Thursday, April 9, 2009

Hatufiki popote bila kuwekeza kwenye elimu ya taifa

NIMESHAWISHIKA kuchangia katika mjadala unaoendelea kuhusu sekta ya elimu nchini. Katika hoja zangu nitaongozwa na dhana niipendayo ya maslahi ya umma (public good au the greater good).

Katika hitimisho nitajaribu kueleza ni kwa vipi mfumo wa mikopo ya elimu ya juu nchini unaweza kuchochea hulka za ufisadi miongoni mwa wasomi na wataalamu.

Kwa bahati nzuri, Tanzania imejitahidi kujenga na kuendeleza misingi ya elimu. Hadi sasa tuna idadi kubwa ya shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu. Kwa maana hiyo, maendeleo ya elimu peke yake si kigezo tosha cha kuleta maendeleo ya taifa.

Mwaka 2002 Rais Jacques Chirac wa Ufaransa alisema: “Hatuwezi kupata maendeleo ya jamii bila kuzalisha mali, na mali haiwezi kuzalishwa bila elimu na uwekezaji.”

Rais Chirac hakusema tuhangaikie kupata elimu peke yake, bali alituasa kuhusu kigezo kingine muhimu ambacho ni uwekezaji. Na hapa ndipo tunastahili kujiuliza na kutafakari kikamilifu iwapo elimu yetu inafuata misingi ya uwekezaji.

Inawezekana tukapata jibu la haraka kwamba upo uwekezaji wa kutosha, kwa maana kwamba tunaingiza fedha na rasilimali katika miradi ya elimu, tunazalisha wataalamu wengi, tunafanya utafiti mwingi, na pia tunarejesha fedha zinazokopeshwa kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Lakini pamoja na yote hayo, bado hatujapata maendeleo. Rasilimali zetu bado hazitumiki kikamilifu, na elimu yetu bado ina matatatizo. Wakati tunajiuliza, tunaweza kujifunza kutoka kwa majirani zetu kama Uganda.

Mwaka 2007, Rais Museveni wa Uganda alisema: “Japokuwa serikali yetu imewekeza sana katika elimu ya msingi, na sasa katika elimu ya sekondari, tunahitaji jitihada zaidi katika kuongeza ubora. Nimeelezwa kuwa tatizo letu katika sekta ya elimu si fedha, bali ni ukosefu wa ufanisi katika kutengeneza mazao ya akili, ambayo yana thamani kubwa zaidi kuliko mazao ya kawaida”.

Kulingana na maoni hayo ya Rais Museveni, umasikini wa taifa unakomaa kutokana na uwekezaji hafifu katika elimu au taaluma. Kiini cha tatizo hili ni hulka za ubinafsi au fikra finyu katika taaluma.

Undani wa jambo hili unapatikana pia toka kwa Rais wa zamani wa Marekani, Theodore Roosevelt ambaye mwaka 1910 alisema: “Endapo elimu ya mtu yeyote haiongozwi na kurekebishwa na maadili thabiti, basi kadri mtu huyo atakavyoendelea kuongeza elimu yake ndivyo atakavyozidi kuwa mbovu, na ndivyo atakavyoendelea kuwa hatari zaidi katika jamii.

Roosevelt anaongeza: “Juhudi, elimu, au sifa zozote humfanya binadamu awe fedhuli mbaya zaidi iwapo zitalenga tu kutimiza haja zake binafsi za maendeleo katika mazingira ya uadui yanayopuuza maendeleo ya jamii nzima.”

Ufedhuli wa kukosa mwamko wa elimu ya taifa tunauona bayana katika kilio cha Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo ambaye mwaka 1999 alisema kwamba: “Ilifika wakati ambapo maafisa wa serikali walizama kabisa katika hulka ya ufisadi na kutothamini maadili ya uongozi, na walionyesha mwamko hafifu sana katika kushughulikia maendeleo ya jamii na maslahi ya umma.”

Miaka mitano baadaye kilio kama hicho kilisikika tena huko Guyana ambako Rais Bharrat Jagdeo alisema: “Watu waliokabidhiwa majukumu ya kuongoza nyanja mbalimbali za maendeleo wangeweza kuleta mafanikio makubwa zaidi kama wangejitahidi kuonyesha upendo kwa umma na kujali zaidi maslahi ya jamii nzima.”

Katika siku za karibuni wanasiasa, wabunge, wasomi, na wananchi wengi hapa Tanzania wametafakari matatizo ya ufisadi katika nchi yetu. Hata hivyo zipo athari kubwa zaidi za kifikra na kitaaluma ambazo bado hatujazibaini; ingawaja tayari zimejitokeza bayana.

Rais Barrack Obama wa Marekani, mwaka 2006, akiwa seneta, alisema: “Ufisadi unayo tabia ya kuchochea usugu wa matatizo makuu katika maisha ya jamii, kwani huvuruga upeo wa kufikiri na kutafakari jinsi ya kushughulikia majanga mbali mbali”.

Kadhalika, Obama alibaini kuwa “ufisadi hudiriki kupandisha juu zaidi ngazi au kamba ya kutokea katika dimbwi la umasikini, kiasi kwamba jitihada za kujinasua miongoni mwa wanyonge waliozama katika dimbwi hilo hulazimishwa daima kuwa ndoto zisizotekelezeka”.

Kama alivyobashiri Obama, hapa Tanzania tumeona bayana kwamba ufisadi umefanikiwa kudhoofisha mifumo yetu ya kufikiri, kujadili, kukubaliana, kuamua, na kutekeleza mikakati ya kutatua matatizo makubwa ya kitaifa, hasa katika eneo la nishati.

Hii ina maana kuwa hata kama fedha zote zilizochotwa na mafisadi zingerudishwa ghafla, au kama tukiamua kusamehe fedha hizo, bado tutabaki na ulegevu ulioletwa na sumu ya ufisadi katika kufikiri na kutatua matatizo.

Matokeo ya udhaifu huu ni kwamba tumefikishwa mahali ambapo tunaambiwa kuchagua kati ya kukumbatia ufisadi au kuzama katika giza totoro.

Kama tunakubaliana kwamba hatutaki ufisadi na pia hatutaki kuingia katika giza totoro, au matatizo mengineyo kama hayo, tutakuwa tumejenga imani kwamba ipo njia ya tatu ya kutokea, inayoweza kutupeleka katika hali ya afueni zaidi. Na njia hiyo ya tatu haiwezi kupatikana katika mazingira yoyote zaidi ya kuwekeza katika elimu ya taifa, ili kuifanya taaluma iwe rasilimali na mwongozo kwa ajili ya maendeleo ya taifa zima.

Mara nyingi sana tumejiuliza swali la kwa nini tunabaki masikini wakati tunazo rasilimali za kutosha bila kupata majibu ya uhakika. Nadiriki kusema kuwa jibu pekee ni kuwa bado nchi yetu haina ubunifu wa kitaaluma unaoweza kujenga mahusiano bora zaidi baina ya misingi ya maendeleo.

Mwalimu Nyerere alituasa vizuri sana kuhusu misingi ya maendeleo na umuhimu wa taaluma katika taifa. Lakini kwa bahati mbaya, Nyerere hakusema tangia mwanzo kuwa elimu ni mojawapo kati ya misingi mikuu ya maendeleo.

Hata hivyo, ni dhahiri kabisa kuwa Nyerere alitambua na kueleza bayana umuhimu wa elimu, na alitumia rasilimali nyingi za taifa kuimarisha elimu kama msingi wa maendeleo.

Naamini kuwa Mwalimu Nyerere asingeweza kamwe kusahau kutaja elimu miongoni mwa misingi mikuu ya maendeleo, na hii inanifanya niamini kuwa alichotaka tuelewe ni kwamba elimu ndiyo mama wa misingi yote ya maendeleo.

Hata hivyo, hatuwezi kuliacha jambo hili libaki katika ngazi ya hisia kwa muda wote. Tunayo nafasi na jukumu la kutafakari fikra za Mwalimu Nyerere katika mazingira ya sasa, na naamini kwamba Rais Kikwete tayari ameonyesha nia ya kutuongoza kuona kwamba elimu lazima ichukue nafasi ya kipekee katika harakati za maendeleo ya taifa.

Ili tuweze kuinua uchumi na maendeleo ya taifa ni lazima tuwekeze katika elimu kwa mtazamo wa kuunganisha nguvu za taaluma na utafiti katika kukuza na kuendeleza rasilimali na kila raia lazima achangie na afaidike.

Kuchangia gharama za elimu, kupatikana mikopo ya elimu ya juu toka serikalini, na kupanua miundombinu au taasisi za elimu ni baadhi ya mikakati inayoweza kulifanya taifa liwe na watu wengi wenye elimu na ajira, ambalo ni jambo lenye manufaa mengi.

Hata hivyo, haya yote bado hayatoshi kukamilisha lengo kuu la elimu katika maslahi ya taifa. Maendeleo ya taifa hayapatikani kutokana na kuwapo kwa idadi kubwa ya watu wenye ujuzi au wenye ajira, bali ni kutokana na michango ya ubunifu toka kwa watu ambao hudhamiria na kuwezeshwa kufika katika kilele cha malengo ya elimu.

Ni rahisi zaidi kufika katika kilele cha elimu, na ni rahisi zaidi kuyajua yale ambayo waliofika kileleni huonekana kuyafanya, kuyasema, au kuyaandika. Ni rahisi pia kupata vyeti na vyeo vinavyohusiana na sifa za elimu ya juu.

Jambo gumu ni jinsi gani mafanikio au malengo hayo yanaweza kupitishwa katikati ya maslahi binafsi, hadi kufikia upeo wa fikra na ubunifu wenye maslahi ya taifa.

Elimu ya juu nchini inaelekea kuongozwa na mikakati iliyo chini ya bodi ya mikopo ya elimu ya juu, yaani HESLB. Hata hivyo, hatuna budi kubaini kwamba mfumo huu wa mikopo unaathiri sana mchango wa elimu ya juu katika maendeleo ya taifa.

Hii ni kwa sababu mfumo huu unajenga hisia potofu kwamba wanafunzi katika vyuo vikuu wanagharamia au kulipia elimu yao, na kwa hiyo wanao uhuru wa kukidhi maslahi yao binafsi. Lakini ukweli ni kwamba HESLB haitoi mikopo kwa wanafunzi, na wala wanafunzi hawagharamii elimu yao. Kinachotokea ni kichekesho chenye hasara, ambacho ni kwamba serikali inatoa ruzuku ya elimu kwa wanafunzi, wanafunzi wanagharamia kuwapo kwa HESLB, na HESLB inasababisha wanafunzi wakosane na serikali na wakose mwamko wa kuchangia katika elimu ya taifa na maendeleo ya jamii.

Ili kuwekeza kikamilifu katika elimu, ni bora serikali iondokane na dhana ya mikopo ya elimu ya juu, na badala yake irudi katika mfumo wa ruzuku toka wizarani. Katika kukamilisha uwekezaji huo, serikali ianzishe utaratibu bora zaidi wa kutambua na kugharamia wanafunzi wenye mwelekeo wa kuendeleza elimu ya taifa kupitia mfumo wa ruzuku.

Kwa maana hii ni lazima serikali iwe tayari kutumia fedha za umma kuendeleza wasomi wanaoweza kuishauri katika jitihada za kendeleza rasilimali, kuokoa fedha, kujenga imani ya wananchi, kudumisha amani na kulinda maslahi ya vizazi vijavyo.

Kupitia mfumo wa ruzuku, serikali inaweza kutumia fedha zinazoitwa mikopo bila kuwa na migomo katika vyuo vikuu.

Hapo itawezekana kukusanya fedha zaidi kupitia ubunifu na usimamizi wa wataalamu wanaopata elimu. Badala ya kumdai mtaalamu arejeshe mkopo kwa miaka 20, mfumo wa ruzuku unaweza kumfanya asimamie vizuri uzalishaji au uokoaji wa fedha za umma kiasi cha kurejesha fedha hizo ndani ya mwaka mmoja, hasa katika sekta za madini, uvuvi na ukusanyaji wa kodi.

Licha ya kusimamia uzalishaji na kubuni mbinu za kuendeleza rasilimali za taifa, wataalamu hao na raia wote bado watawajibika kulipa kodi, na ambayo bado inaweza kujumuisha makisio ya marejesho ya ruzuku au mikopo hiyo inayotumika katika elimu ya juu.

Jambo la msingi hapa ni kwamba elimu ya taifa ni ubunifu wa ziada, ambao mtu anaweza akauficha iwapo amechukizwa na mfumo uliopo. Ili kuweka uwazi unaofaa, watu wenye vipaji lazima wagharamiwe na umma na kisha wahudumie umma.

Utaratibu wa sasa wa kupima utajiri wa kila mzazi na kumtaka alipie gharama za mtoto wake hautusaidii kujenga misingi ya elimu ya taifa. Badala yake, wananchi wenye uwezo kifedha wanastahili kuchangia zaidi katika elimu kupitia malipo ya kodi ya kila mwaka.

Iwapo hao wenye uwezo kifedha watalipa kodi kikamilifu, serikali itaweza kutoa ruzuku kubwa zaidi kugharamia elimu. Kadhalika mfumo huu wa kodi na ruzuku utawafanya matajiri wote wachangie elimu kila wakati, badala ya kusubiri waingize watoto wao katika vyuo vikuu.

Miongoni mwa matatizo makuu ambayo nahisi yameanza kujitokeza kutokana na sera za HESLB ni mfumuko wa kugushi vyeti vya kidato cha sita. Baada ya kutangazwa utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaopata daraja la kwanza na la pili tu, inaelekea hata wizi wa mitihani umepitwa na wakati. Badala yake, upo uwezekano kuwa tayari kuna wimbi baya zaidi la kugushi na kununua vyeti vya daraja la kwanza vya kidato cha sita, kama sehemu ya kutafuta mikopo ya HESLB.

Inawezekana tukawa na idadi kubwa ya wanafunzi walio mwaka wa kwanza katika vyuo vikuu ambao wamechaguliwa kwa kutumia vyeti vya aina hii. Sasa hivi wapo wanafunzi wengi sana ambao baada ya kupata daraja la nne katika kidato cha nne, wamebadilika ghafla na kupata daraja la kwanza katika mitihani ya kidato cha sita!

Uzoefu wangu unanilazimisha nifikiri kuwa jambo hili haliwezekani bila kugushi vyeti kwa mbinu kali, na wala si wizi wa mitihani.

Kwa hiyo, basi, bila kuwa na mfumo bora wa elimu na kuwekeza katika elimu, tutaendelea kutoa mikopo kwa watu ambao hata kidato cha nne hawajafika, mradi tu wamekaa mjini na kujua wapi vinatengenezwa vyeti vinavyoonekana kuwa halisi, nje ya taratibu za Baraza la Mitihani la Taifa.

Wilfred Kahumuza ni mdau wa sekta ya elimu nchini wa muda mrefu.

No comments: