UCHUMI wa dunia unaendeshwa na nchi tajiri chini ya kivuli cha masharti yatolewayo na taasisi za ukopeshaji za Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Taasisi hizi mbili hushirikiana kwa karibu na Jumuia ya Biashara Duniani (WTO) na Jumuia ya Makubaliano ya Jumla katika Ushuru wa Forodha na Biashara (GATT).
Kuna sababu kubwa mbili zitolewazo na taasisi za Bretton Woods kuhalalisha mikopo inayoambatana na masharti. Kwanza, ni kuhakikisha mkopaji anauwezo wa kulipa deni na riba. Pili, eti nchi inaomba mkopo au msaada kwa sababu sera zake zilishindwa kuzaa matunda. Kwa hiyo taasisi hulazimika kutoa sera mpya ili kulinda mkopo unaotolewa.
Waswahili husema; mwenye njaa hana miiko. Mwanzoni mwa miaka ya 1980, Tanzania ilitupilia mbali misingi iliyoijenga kwa muda mrefu na kukubali masharti ya taasisi za Bretton Woods, yaliyopewa kaulimbiu ya SAP (Structural Adjustment Program). Mosi, Serikali ilitakiwa kuondoa ukiritimba wa kulinda bidhaa za ndani kwa kuruhusu bidhaa kutoka nje bila masharti yoyote.
Pili, ilitakiwa kushusha thamani ya shilingi ili kukatisha tamaa manunuzi ya bidhaa kutoka nje (imports), na kuongeza bidhaa zilizouzwa nje (exports). Tatu, fedha za mikopo na misaada zisingetumika kuwapa ruzuku wakulima ili kupunguza makali ya uzalishaji. Na nne, serikali ilishauriwa kubana matumizi katika sekta zote.
Sera za SAP zilivizika kabisa viwanda vichanga vilivyokuwa vimeanzishwa Tanzania. Viwango vya uzalishaji Tanzania vilikuwa ni vya chini sana. Fedha za kigeni zilitumika kununua malighafi kutoka nje, mfano, mafuta, vitabu, madawa na mbolea. Shilingi iliposhushwa thamani na fedha za kigeni kupanda, gharama za uzalishaji zilipanda na kusababisha mfumuko wa bei kwa bidhaa zilizozalishwa na viwanda vya Tanzania.
Mikopo iliyotolewa mwanzoni mwa miaka ya 1990, iliambatana na masharti yaliyoitaka serikali kubinafsisha mashirika ya umma, kuvutia wawekezaji na kuweka mazingira ya kukuza sekta binafsi. Juni 2000 serikali ya Tanzania ilitia saini makubaliano ya sera na IMF. Hata hivyo, Tanzania iliendelea kuelemewa na msalaba wa madeni.
Risala iliyosomwa Februari 2006 na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Salome Mbatia, wakati akifungua warsha ya Mpango wa Milenia, ilitoa mwanga.
Alisema; “deni la nje ni kikwazo kikubwa dhidi ya jitihada za maendeleo na kukua kwa uchumi katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania. Hadi kufikia Novemba 2005, deni la nje kwa Tanzania lilikuwa dola bilioni 7.88 na serikali ilikuwa inalipa wastani wa dola milioni 150 kila mwaka”.
Akichangia hoja katika mkutano wa uchumi duniani uliofanyika Davos, Januari 2005, Rais Benjamin Mkapa alisema mapato ya serikali yalitumika kulipa madeni mapya na kuhudumia ya zamani. Aliomba madeni yafutwe ili mapato ya serikali yatumike katika huduma muhimu za jamii kama elimu na afya. Kilio kilisikika na Tanzania ilifutiwa madeni katika mkutano wa mataifa yenye maendeleo ya viwanda G8 uliofanyika Gleneagles, Julai 2005. Hata kabla ya kufutiwa madeni, bodi ya Benki ya Dunia ilikwisha kuanzisha mpango kabambe wa kuikopesha Tanzania (CAS).
Kuanzia Julai 2005 mpaka Machi 2009, Benki ya Dunia imekwisha kuikopesha Tanzania zaidi ya dola bilioni 2. Asilimia 85 ya mikopo hiyo imewekezwa katika miradi isiyopashwa kupewa kipaumbele na isiyozalisha fedha taslimu.
Mifano michache ni mkopo wa dola milioni 3.5 kwa ajili ya mradi wa Kihansi wa kutunza vyura (Kihansi Spray Toads). Na dola milioni 40 kwa ajili ya kutoa mafunzo, motisha, vivutio na zawadi kwa wizara, idara na asasi za serikali ili kuhimiza tija, utendaji na uwajibikaji.
Kutumia fedha za mikopo kutunza vyura, kutoa motisha, zawadi na miradi mingine isiyozalisha fedha taslimu ni kuwatumbukiza raia katika lindi la umasikini kinyume na Malengo ya Milenia.
June 2008 Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo, aliliambia Bunge kwamba Bajeti ya Serikali ya 2008/2009 ni shilingi bilioni 7216. Takriban asilimia 34 ya fedha hizo inatokana na mikopo au zawadi kutoka nje na asilimia 65 inatokana na mapato ya ndani. Alisema mpaka Desemba 2007, deni la taifa lilifika dola bilioni 7. Katika kipindi cha miaka miwili tu, 2005 mpaka 2007, deni la taifa lilirudi karibia lilipokuwa kabla ya kufutiwa madeni.
Kuna mifano mingi, lakini kwa sababu ya mgao wa umeme unaoendelea, mfano muafaka ni mradi wa kuzalisha umeme wa Songosongo. Mradi unaotoa taswira ya jinsi nchi tajiri zinavyonufaika na masharti yanayoambatana na mikopo kutoka katika taasisi za ukopeshaji.
Ghrama za miundombinu ya mradi wa Songosongo zimegawanywa katika sehemu nne. Mosi, kukarabati na kufufua visima vya gesi kisiwani Songosongo. Pili, kujenga karakana na kufunga mitambo ya uchakataji ili kuchuja, kusafisha na kuondoa maji na kemikali chafu ndani ya gesi.
Tatu, kujenga bomba la kilomita 232 kutoka kisiwani mpaka kituo cha Ubungo Dar es Salaam, na bomba la kilomita 16 kutoka Ubongo mpaka kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill. Na nne, Kuboresha mitambo minne ya zamani katika kituo cha Ubungo ili izalishe umeme kwa kutumia gesi badala ya mafuta, na kununua mitambo miwili mipya ya kuzalisha umeme.
Gharama za miundombinu zinakadiriwa kuwa takriban dola milioni 320. Serikali ya Tanzania ilipata mkopo wa dola milioni 183 kutoka Benki ya Dunia (WB), dola milioni 40 kutoka Benki ya Rasirimali ya Ulaya (EIB) na dola milioni 175 kutoka Benki ya Maendeleo ya Asia (ADB).
Masharti ya mikopo yalikuwa mawili; mosi, kuishirikisha sekta binafsi kwa kuunda kampuni ya kusimamia mradi wa Songosongo. Pili, serikali kuhifadhi hiyo mikopo ili kuikopesha tena kampuni itakayoundwa kusimamia mradi. Iliundwa kampuni ya Songas na serikali iliikopesha tena hiyo mikopo kwa riba ya asilimia 7.1.
Julai 2004 kampuni ya Songas inayomiliki miundombinu yote, iliingia mkataba wa miaka 20 wa kuiuzia umeme TANESCO. Malipo ya TANESCO kwa Songas yamegawanywa katika sehemu mbili; kwanza ni manunuzi ya umeme unaozalishwa. Mitambo ya Songas inazalisha megawati 115 ambazo zinaweza kuigharimu TANESCO dola milioni 4 kwa mwezi.
Pili ni gharama za miundombinu (capacity charge) ambazo zimegawanywa katika sehemu tatu. Mosi, mtaji uliowekezwa na wabia wa Songas wa dola milioni 60 na riba ya asilimia 22. Pili, mkopo wa dola milioni 320 na riba ya asilimia 7.1, ambao ulitolewa na Tanzania kwa Songas. Tatu, gharama za kuhudumia miundombinu na kuzalisha umeme.
Ili kupunguza makali ya gharama za miundombinu, Oktoba 11, 2001 serikali ilikubaliana na Songas kwamba, kama TANESCO haitailipa Songas mkopo wa dola milioni 320 na riba ya asilimia 7.1, basi Songas itasamehewa deni hilo. Mpaka sasa TANESCO imeshindwa kulipa hilo deni, hivyo serikali imeliahilisha mpaka TANESCO itakapoweza kulilipa.
Pamoja na msamaha huo, gharama za miundombinu zilizosalia peke yake, bila ununuzi wa umeme, zinaigharimu TANESCO takriban dola milioni 6 kwa mwezi. Kuzimudu inabidi, ama; TANESCO ipate ruzuku kutoka serikalini au ipandishe bei ya umeme kwa wateja.
Mpenzi msomaji fikiria, serikali ilipewa mikopo kwa masharti ya kuikopesha tena kampuni binafsi ya Songas ili iweze kusimamia ujenzi na uendeshaji wa mradi. Lakini Songas iliingia mkataba na TANESCO (inayomilikiwa na kupata ruzuku kutoka serikali) unaosema, si Songas bali ni TANESCO inayopaswa kuilipa serikali huo mkopo na riba.
Kadri ya mkataba, TANESCO isipolipa, Songas inasamehewa deni. Songas inaweza kusamehewa deni na serikali kwa sababu TANESCO haiwezi kulilipa, lakini serikali inalazimika kulipa hilo deni katika mabenki ya WB, EIB na ADB.
Kwa nini mkopo wa mradi wa Songosongo haukutolewa moja kwa moja kwa kampuni ya Songas badala ya serikali? Au kwa nini serikali haikukopa kwa niaba ya TANESCO ili kuliwezesha shirika kuingia katika ubia na Songas bila kulazimika kulipia gharama za miundombinu?
Kwa nini Songas wasiuze umeme moja kwa moja kwa wateja badala ya kuiuzia TANESCO? Mbona kampuni ya Orca inauza gesi katika viwanda vya Kioo, TBL, Urafiki, na Aluminium Afrika bila kulipia gharama za miundombinu?
Wabia wa Songas ni Globeleq (mtaji wa dola milioni 33.8 na hisa asilimia 56). Globeleq iliundwa mwaka 2002 na kitengo cha maendeleo ya kimataifa (DFID) cha serikali ya Uingereza. Ni shirika la umma linalomilikiwa na serikali ya Uingereza kwa asilimia 100.
Kampuni ya Maendeleo ya Uholanzi (FMO) - (mtaji wa dola milioni 14.6 na hisa asilimia 24). FMO iliundwa mwaka 1970 na serikali ya Uholanzi, ambayo inamiliki asilimia 51 ya hisa za kampuni hiyo. CDC (mtaji wa dola milioni 3.6 na hisa asilimia 6). CDC iliundwa mwaka 1948 na serikali ya Uingereza, ambayo inaimiliki kwa asilimia 100.
Wengine ni TDFL (mtaji wa dola milioni 4 na hisa asilimia 7). TDFL inamilikiwa na tawi la benki ya Uingereza la African Banking Corporation kwa asilimia 68 na serikali ya Tanzania kwa asilimia 32. Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) - (mtaji wa dola milioni 3 na hisa asilimia 5). Shirika la Umeme (TANESCO) - (mtaji wa dola milioni moja na hisa asilimia 2).
Kwa nini nchi tajiri zinashabikia mikopo kwa nchi masikini inayoambatana na masharti ya kuinua sekta binafsi, lakini katika mradi huu, Uingereza imeleta kampuni ya Globeleq inayomilikiwa na umma? Sekta binafsi ya Tanzania itakua vipi kama asilimia 76.6 ya hisa za Songas zinamilikiwa na serikali za nchi tajiri za Uingereza na Uholanzi?
Ni watanzania peke yao kupitia TANESCO na serikalini wanaogharamia mtaji wa wabia wa Songas wa dola milioni 60, mikopo ya dola milioni 320 iliyogharamia miundombinu, gharama za kuendesha mitambo, ambayo awali ilimilikiwa na TANESCO na gesi inayotumika kuendesha mitambo, ambayo ni mali ya Watanzania. Pia wananunua Umeme unaozalishwa.
Baada ya miaka 20 ya mkataba, Shirika la umma la Uingereza (Globeleq) litaondoka na faida, na shirika la umma la Tanzania (TANESCO) litarithi madeni yasiyolipika.
No comments:
Post a Comment