Tanzania inaendelea kupoteza mamilioni ya fedha kutokana na serikali kusuasua kupeleka bungeni muswada wa sheria itakayoongoza sekta hiyo nchini.
Inaelezwa kuwa kutokuwepo kwa sheria ya madini nchini kumesababisha sekta hiyo kuendeshwa kiholela na kutokuwepo kwa udhibiti wa kutosha, hali ambayo inawanufaisha zaidi wawekezaji wa nje wanaotumia mwanya huo kuhamishia nchi za nje fedha zinazotokana na biashara hiyo.
Madini moja ya sekta inayoelezwa kuzalisha mabilioni ya fedha kila mwaka, imekuwa ikichangia kwa kiasi kidogo tu katika pato la taifa, hali ambayo imekuwa ikiwashangaza watu wengi wakiwemo wachumi kiasi cha kuzusha malalamiko kutoka kwa wananchi.
Wataalam mbalimbali, wachumi na wabunge mara kwa mara wamekuwa wakipiga kilele kuitaka serikali ifumbue macho na kutazama jinsi taifa linavyoibiwa mamiloni ya fedha katika sekta hiyo, lakini kasi imekuwa ndogo katika utekelezaji.
Pamoja na kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na madini mengi na ya kila aina, vikiwemo vito vya thamani ambavyo baadhi yake havipatikani mahali popote duniani, bado haijaweza kunufaika na sekta hiyo kutokana na kuwepo kwa utaratibu mbovu katika kuisimamia.
Hata hivyo, Rais Jakaya Kikwete, baada ya kuingia madarakani, aliliona tatizo hili na kuchukua hatua ya kuunda tume ya kufuatalia sekta ya madini na kisha tume hiyo itoe mapendekezo yake ili taifa liweze kunufaika na sekta hiyo kuliko ilivyosasa.
Tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mark Bomani, kwa bahati nzuri ilishakamilisha kazi na kukabidhi ripoti yake kwa Rais Kikwete.
Baadhi ya mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo ni kutaka itungwe sheria mpya ya madini na kufanyiwa marekebisho sera inayoongoza sekta hiyo.
Inaelezwa kuwa endapo serikali itakubaliana na mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti ya Tume ya Jaji Mark Bomani, taifa litaanza kunufaika kwa kiasi kikubwa na madini yake kuliko ilivyo sasa ambapo pamoja na kukua kwa sekta hiyo hadi kufikia kuchangia asilimia 40 ya mapato yatikanayo na mauzo nje ya nchi, lakini inachangia asilimia 3 tu ya Pato la Taifa.
Katika kikao cha Bunge cha Novemba mwaka jana, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema kulingana na ripoti ya Jaji Mark Bomani, sekta ya madini inakabiliwa na changamoto, ikiwemo mchango wake mdogo katika pato la taifa, madini kuendelea kuuzwa yakiwa ghafi na uchimbaji duni wa wachimbaji wadogo na kupendekeza kufanyiwa marekebisho kwa sheria na sera hizo.
Alisema kutokana na kutolewa kwa taarifa hiyo, tayari kikosi kazi kimeundwa ili kuangalia namna bora ya kutekeleza mapendekezo yaliyomo katika ripoti hiyo ya Tume ya Rais.
Hata hivyo, wadau mbalimbali wanalalamikia kasi ndogo ya serikali kupeleka muswada wa sheria hiyo bungeni ili uweze kujadiliwa na kisha kupitishwa ili uweze kutumika kuongoza sekta hiyo muhimu.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ambaye alikuwa ni mmoja wa wajumbe wa Tume ya Jaji Bomani, jana aliliambia gazeti hili, kuwa wakati tume hiyo ilipokuwa ikifanya kazi zake, ilibaini mapungufu mengi kwenye sekta ya madini, mapungufu ambayo yamesababisha serikali kukosa mabilioni ya fedha.
Alifichua kuwa makampuni ya madini yamekuwa yakiinyonya Tanzania kwa kutumia njia mbali mbali, ya kwanza ikiwa ni kulipa mrahaba mdogo kuliko hali halisi na pili ni kupitia msamaha wa kodi ya mafuta ambao makampuni hayo yamepewa na serikali.
Alifafanua kuwa kwa utaratibu wa sasa makampuni ya madini yanalipa mrahaba kwa kiwango cha asilimia 3 tu tena baada ya kuondoa gharama zote za uzalishaji na nyinginezo.
Alisema utaratibu huo umekuwa ukiisababishia serikali kupata mapato kiduchu ikilinganishwa na faida kubwa ambayo makampuni ya uchimbaji madini yamekuwa yakipata.
Zitto alisema kutokana na kutumika utaratibu huo wa kinyonyaji, katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 1998 hadi 2008, serikali ilipoteza zaidi ya sh. 883, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko hata misaada inayotolewa na Umoja wa Ulaya (EU) kwa Tanzania.
Kuhusu jinsi msamaha wa kodi ya mafuta kwa makampuni ya uchimbaji wa madini unavyolikosesha taifa mapato mengi, Zitto, alisema kwa kipindi cha mwaka 2005/2006, zaidi ya sh. 32 bilioni zilipotea kutokana na msamaha huo, huku makampuni hayo katika kipindi hicho yakilipa sh 23 bilioni tu kama mrahaba.
Aliongeza kusema kuwa katika kipindi cha mwaka 2006/2007 serikali ilikosa zaidi ya sh. bilioni 59 kutokana na msamaha huo, huku makampuni hayo yakilipa sh. bilioni 25 tu kama mrahaba katika kipindi hicho.
Mbunge huyo, alisema kwa kipindi cha mwaka 2007/2008 serikali ilikosa tena zaidi ya sh bilioni 91, huku makampuni hayo yakilipa sh bilioni 28 tu kama mrahaba.
``Ukiangalia takwimu hizi utaona kwamba makampuni hayo yamesamehewa kiasi kikubwa cha kodi huku yenyewe yakiilipa serikali kiasi kidogo tu cha fedha kama mrahaba, hivyo utaona serikali inapoteza mabilioni ya fedha kutokana na msamaha, huku makampuni yakitengeneza faida kubwa`` alifafanua.
Alieleza kuwa serikali kuyaachia makampuni ya uchimbaji wa madini kutumia umeme wao, pia kunalikosesha Shirika la Umeme nchini (Tanesco) mabilioni ya fedha kutokana na kushindwa kuyauzia umeme makampuni hayo.
Zitto, alieleza kuwa Tume ya Jaji Mark Bomani baada ya kubaini mapungufu mengi katika sekta ya madini, katika ripoti yake iliyoitoa baada ya kukamilisha kazi yake, ilitoa mapendekezi kadhaa ya kufanyiwa kazi na serikali haraka.
Aliyataja mapendekezo hayo kuwa ni kubadilisha kiwango cha mrahaba kutoka asilimia 3 hadi 5 na kiwango hicho kitozwe kabla ya makampuni kuondoa gharama za uzalishaji na kufutwa kwa msamaha wa ushuru wa mafuta kwa wawekezaji.
Pendekezo jingine ni kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Madini ambao utasaidia maendeleo ya sekta hiyo na jingine ni kutaka kiasi cha fedha za mrahaba ziende moja kwa moja kusaidia maendeleo ya vijiji vyenye migodi.
Jingine ni kutungwa kwa sheria mpya ya madini na kuifanyia marekebisho sera ya madini nchini na pia uwekwe mkakati wa kuhakikisha sekta ya umeme nchini inasaidia maendeleo ya sekta ya madini.
Hata hivyo, mbunge huyo, alionyesha kutoridhishwa na kasi ndogo ya serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria ya madini, akisema kuwa hali hiyo inaligharimu taifa kuendelea kupoteza fedha nyingi bila ya sababu za msingi.
``Muswada wa sheria hii kwanza ulikuwa uletwe na serikali bungeni Februari mwaka huu lakini haukuja, sasa tumeambiwa utaletwa kikao kijacho cha bunge, hata hivyo tunatarajia kikao kijacho cha bajeti serikali itatangaza mabadiliko makubwa kwenye sekta ya madini`` alisema.
Alitoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kuishinikiza serikali iharakishe kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Jaji Bomani ili taifa lisiendelee kupoteza fedha zaidi.
Sheria ya madini iliyopo sasa ambayo ilipitishwa na bunge mwaka 1997 inaelezwa imechangia kwa kiasi kikubwa kulisababishia taifa hasara ya zaidi ya dola za Marekani milioni 883kutokana na mapungufu yake.
Katika kipindi hicho, bunge lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali za Fedha, ambayo ndiyo iliyoweka msingi wa sheria za kodi za madini, ambazo hazikujali maslahi ya taifa na badala yake kuwanufaisha zaidi wawekezaji.
Kwenye sheria hii kuna kipengele cha asilima 15 kinachosema baada ya kampuni ya uchimbaji madini kutoa gharama zake za uzalishaji, inaruhusiwa kuongeza asilimia nyingine 15 ya gharama hizo na kutokana na sheria hiyo toka mwaka 1997 hadi 2007 kikiwa ni kipindi cha miaka 10 imeiingizia hasara serikali ya dola za Marekani milioni 883 sawa na sh trilioni 1 za Tanzania kwa kiwango cha sasa cha kubadilisha fedha, endapo fedha hizo zingekusanya zingesaidia mambo mbalimbali ya maendeleo.
Hatua hiyo ilimfanya, Basil Mramba, wakati huo akiwa Waziri wa Fedha, apeleke bungeni muswada wa sheria wa kuifuta na baadaye kuridhiwa na bunge, lakini mwaka mmoja baadaye 2002, Mramba huyo huyo alipeleka tena muswada wa sheria wa kutaka sheria hiyo irudishwe na wabunge waliokuwa bungeni kipindi hicho wakaipitisha.
Kupitishwa kwa sheria kuliyafanya makampuni ya uchimbaji madini kuchelewa kulipa kodi kutokana na kupewa muda mrefu wa kufanya hivyo.
Kwa mfano kampuni ya uchimbaji madini ya Bulyanhulu iliyoanza uchimbaji mwaka 1999, itaanza kulipa kodi mwaka 2019, hii ina maana kuwa itaanza kulipa kodi mwaka wa mwisho wa urais wa awamu ya tano, kampuni nyingine ni ya Anglo-Gold iliyoanza kuchimba mwaka 2002 lakini itaanza kulipa kodi mwaka 2012 na kampuni ya madini ya Resolute ya Nzega inaweza isilipe kabisa kodi kwani madini ya dhahabu iliyokuwa ikichimba katika eneo hilo yamemalizika kabla ya kipindi chake cha kuanza kulipa kodi hakijafika.
* SOURCE: Nipashe
1 comment:
ingawa wengi wetu hatukubaliani na hali hii ya ufisadi hapa kwetu tanzania, lakini bado tumeshindwa kubuni mbinu ya pamoja ya kuweza kuwaunganisha watu wote katika harakati hizi za kupambana na huu ufisadi. kukosekana kwa nguvu ya pamoja na uelewa mdogo wa wananchi walio wengi ni vigezo ambavyo wanavitumia viongozi wenye nia ya kutafuna nchi hii mpaka mwisho. kipindi kama hiki vyama vya kiraia vilipaswa viwe mstari wa mbele katika mapambano haya, lakini kutokanana na sheria za nchi zilizowekwa kiujanaja na watala vimeshindwa kufanya hivyo badala yake CSO's wameendelea kuwa kupiga kelele pembezoni na watawala kuendeleza ufisadi bila woga. nyakati zitafika wenye inchi watakapoamka, ole kwao viongozi wasio waadilifu!
kila la kheri.
Post a Comment