Thursday, April 2, 2009

Tuzo ya Kilango na kauli za akina Kingunge


NIUNGANE na Rais Jakaya Kikwete kumpongeza Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango Malecela, kwa kutunukiwa Tuzo ya Mwanamke Jasiri kwa mwaka 2009 ya Serikali ya Marekani, kupitia Ubalozi wake nchini.

Kilango anafungua dimba kwa wabunge wanawake kuchochea mabadiliko nchini bila woga. Anazidi kuwajengea imani wanawake mbele ya umma wa Watanzania kwamba ìinawezekana timiza wajibu wako. Hongera Kilango ambaye baadhi ya Watanzania wamempachika jina la Mama Socratesî kwa kuzingatia msimamo mkali wa haki, wa mwanafalsafa huyo wa Kigiriki.

Bila shaka, kati ya mambo yaliyomfanya mbunge huyo kuonekana kuwa mwanamke jasiri kwa mwaka 2009 ni kauli zake nzito za kupiga vita ufisadi akiamini kuwa ni sehemu ya vikwazo dhidi ya ahadi ya kuwaletea Watanzania maisha bora.

Amekuwa akipambana kwa hoja, bila kujali kuwa anapambana na watu wenye nguvu za kifedha na madaraka, nguvu ambazo siku moja zinaweza kumdhuru. Hakika Taifa linastahili kujivunia Anne Kilango Malecela na si wananchi wa Same Mashariki pekee.

Kwa wanaokumbuka mjadala dhidi ya ufisadi wa shilingi bilioni 133 kutoka katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) bungeni, bila shaka sauti ya Anne Kilango bado haijafutika vichwani mwao. Sauti iliyoshiba hoja, iliyotikisa wahusika wa ufisadi na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuamsha na kuwaongezea ari Watanzania wengi.

Ninukuu baadhi ya kauli za Anne Kilango bungeni. Kauli ambazo zinathibitisha kuwa alikuwa akizungumza kwa uchungu na si kwa unafiki kama ilivyo kwa viongozi wengi wa kisiasa nchini. Nukuu hizi naamini zitasaidia kumfahamu zaidi Anne Kilango.

Tuanze na nunukuu yake kutoka kwa mwanafalsafa Socrates wa Ugiriki. Hapa Anne Kilingo alimnukuu mwanafalsafa huyo akisema; ìWatu wengi maarufu duniani wako tayari kufa kwa ajili wanachokiamini kuwa ukweli na haki.î

Lakini mbali na kumnukuu Socrates, Anne Kilango aliweka bayana msimamo wake akisema; ìTusiposimama imara tutakuwa taifa lisiloheshimika. Ukiona kakikundi kadogo kanahodhi fedha za taifa na sisi wabunge tupo, it is wrong (ni kosa).î

"Ulinzi wa fedha za Watanzania kwa muda mrefu uliachwa wazi. Watu waliingiaje wakachukua fedha za EPA. Hizi ni fedha za wananchi, ni mapato ya ndani, bila kuogopa kitisho chochote, bila kurudishwa fedha za EPA hapa patakuwa padogo, sitakubali kukana falsafa ya Socrates, haki na ukweli.

ìHizi ni fedha za wananchi wa Same Mashariki, fedha za wananchi wa Igunga, fedha za wananchi wa Kigoma Mjini, ni fedha za wananchi.î Kwa wafuatiliaji wa mijadala bungeni bila shaka sauti ya Anne Kilango itakuwa bado inazungumza ndani ya vichwa vyao na hasa kwa kukumbuka nukuu hizo.

Shukrani Ubalozi wa Marekani kwa kutambua mchango wa Kilango katika vita dhidi ya ufisadi nchini. Ni dhahiri, Kilango anastahili Tuzo hiyo ingawa pia ndoto yake ya kuhakikisha watuhumiwa wote wa EPA wanafikishwa katika vyombo vya sheria haijatimia.

Lakini Tuzo hii ina maana gani kwa Watanzania? Kwanza, tujadili maana ya Tuzo hii kwa kumtazama Rais Jakaya Kikwete. Kama nilivyogusia awali, ndoto ya Anne Kilango Malecela kupigania mafisadi wote wa EPA kuchukuliwa hatua haijatimia, kiongozi wa kusimamia au kushinikiza ndoto hiyo itimie ni Rais Kikwete.

Ukweli ni kwamba Tuzo hii inatukumbusha kuwa kama Taifa la watu wanaochukia ufisadi kwa kuungwa mkono na nchi rafiki kama Marekani bado wezi wa EPA wote hawajafikishwa mahakamani. Hapa nazungumzia kampuni kama ya Kagoda Agriculture Ltd, ambayo pekee inatajwa kuchota Sh bilioni 40, ikiwa ndiyo kampuni kiongozi katika wizi huo kwa kuchota fedha nyingi zaidi.

Ingawa awali nimeanza kwa kuungana na Rais Kikwete katika kumpongeza Kilango kwa kutunukiwa Tuzo, lakini naamini pongezi za Rais Kikwete kwa mbunge huyo bado hazijakamilika. Pongezi za Rais zitakamilika tu pale mafisadi wote wa EPA watakapofikishwa mahakamani, tofauti na hali ilivyo sasa.

Ikumbukwe kuwa wakati Rais Kikwete akijivunia Anne Kilango Malecela kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumpongeza kwa Tuzo hiyo, baadhi ya watendaji serikalini wamekuwa wakitoa kauli za kutia shaka kuhusu uwezo wao kiutendaji, hususan vyombo vya upelelezi.

Mara kwa mara tumekuwa tukiwasikia watendaji hao wakisisitiza kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuifikisha mahakamani kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd. Ni katika mazingira haya Tuzo ya Kilango inatukumbusha kuwa bado juhudi za Serikali ya Kikwete katika kuwashughulikia wezi waliokiri kuiba fedha za umma zinahitaji kasi ya nyongeza.

Jambo la kutia shaka ni kwamba zipo dalili za mazingira ya ushirikiano kati ya wahusika halisi wa wizi wa Sh bilioni 40 kupitia Kagoda na baadhi ya watendaji serikalini. Haiingii akilini kwa watendaji wa serikali, hususan wapelelezi, kutueleza kuwa ushahidi hautoshi na wakati huo huo serikali hiyo hiyo ikikiri kuwa imeibiwa hizo fedha na kampuni hiyo.

Ukweli ni kwamba utashi wa dhati serikalini katika kuichukulia hatua kampuni ya Kagoda ni wa kutilia shaka. Ndiyo maana wapo baadhi ya Watanzania wanaoamini kuwa kuna mchezo wa ìdanganya totoî katika kushughulikia sakata la EPA.

Itoshe tu kusema kwamba Tuzo ya Kilango ni changamoto kwa Rais Kikwete kufanikisha vita dhidi ya ufisadi serikalini, vinginevyo pongezi zake kwa mbunge huyo hazitakuwa na nguvu ya kimantiki mbele ya umma.

Rais Kikwete anapaswa kuwa imara zaidi katika suala hili vinginevyo mbali na pongezi zake kuonekana kutokuwa na nguvu za kimantiki mbele ya umma, lakini pia atakuwa akikiweka chama chake katika wakati mgumu katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2010.

Kwa bahati nzuri, wanachama wenzake ndani ya CCM pia wanatambua ugumu utakaokuwapo katika uchaguzi mwakani kama wezi wote wa EPA wote hawatafikishwa mahakamani.

Swali kubwa la kuendelea kujiuliza ni kwamba, kwa nini watendaji serikalini wawe mstari wa mbele kunadi kuwa hakuna ushahidi wa kutosha katika kuifikisha mahakamani Kagoda, ilihali wakikiri kuwa wizi umefanyika na kampuni hiyo imerejesha fedha ilizoiba?

Lakini hiyo ni sehemu moja kuhusu changamoto zinazojitokeza kwetu kama Taifa baada ya Tuzo hii ya Kilango, sehemu ya pili inahusu baadhi ya wanasiasa ndani ya CCM. Wanasiasa hawa tunaweza kuwagawa katika makundi mawili.

Kundi la kwanza ni lile lililokuwa likichukizwa na mwenendo wa Anne Kilango na wabunge wengine walioko mstari wa mbele kupinga ufisadi hadharani. Kundi hili limekuwa likitumia majukwaa ya kisiasa kurudisha nyuma juhudi za akina Kilango na wenzake, na baadhi katika kundi hili waliandika katika magazeti kuwashambulia akina Kilango.

Kwa mfano, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, Muhammed Seif Khatib, mwaka jana aliwahi kuandika katika safu yake ya Kipanga inayochapichwa katika gazeti la Mzalendo, akijenga dhana kwamba Anne Kilango na wenzake hawastahili kuendelea kuwapo CCM. Khatib alijenga hoja yake akisema kundi hilo la wanaopinga ufisadi ni sawa na chawa katika upindo.

Lakini sauti nyingine zilizokuwa zikipinga juhudi za Anne Kilango na wenzake ni kwa kutumia mlango wa nyuma ni pamoja na mzee Kingunge Ngombale-Mwiru, bila kumsahau Peter Kisumo na wengine, tena baadhi wakiwa ni wabunge wa majimbo, ambao siwezi kuwataja kutokana na ufinyu wa nafasi.

Hawa walisimama katika majukwaa wakipaza sauti za kuwatisha au kuwakatisha tamaa akina Kilango. Nakumbuka kauli ya Kingunge, mwishoni mwa Agosti, mwaka jana, wakati akipokea maandamano ya CCM Mkoa wa Dodoma, yaliyolenga kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete kwa hotuba yake aliyoitoa bungeni mwezi huo.

Kingunge alinukuriwa na baadhi ya magazeti akisema; ìUmezuka mtindo hivi sasa, wapinzani wanaibua hoja ili kuwakamata vizuri CCM, wanasema hoja hii ni ya kitaifa (ufisadi), kwa maslahi ya wananchi hivyo viongozi wetu wa CCM nao wanajikuta wakiingia katika mijadala hiyo bila kujua kwamba wanachofanya ni kukidhoofisha chama.î

Katika mkutano huo Kingunge aliweka bayana kukerwa na wabunge pamoja na wana-CCM waliokuwa wakishabikia vita dhidi ya ufisadi na hasa ufisadi uliofanywa na baadhi ya viongozi katika kashfa ya kampuni ya kitapeli ya Richmond pamoja na EPA.

Lakini pia Kingunge alionekana kuchukizwa na wapinga ufisadi wanavyopambwa na magazeti akisema; ìUmaarufu wa magazetini haufai, ni wa kupita tu, na inapofikia kipindi fulani hata hayo magazeti yanakusahau, wapo tuliowaona lakini wako wapi sasa.î Aliweka bayana msimamo wake huo kuhusu magazeti bila kutambua kuwa hadhi ya kiongozi fulani inadumu na kuheshimika daima kwa kutegemea mwenendo wa mhusika.

Kwa wakati ule, nilitafsiri kauli hiyo kuwa ni haramu dhidi ya ustawi wa utawala bora unaozingatia misingi ya uwazi, kuwajibika na kuwajibishana. Nilitumia safu hii japo katika gazeti jingine kuandika kumpinga mzee Kingunge, katika makala iliyopewa kichwa cha habari ìRichmond na vituko vya Kingunge uzeeniî

Wiki iliyopita baada ya Anne Kilango kutunukiwa Tuzo, moja kwa moja nikarejea kauli ya Kingunge na wenzake. Nikajiuliza, nini maana ya Tuzo hii ya mbunge huyo kwa CCM? Nilijiuliza hivyo huku nikikumbuka kauli za kukatishana tamaa kwamba ìkeleleî za akina Kilango dhidi ya ufisadi ilikuwa ni kuibomoa CCM na kuimarisha upinzani.

Nini maana ya Tuzo hiyo kwa CCM? Tuzo hii inaweza kuwa na maana pana zaidi kwa CCM, lakini kubwa zaidi ni kuthibitisha kuwa ndani ya chama hicho wapo viongozi wachache wanaopigania ustawi wa Watanzania wote. Lakini pia, kauli za Kingunge na wenzake sasa zinajidhihirisha namna zinavyopwaya si tu mbele ya Watanzania, bali hata katika Jumuiya ya Kimataifa.

Sasa ni dhahiri kuwa msimamo wa akina Kingunge na wenzake kwamba wabunge wa CCM wamekuwa wakidandia hoja za upinzani si sahihi. Ni hoja zilizojengwa katika misingi ya propaganda za kuwalinda watuhumiwa wa ufisadi wanaovaa sare za CCM na kuhudhuria vikao vya juu vya chama hicho.

Hongera Anne Kilango Malecela, Watanzania na jumuiya ya kimataifa sasa wanakutambua kuwa wewe ni mpenda haki anayechukia maasi dhidi ya maadili. Wewe ni kiongozi jasiri, usiyezimia (kupoteza fahamu) kwa kukemewa au kutishwa na mafisadi.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

No comments: