokuwa upande wowote, na wengine wameamua kuungana na wanaosababisha hali hii.
Kwa kifupi na kwa ujumla, msomi wetu ambaye kwa elimu yake na nafasi yake katika jamii, anapaswa kuwa mlinzi na kisima cha busara, hekima, uhuru na haki; ni mvivu, mwoga, muasi, asiye radhi kupambana dhidi ya maovu katika jamii yake.
Matokeo yake ni nchi kugubikwa na majanga ya rushwa, ufisadi, demokrasia duni, na uporaji wa rasilimali za Taifa unaofanywa na wageni kwa kushirikiana na baadhi ya wzawa kwa nchi isiyo na mlinzi.
Tafsiri ya neno “momi”, ni mtu mwenye uelewa mzuri juu ya mambo; mtu mwenye akili, uwezo wa kufikiri na mmaizi wa mambo. Mmaizi huyu, kwa nafasi yake katika jamii, anatarajiwa kujihusisha na kuhusika na yote katika mazingira yake, ikiwa ni pamoja na jinsi anavyoshiriki na kujishirikisha na wanaomtawala.
Msomi hapaswi kuambiwa tu jinsi mambo yalivyo na yanavyotakia kuwa, bali anapaswa kujihusisha katika kuleta mabadiliko yanayotakiwa na mchakato mzima wenye kuleta mabadiliko hayo. Huo ni wajibu wake usiokwepeka, kwa sababu jamii na nchi kwa ujumla ilikwishajitolea kwa kutoa sadaka ya kile kidogo ilicho nacho, aweze kupata elimu, ili hatimaye aitumikie kwa wema na kwa maendeleo ya wote. Asipofanya hivyo ni mwasi kwa jamii na Taifa lake.
Moto wa majanga yote tuliyoyataja hapo mwanzo unaoendelea kulitafuna Taifa si tu unaongezeka na wasomi wetu wakiangalia, bali wakati mwingine wao ni washiriki katika kuchochea kuni kwa sababu wanazozijua.
Ni kwa sababu hii ipo siku ambay umma wa Kitanzania utachoshwa na uasi huu na kuamua kumsukuma msomi kizimbani kujibu mlolongo wa tuhuma, zikiwamo, kushindwa kutenda na kuwajibika katika kuiokoa jamii nyakati za hatari na migogoro, kuhatarisha ustawi wa Taifa na raia wake; kula njama na ubepari wa kimataifa na mashirika ya nje ya kuhodhi (transnationals), kudumaza, kuua sera sahihi za uchumi za nchi; kuasi mstakabali wa kitaifa (national cause) kwa kujishirikisha na rushwa na ufisadi; na shitaka la mwisho, kuiuza nchi kwa “mbwa mwitu”.
Pale kizimbani, msomi huyu inawezekana akauliza: Kwa nini niandamwe mimi pekee, wakati kuna washiriki (accomplices) wengi tu katika jinai hii? Chochote na kiulizwe; lakini ushahidi wote utamlemea msomi kwa sababu ya jukumu na wajibu wake katika jamii, kama tulivyoeleza hapo mwanzo. Nani asiyejua, asiyeona jinsi wasomi wetu walivyoshindwa kutoa mchango katika kuboresha mchakato wa demokrasia ya kweli katika nyanja za siasa na uchumi; kwamba utawala wa sheria unabezwa, Katiba inakanyagwa kwa kisigino, huku uchumi wa nchi na wa mtu mmoja mmoja (isipokuwa kwa wateule) ukiporomoka kwa kasi ya kutisha?
Je, msomi huyu anaelewa nini, na ametendaje juu ya changamoto mpya kufuatia mfumo huria wa siasa na uchumi wa soko na madhara yake kwa jamii? Chukua mfano wa rushwa: ugonjwa huu si tu kwamba unaangamiza maadili ya kijamii, bali pia unadumaza na kudhoofisha taasisi zote za kidemokrasia nchini. Je, ni kweli hajui, au anajifanya kutojua, kwamba sababu kuu ya rushwa katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa ni matokeo ya kutozingatiwa kwa misingi ya utawala bora, uwanja ambao yeye ni mshiriki na mchezaji?. Atueleze, ameipeleka wapi, au ameifanyia nini Taarifa ya Tume ya Jaji Joseph Warioba juu ya Mianya ya Rushwa nchini?
Uchumi wetu umeshindwa kuchanganya, huku msomi akipiga kelele juu ya paa kwamba “ndege ya uchumi wa nchi inapaa”, wakati ukweli ni kuwa ndege hiyo iko chini, gurudumu zake zimetoboka. Ni nani aliye nyuma ya kashfa za EPA, IPTL, Deep Green, Richmond / Dowans, Mfuko wa “Import Support, Mikataba ya uwekezaji ya kiporaji, kama si msomi mwenyewe?
Nani anayeunda Bunge butu la nchi, lisiloweza kumtetea na kumsemea mwananchi wa chini, lililogubikwa na minyukano ya kugombea maslahi badala ya kupigania maendeleo kwa wote, kama si msomi huyu? Nani anayewauza wananchi kwa “mbwa mwitu”, kwa mashirika mumiani kama Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), na kwa nchi tajiri zenye kupora na kukomba rasilimali zetu, kama si msomi huyu?
Heri waasisi wa uhuru wetu, wengi hawakuwa wasomi sana kama watawala wa leo, lakini walijali maslahi ya walio wengi, walijitoa mhanga, bila hivyo tusingepata Uhuru. Je, tuelewe kwamba usomi siku hizi maana yake ni umamluki wa mitaji na ubeberu wa kimataifa?.
Je, ushahidi wote huu, hautoshi kumpeleka lupango kwa tuhuma zinazomkabili? Umma utamke hukumu na adhabu yake. Lakini subiri kidogo. Ni msingi wa kisheria, kwamba mtu hawezi kuhukumiwa bila kusikilizwa. Tumpe nafasi hiyo, ambayo ni haki yake ya kikatiba pia.
Atafungua utetezi wake kwa kukana na kukanusha kwa nguvu zote tuhuma dhidi yake akisema tatizo si yeye , bali tatizo ni sera za uchumi, wanasiasa na mfumo wa siasa unaopaswa kulaumiwa.
Atacharuka na kuhoji: “Ni nani anayeamua juu ya mahitaji ya jamii? Ni msomi, watu au wanasiasa”. Atasema, kama angeruhusiwa kupitia maktaba yake vizuri, angeweza kuandika vitabu vingi kuonyesha kwamba, ni wanasiasa (iwe hao ni wasomi au la), ndio wanaoamua juu ya mahitaji ya kiuchumi na kisiasa ya jamii na yeye kuwekwa pembeni.
Atasema, Sera kama zile za elimu ya kujitegemea, maendeleo vijijini, mashirika ya umma na vyama vya ushirika, vijiji vya ujamaa, madaraka mikoani, sera za nje, mfumo wa chama kimoja na nyingine zote zilizoifikisha nchi hapa, hazikutungwa na kusimamiwa na wasomi kama yeye, bali wanasiasa, chini ya chama na Bunge lililodhibitiwa.
Atakumbusha juu ya maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ya mwaka 1966, dhidi ya maamuzi ya wanasiasa ya kujiongezea marupurupu kwa gharama ya wanyonge, kwamba ulikuwa mfano hai jinsi wasomi wasivyoiva chungu kimoja na wanasiasa, lakini wakanyukwa nyundo na kufukuzwa chuoni kama njia ya kuwanyamazisha.
Ataeleza chimbuko la mifaraikano, kati ya wasomi na wanasiasa, kwamba linaanzia enzi baada ya Uhuru. Kwamba, mwanzoni wasomi na wanasiasa walishirikiana vizuri katika harakati za kutafuta uhuru na demokrasia ya kitaifa. Baadaye, wakati wasomi wakiendelea kuimarisha dhana ya demokrasia ya kitaifa (nationalist democracy) kwa njia ya mijadala, midahalo na machapisho miaka ya 1960, wanasiasa kwa upande wao, walijikita katika kuhamasisha umma kufikia lengo hili. Hii ilikuwa ndoa ya maridhiano, kati ya wasomi na wanasiasa, walipoweza kuunda timu moja.
Lakini miaka ya 1970 mambo yalibadilika, wakati ukinzani ulipoanza. Wakati wasomi waliendelea kuimarisha na kukomaza demokrasia na matunda ya uhuru, wanasiasa walichoropoka kutaka kuibadili dhamira ya kitaifa (nationalistic consciousness) kuwa itikadi ya kimaendeleo (ideology of developmentalism), na ndiyo iliyokuja kuwa itikadi ya tabaka la watawala waliyoitumia kuendeleza ubinafsi.
Itikadi hii ilisisitiza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa gharama ya demokrasia, kiasi kwamba aliyelilia demokrasia hakuwa “mwenzetu”, wengi wao wakiwa wasomi. Itikadi hii ilibeza kiungo kati ya demokrasia na maendeleo ya kiuchumi kwa kudai kwamba, ukuu wa siasa, na si ukuu wa demokrasia, ulikuwa mhimili wa maendeleo ya kiuchumi.
Pengine hii ilikuwa ni kuitika wito wa Kwame Nkrumah bila kuuelewa vizuri kwamba, “utafuteni kwanza ufalme wa kisiasa, na mengine yote mtazidishiwa”. Kweli nchi iliutafuta ufalme huo badala ya ufalme wa kiuchumi na demokrasia, lakini hadi leo, si ufalme wa kisiasa wala wa kiuchumi tuliopata, kwani tunaendelea kuwa tegemezi kwa vyote kutoka nje.
Kuvunjika kwa ndoa kati ya wasomi na wanasiasa kulizaa uhasama wa kuitana majina mabaya mabaya – “mpinga maendeleo” “mpinga mapinduzi” na majina mengine kwa sababu tu mtu ameamua kutofautiana kimawazo na baadhi ya wanasiasa. Kuanzia hapo, msomi alipata baridi kwa kunyimwa nafasi ya kushiriki katika kuleta mabadiliko ya kijamii; ubunifu ukafifia, akaamua kuziba mdomo kwa hofu ya kuishia kizuizini.
Ni miaka ya 1980 tu wakati mfumo wa chama kimoja ulipobainika kushindwa na migogoro ya kiuchumi kukithiri, ndipo umuhimu wa demokrasia katika maendeleo ulipoanza kujidhihirisha.
Mabadiliko haya, ya demokrasia inavyoonekana sasa ni msingi muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi, amani na utulivu na si kinyume chake. Lakini atasema, katika mazingira haya mapya, ya siasa kununua utajiri, na utajiri kununua siasa, msomi asiye na fedha au asiye fisadi, ana nafasi gani ya kusikilizwa? Je, wanasiasa watamwelewa na kumkubali?
Kama Bunge limesheheni wafanyabiashara, kiasi kwamba maslahi binafsi ndiyo yenye kutawala mijadila Bungeni na sheria zinazotungwa, msomi afanye nini katika mazingira kama hayo?, atauliza.
Atasema, msomi anashindwa kuitumikia jamii yake ipasavyo kwa sababu anabezwa, hapewi nafasi kushughulisha elimu yake kikamilifu. Na kwa sababu hiyo ndiyo maana wasomi wengi wanakimbilia siasa na kutelekeza taaluma zao, kwa sababu wanasiasa wamejitengenezea “pepo” na kuwatupa wasomi jehanamu.
Atamaliza kwa kumnukuu Profesa Alvin Toffler, katika kitabu chake “Powershift”, kwamba “kama elimu ndiyo chanzo cha madaraka ya kidemokrasia, basi hakika mchakato wa kisomi, lazima utilie mkazo uhuru wa mawazo, kutofautiana na kupiga vita aina zote za udikteta, kauli-tabia (dogma), utii na unyenyekevu potofu”.
Mwisho atahoji, “msomi atatekelezaje wajibu wake katika jamii kwa kuitwa “mpinzani”, “mpinga maendeleo”, “si mwenzetu”, “kipofu” au “mvivu wa kufikiri”?. Msomaji, kwa maoni yako, je unafikiri ana kesi ya kujibu? Kwa lipi?
No comments:
Post a Comment