KAULIMBIU ya Tamasha la Kigoda cha Mwalimu ni: Binadamu wote ni sawa, Afrika ni moja na Afrika ni lazima iungane.
Sina uhakika kama walioandaa tamasha hili, wanaichukulia kaulimbiu hii kama “wimbo” wa kuburudisha na kuchangamsha na baadaye maisha yanaendelea kama kawaida; au wanaichukulia kaulimbiu hii kama mvinyo; kuna msemo kwamba penye mvinyo pana ukweli!
Mvinyo ukitoka kichwani, ukweli unageuka uongo? Je, kaulimbiu hii ni kama tulizozizoea za wanasiasa? Wasomi wetu wanaamini kaulimbiu hii? Tamasha litaendeshwa kwa lugha gani? Kiswahili, Kiyoruba, Kinyarwanda na Kiganda, au Kiingereza na Kifaransa?
Kwa nini zisitumike lugha za Afrika, wakawapo “wasomi” wakatafsiri? Usomi, ni pamoja na kuzifahamu vizuri lugha zetu; kuzitumia lugha zetu kuelimishana na kuunda mshikamano. Bila hivyo tutagawanywa makundi makundi kwa kutumia lugha za kigeni na kuendeleza ukoloni mamboleo. Afrika haiwezi kuungana bila kuwa na lugha zake, fikra zake na falsafa yake. Afrika haiwezi kuungana kama tunaendelea kuimba wimbo bila matendo.
Ni wazi kwenye tamasha tutaimba mashairi na nyimbo, tutacheza ngoma na kuimba ngonjera. Tutakunywa mvinyo na kutema cheche za ukweli wote! La msingi na ambalo ni muhimu, ni kwamba nyimbo hizo, mashairi hayo na ngojera hizo zisipite kama mvua za masika. Zipande mbegu ya kuota, mbegu ya kuendeleza mawazo ya Mwalimu Nyerere, ya Umoja wa Afrika. Mvinyo tukaokunywa, utusukume kutema cheche cha ukweli usiogeukwa, ukweli wa kudumu, ukweli wa kujenga Umoja wa Afrika.
Mwalimu Nyerere, hakuimba wimbo wa Binadamu wote ni sawa, Afrika ni moja na Afrika ni Lazima iungane; hakutumia mvinyo ili aseme ukweli. Alitekeleza kwa matendo! Ndiyo maana wakati wa uongozi wake, Tanzania, ilikuwa kimbilio la kila mwanadamu. Wapigania uhuru walikaribishwa Tanzania na kuishi kama nyumbani kwao; walipotaka kutembelea nchi za nje kama Ulaya na kwingineko, walitumia pasi za Tanzania; walianzisha makambi ya mapambano hapa hapa Tanzania. Uganda, ilipopinduliwa na kutawaliwa na Iddi Amin, Mwalimu, alikataa kukaa kimya, alifanya uamuzi mgumu wa kuingilia kwenye mapambano ya vita vya Kagera. Hatukusikia lugha ya wahamiaji haramu wakati wa uongozi wa Mwalimu.
Sasa hivi ni kinyume. Watanzania tumeanza kujenga utamaduni wa ubaguzi, tena ubaguzi mbaya kabisa. Hivi karibuni Tanzania, tumekuwa na zoezi la kuwafukuza wahamiaji haramu kutoka Rwanda, Burundi na Uganda. Hawa tunaunganishwa na damu, na wengine tunazungumza lugha moja na utamaduni unaofanana, lakini tunateganishwa na mipaka ya kikoloni.
Hata hivyo, kwa nini tufukuzane, badala ya kushirikiana? Kwa nini tufukuzane wakati tunaimba wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki? Wakati tunaimba wimbo wa Umoja wa Afrika? Tutaungana bila kuishi pamoja?
Kwanini wahamiaji haramu, wasishawishiwe kuishi kwa vibali na kama wanafanya biashara au uwekezaji kwenye mifugo na viwanda, watozwe kodi na kuchangia pato la taifa? Kama mtu anaweza kuwekeza kutoka Marekani, kwa nini Warundi, Wanyarwanda na Waganda wasiwekeze? Kwa nini tusijenge daraja la kuunganisha Tanzania, Kenya, Burundi, Rwanda na Uganda na daraja hili likaendelea kutuunganisha na nchi za kuzini, kaskazini na magharibi mwa Afrika?
Tanzania haikuwa na ubaguzi. Serikali ya awamu ya kwanza hadi awamu ya pili haikuwa na dalili za ubaguzi. Msamiati wa “Wahamiaji haramu” hatukuufahamu! Mbegu ya ubaguzi imepandwa wakati wa serikali ya awamu ya tatu.
Mwaka 1997 Tanzania iliamuwa kuwarudisha kwa nguvu nyumbani wakimbizi wa Kihutu kutoka Rwanda. Hili lilikuwa ni zoezi la kikatili ambalo nililishuhudia. Kuna wakimbizi ambao walitembea zaidi ya kilomita 100 kwa miguu kuufikia mpaka wa Tanzania na Rwanda wakisindikizwa na wanajeshi.
Baada ya zoezi hili la kikatili, tulianza kusikia watu wakinyang’anywa uraia kwa vigezo vya kuangalia pua zao za Kitutsi na historia yao. Wale wenye asili ya Rwanda, Burundi na Uganda, walibaguliwa! Wengine walisombwa na kupelekwa kwenye nchi hizi bila utashi wao. Baadhi walikuwa wameishi Tanzania maisha yao yote tokea vizazi vya mababu kutokana na mipaka ya kikoloni.
Zoezi hili la wahamiaji haramu limeendelea hadi kwenye serikali ya awamu ya nne. Tanzania nchi iliyokuwa ikuuchukia ubaguzi, sasa inaongoza kwa vitendo vya kibaguzi.
Wakati ubaguzi huu unaota mizizi, wasomi wetu wanaopigia debe Umoja wa Afrika wako wapi? Ni kweli kwamba kuna baadhi ya wasomi wanaunga mkono Shirikisho la Afrika ya Mashariki; wangependa twende haraka kuuda shirikisho. Lakini pia kuna wasomi wanopinga kwa nguvu zote kuanzishwa kwa shirikisho na wengine wanakwenda mbali hata kuupinga Muungano wa Tanzania. Wangependa zirudi tena Tanganyika na Zanzibar!
La kushangaza ni kwamba baadhi ya wasomi hawa wanaopinga shirikisho na Muungano wetu, ni waumini wa Umoja wa Afrika! Wakisimama kuzungumza wanatetea umoja wa Afrika kwa nguvu zote. Ikifika wakati wa matendo, wanajionyesha walivyo! Wanahubiri wasiyoyaishi, wanahubiri wasiyoyapenda! Wanafiki!
Hivyo kuna haja wakati tunamkumbuka Mwalimu, na hasa tunapomkumbuka katika anga za kisomi, kuelezea jinsi wasomi, wa hapa na wa nje wanavyosaliti jitihada zilizoanzishwa na wasomi waliotangulia za kutetea na kuelezea umuhimu wa Umoja wa Afrika. Hapa Tanzania, tumemsaliti Mwalimu Nyerere; tumesaliti jitihada zake za kuwaruhusu Waafrika wote kuja na kuishi Tanzania, tumesaliti jitihada zake za kupigania ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika, tumesaliti jihudi zake za South-South Commission, tumesaliti juhudi zake za upatanishi wa mgogoro wa Burundi.
Kuna mwamko wa nchi za Afrika kupeleka askari wa kulinda amani kwenye nchi za Afrika zenye mapigano. Majeshi yamepelekwa DRC, Darfur, Somalia na kwingineko. Hata majeshi yetu yanashiriki. Hizi ni dalili nzuri, lakini haziondoi matatizo ya nchi husika. Haziondoi umasikini, haziondoi ujinga, hazijengi demokrasia na utawala bora. Kuna haja ya nchi hizi masikini, nchi hizi ambazo zina rasilimali nyingi kuungana ili ziwe na nguvu ya kupambana kwa pamoja.
Kama anavyosema Profesa Mwesiga Baregu: “ Kinachojitokeza baada ya kuchambua makubaliano na taratibu zilizopo ni kwamba mpaka sasa amani, ulinzi na usalama katika Afrika Mashariki unatawaliwa na maana finyu inayozingatia zaidi vyombo vya ulinzi na usalama.
Kwa kuwa mashambulizi ya nchi hizi kutoka nje hayatazamiwi, majeshi yataendelea kuelekeza nguvu zake katika kuthibiti migogoro na kukabiliana na maafa pale yanapojitokeza. Majukumu haya yatayasogeza majeshi ya ulinzi karibu sana na raia kuliko tulivyozoea.
Hili linaweza kuwa jambo zuri la kuleta amani ndani ya raia. Lakini vile vile linaweza kuleta madhara hasa pale ambapo majeshi haya hayajaandaliwa vizuri kwa majukumu haya mapya. Athari moja inaweza kuwa migongano kati ya raia na wanajeshi pale ambapo maslahi ya raia yanakinzana na ya wanajeshi. Athari ya pili inawezekana ikawa mgongano kati ya wanajeshi na askari hasa pale ambapo mipaka ya mamlaka inaingiliwa bila mwongozo maalum. Athari nyingine na kubwa zaidi inaweza kuwa kuingiza hofu ndani ya jamii na kujenga misingi ya udikteta au utawala wa kijeshi. Hili linaweza kuathiri sana haki za binadamu na raia na kurudisha nyuma mipaka ya demokrasia kwa kujenga jamii yenye woga wa ki-siasa.
“Katika hali kama hii kuna haja ya kutambua kimsingi kwamba hiki ni kipindi cha mpito na kwamba ni muhimu kufanya maadalizi ya kukabili mipito hii kwa wakati mmoja. Mchakato wa kutoka kwenye dola ndogo ndogo na hafifu kuelekea shirikisho la Afrika tukipitia shirikisho za kanda kama Afrika ya Mashariki.
Kuna ulazima wa kuelewa ki-msingi na kutangaza kwa uwazi kwamba suala la nchi za Afrika kufanya juhudi pevu za kuugana si la hiari lakini la ulazima kama Afrika na Waafrika wataendelea kuwapo, kujilinda, kulinda mali zao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya ulimwengu.
Hatua hii itahitaji upeo, ujasiri na uwezo wa kuthubutu kubadilisha historia ya Afrika.”
Tunahitaji kuunganisha nguvu, tunahitaji mifumo ya kulifanya Bara la Afrika kuwa bara lenye nguvu kiuchumi, kisiasa na kielimu. Tunahitaji mifumo ya kulifanya Bara la Afika kuwa na watu wenye afya njema na wanaoishi kwa miaka mingi. Tunahitaji mifuno ya kulifanya Bara la Afrika kuwa na imani iliyojengwa na kusimikwa juu ya udongo wa Afrika. Mungu, aliyeiumba Afrika, ndiye huyo huyo aiyeshusha imani yake kwake. Haiwezekani Mungu, akaiumba Afrika na kuicha yatima hadi zilipokuja dini za kigeni.
Tunahitaji kuwa na vyuo vikuu vya Afrika, vinavyofundisha kwa kutumia lugha za Afrika, na kufundisha falsafa ya Afrika. Tunahitaji kujijengea uwezo wa kuweza kupamba na utandawazi. Tishio kubwa la Afrika ni utandawazi, kama anavyosema, amini na kufundisha Profesa Baregu.
Kwa maoni yake silaha ya kupambana na utandawazi ni umoja. Anakataa yale mawazo kwamba utandawazi ni kijiji. Kwa maoni yake, kijiji daima ni maeneo yenye usalama. Mtu ukifika kijijini unakuwa unatarajia kupata malazi, chakula na maji ya kunywa. Utandawazi hauna undugu wa kijiji, na hasa kijiji cha Afrika.
Kwake yeye utandawazi ni pori! Na ili mtu upite salama kwenye pori ni lazima uwe na silaha, vinginevyo unakuwa kitoweo cha simba! Profesa Baregu, anatupatia mtizamo mpya kabisa wa kufananisha utandawazi na pori.
Hivyo tusiimbe wimbo wa Umoja wa Afrika, tusiimbe wimbo wa Binadamu wote ni sawa, bali tutekeleze falsafa hii. Tusimkumbuke Mwalimu Nyerere, kwa mihadhara mizuri ya kupendeza, bali tuunde mifumo ya kutuwezesha kutekeleza falsafa hii ambayo ni urithi wetu mkubwa.
Mwalimu aliwaheshimu binadamu wote na alifanya jambo hilo kwa matendo! Mwalimu aliamini kwamba Afrika ni lazima iungane; na alifanya hivyo kwa matendo kwa kufungua milango ya Tanzania kwa kila Mwafrika. Kigoda cha Mwalimu kiwe taa ya kutuongoza hadi kufikia Umoja wa Afrika. Mungu Ibariki Afrika! Mungu wabariki watoto wa Afrika.
No comments:
Post a Comment