Tuesday, June 19, 2012

Zitto Aichana Bajeti

ATAJA KASORO ZAKE, ASEMA HAINA UNAFUU KWA WANANCHI WA KAWAIDA

Neville Meena, Dodoma
 WAZIRI Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe jana aliwasilisha bungeni bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani kwa mwaka wa fedha 2012/2013, huku akibainisha kasoro lukuki katika bajeti ya Serikali ilioyowasilishwa Alhamisi iliyopita.Bajeti ya Zitto ilitanguliwa na hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Ofisi ya Rais – Mipango, Christina Mughwai ambaye pia aliweka wazi kile alichokiita udhaifu wa Serikali katika kuitekeleza mipango yake ya kiuchumi, hali ambayo inasababisha umaskini kwa wananchi.

Hotuba zote mbili, ya Zitto na Lissu, zilisema licha ya Serikali kutangaza kwamba bajeti ya 2011/12 ilikuwa ya kupunguza makali ya maisha, hakukuwa na nafuu yoyote kwa wananchi kwani maisha yameendelea kupanda.

Pamoja na kupendekeza njia kadhaa za kupanua wigo wa mapato ya Serikali, wapinzani wametaka kufanywa kwa ukaguzi wa deni la taifa, ili kubaini chanzo cha Serikali kukopa na kuweka wazi jinsi fedha hizo zilivyotumika hadi kufikia Sh22 trilioni.

Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni katika hotuba yake alisema mapato ya Serikali yanaweza kuongezwa kwa Sh2.885 trilioni, hivyo kupunguza utegemezi wa mikopo ya kibiashara ambayo imekuwa ikiligharimu taifa kiasi kikubwa cha fedha.

Vyanzo vya kodi na kiasi cha fedha kwenye mabano alivyopendekeza ni marekebisho ya kodi za misitu ikiwamo mkaa (Sh130.8 bilioni), Kupunguza misamaha ya kodi, kuzuia ukwepaji kodi na udanganyifu wa biashara ya nje (Sh742.74 bilioni), Mauzo ya hisa za Serikali (Sh415.55 bilioni), Marekebisho ya kodi Sekta ya Madini na asilimia 25 ya Mauzo ya Madini Nje (Sh578.36 bilioni) na Marekebisho ya Kodi na Usimamizi bora wa Mapato Kampuni za Simu (Sh502.26 bilioni).

Mapendekezo mengine ni Marekebisho ya Kodi ya Tozo ya Kuendeleza Stadi (Sh243.52 bilioni), mapato ya wanyamapori (Sh61.64 bilioni), kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta kwa kampuni za madini (Sh44.9 bilioni), Usimamizi wa mapato ya utalii (Sh51.75 bilioni), Kuimarisha biashara Afrika Mashariki (Sh 114.15 bilioni).

Zitto alisema kama wapinzani wangekuwa madarakani wangekusanya kiasi cha Sh15 bilioni sawa na ile ya Serikali, lakini tofauti ni hatua ya kutenga asilimia 35 ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa bajeti kutoka asilimia 42.37 za Serikali hadi asilimia 21.3.
     
Deni la Taifa

Kuhusu deni la Taifa, mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alisema Serikali haipaswi kuendelea kukopa, kwani taarifa rasmi za kibenki na ukaguzi wa hesabu zinaonyesha kwamba deni hilo linakua kwa kasi tofauti na maelezo ya Serikali kwamba linahimilika.

“Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa Deni la Taifa linazidi kuongezeka kwa asilimia 38 kutoka Sh10.5 trilioni mwaka 2009/2010 hadi Sh14.4 trilioni 2010/2011. Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Deni la Taifa limefikia Sh20.3 trilioni mpaka ilipofika mwezi Machi mwaka 2012,”alisema Zitto na kuongeza:

“Ukisoma taarifa ya Mwezi wa Mei 2012 ya Benki Kuu ya Tanzania, Deni la Taifa sasa limefikia Sh22 trillion. Suala hapa sio ustahmilivu wa Deni kama inavyodai Serikali, bali ni kwamba tunakopa kufanyia nini?”

Alisema hesabu za bajeti ya Serikali ya 2012/13 inayopendekezwa zinaonyesha kwamba Serikali bado ina mpango wa kukopa kwa ajili ya kugharamia matumizi ya kawaida ambayo hayazalishi wala kutozwa kodi.

“Hatutaki mikopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari n.k. Tuchukue mikopo kuwekeza kwenye miradi itakayokuza uchumi na kuzalisha kodi zaidi,” alisema.

Kuhusu mfumuko wa bei, Zitto alikosoa hatua zinazopendekezwa na Serikali kukabiliana nao, kwamba ni zile zilizoshindwa katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, mwaka huu.

Alisema hatua hizo ambazo ni kutoa vibali kwa wafanyabiashara vya kuagiza mchele na sukari bila kutoza kodi, haziwezi kusaidia kwa kuwa hatua kama hizo zilipochukuliwa awali zilisababisha bei ya bidhaa hizo kuongezeka.

“Baada ya hatua hii bei ya sukari ilipanda kutoka Sh1,700 mpaka 2,800 kwenye maeneo mengi nchini… Serikali inachukua hatua zile zile kwa tatizo lile lile ikitegemea matokeo tofauti,” alisema Zitto.

Alirejea pendekezo la mwaka jana kwa Serikali kutoa vivutio kwa wakulima wadogo kuzalisha chakula kwa wingi akisema kuwa hatua hiyo pekee ndiyo itapunguza mfumuko wa bei.

“Hakuna mbadala wa kudhibiti mfumuko wa bei zaidi ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwekeza kwa wananchi wetu. Serikali inafikiria uzalishaji utaongezeka kwa kusaidia wakulima wakubwa ambao watageuza wananchi wetu kuwa manamba na vibarua ndani ya nchi yao,” alisema na kuongeza:

“Tuwekeze kwa watu wetu vijijini ili waongeze uzalishaji na kwa kufanya hivyo mfumuko wa bei ya chakula utakuwa historia. Hakuna mwarobaini wa kupanda kwa bei za vyakula isipokuwa kilimo”.

Kampuni za Simu

Katika hatua nyingine, kambi hiyo imepinga pendekezo la nyongeza ya asilimia mbili katika muda wa maongezi ya simu kwa maelezo kwamba hatua hiyo itamkadamiza mwananchi wa kawaida, kwa kuwa itaongeza gharama za simu.

“Hoja ya wananchi hapa ni kwamba Kampuni za Simu za mkononi hazilipi kodi ya kutosha na hasa Kodi ya Makampuni (corporate tax). Kampuni za simu zinapaswa kulipa kodi ya mapato na sio kukandamiza wateja kwa ushuru wa bidhaa, ilihali huduma zenyewe za simu hazina ubora,” alisema.

“Waziri Mkuu alipokuwa anafunga Bunge la Bajeti mwaka 2011 alitangaza kampuni ambazo ni walipa kodi wakubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Katika orodha hiyo kulikuwa na kampuni moja tu ya simu za mkononi, AirTel.”

Katika hatua nyingine, aliitaka Serikali kutoa maelezo bungeni kuhusu sababu za kutumia fedha zilizorejeshwa kutokaana na ununuzi wa rada bila fedha hizo kupata idhini ya Bunge kwa mujibu wa sheria.

Bajeti ya 2011/2012

Zitto alisema hatua za Serikali kutumia Sh296 bilioni na dola za Marekani milioni 183 kwenye Umeme, pia Sh27 bilioni kununua mahindi na kusambaza kwenye masoko, hazikuleta nafuu yoyote katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.

Hatua nyingine ambazo alisema hazikusaidia ni pamoja na kupunguza kodi na tozo kwenye mafuta ya dizeli na petroli, kuanza kutekeleza mpango wa dharura wa umeme na kutoa fedha za kununua chakula kwa Wakala wa Chakula.

“Licha ya hatua hizo kuchukuliwa, mfumuko wa bei uliongezeka maradufu kutoka wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2010/11 mpaka wastani wa asilimia 17.8 mwaka 2011/12. Serikali imefeli katika lengo lake la kupunguza makali ya maisha kwa wananchi,” alisema Zitto na kuongeza:

“Sio tu kwamba Serikali imeshindwa kudhibiti upandaji holela wa gharama za maisha bali pia hatua za Serikali zimeongeza kasi ya kupanda kwa makali ya maisha”.
Mkanganyiko wa maelezo

Kwa upande wake Christina Mughwai alibainisha kuwapo kwa mkanganyiko katika hotuba ya Serikali ya hali ya uchumi na mipango ya maendeleo, jambo ambalo alisema ni aibu kwa Serikali.

Alisema wakati Serikali inasema kwamba ukuaji usioridhisha wa Pato la Taifa unatokana na ukame ulioathiri Sekta ya Kilimo, kwa upande mwingine katika kitabu hicho hicho inasema kwamba uzalishaji wa mazao ya chakula hususani ngano, mihogo, maharage, ndizi na viazi uliongezeka ikilinganishwa na mwaka 2010 kutokana na hali nzuri ya hewa na mtawanyiko mzuri wa mvua kwa ustawi wa mazao.

“Mkanganyiko huu ni dalili ya ukosefu wa umakini katika kuandaa taarifa muhimu za Serikali na unaitia Serikali hii aibu,” alisema mbunge huyo wa Viti Maalum (Chadema).

Alisema kuongezeka kwa mfumuko wa bei hadi kufikia asilimia 19.2 Novemba mwaka jana kulipunguza uwezo wa Serikali kununua bidhaa na huduma kwa takribani asilimia 6.

“Hii ni sawa na Sh780 bilioni kuyeyuka katika Bajeti katika kipindi cha miezi minne tu ya utekelezaji wa wake,” alisema.

Alisema kasi ya ukuaji wa mfumuko wa bei ni dhahiri kwamba, sehemu kubwa ya bajeti hasa ya maendeleo ilishindwa kutekelezeka.

Msemaji huyo alibainisha kuwa hali ni mbaya zaidi kwa wananchi kutokana na mfumuko wa bei za vyakula ambao kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ulifikia asilimia 24.7 Novemba mwaka jana.

“Ukilinganisha na bei za vyakula mwaka 2010, mwananchi amepoteza uwezo wa kununua chakula kwa zaidi ya robo kati ya Novemba 2010 na Novemba 2011. Jumla ya vyakula ambavyo mwananchi alinunua kwa Sh10,000 mwaka 2010, sasa atanunua kiwango kile kile kwa Sh12,500,” alisema.

Kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania, alisema imeendelea kushuka ukilinganisha na fedha za kigeni kutokana na kutokuwapo kwa mikakati thabiti ya kuihimarisha.

“Kushuka kwa thamani ya shilingi licha ya kupanda kwa mauzo yetu nje kwa sekta zote mbili tunazotegemea sana (madini na utalii) kunaacha maswali mengi kuhusiana na chaguo letu kuhusu Hifadhi ya Fedha za kigeni,” alisema Mughwai.



Wachumi nao waiponda
Katika hatua nyingine, wachumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wameichambua bajeti ya Serikali wakisema imelenga kuwanufaisha viongozi wa Serikali, huku ikiwaacha njia panda wananchi.
Licha ya kuichambua bajeti hiyo, wasomi hao pia wameitaka Serikali kuweka tofauti za kisiasa pembeni unapofikia wakati wa kuandaa bajeti, huku wakipendekeza kuwe na mchakato maalum ambao utawashirikisha wataalam wa masuala ya uchumi na maendeleo.
Wametolea mfano wa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu waChadema, Zitto Kabwe.

Pia, wamesema kitendo cha Serikali kutegemea mapato kwa kuongeza kodi katika vinywaji na sigara ni aibu kwa taifa, huku wakitaka kodi zaidi zitozwe katika sekta za nishati na madini.

Wakizungumza jijini Dar es Salaam jana katika mdahalo ulioandaliwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Maendeleo kwa Kushirikiana na Kitengo cha Uchumi (UDSM), wachumi hao walisema bajeti ya mwaka huu ni mbaya, haina dira ya kumkomboa mwananchi hasa kwa kuwa ni tegemezi kwa wahisani.

Prosesa Humphrey Moshi alisema ili bajeti iweze kuwa na mwelekeo inatakiwa kuandaliwa kutoka chini kwa kuangalia makadirio ya kila wilaya na mikoa.

Profesa Moshi alisema licha ya kuwepo kwa wataalam wa uchumi nchini Serikali haiwatumii kwa kuwa tu wao ni wapinzani, hata kama wanao uwezo wa kusaidia mambo mbalimbali kwa ajili ya taifa.
 “Tuondoe tofauti za u-Chadema na u-CUF pale taifa linapokumbwa na masuala ya kijamii, kwani kama tutamtumia Profesa Lipumba au hata Zitto, wanaweza kuishauri Serikali na kuandaa bajeti nzuri,” alisema.

Kwa upande wake Dk Rose Shayo wa Taasisi ya Maendeleo ya chuo hicho, alisema ni aibu kwa nchi kama Tanzania yenye kila aina ya utajiri kutegemea fedha kutoka nje ili iweze kuwa na bajeti iliyoshiba.
Alisema kuwa ni miaka 50 imepita tangu Tanzania ipate uhuru, lakini bado Serikali inaendelea kuwa na bajeti ambayo haiwasaidii watu wa hali ya chini, licha ya kuwa nchi ina vyanzo vingi vya mapato.


Naye Mhadhiri Mwandamizi, Dk Jehovaness Aikaeli wa kitengo cha uchumi alisema bajeti hiyo haina dira na haitaweza kutatua matatizo katika sekta ya maendeleo kwa kuwa fedha zilizotengwa ni kiduchu.

Naye Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya alisema kuwa Serikali imeshindwa kutoa uchambuzi yakinifu katika suala zima la uchumi wanchi kwakutoweka halihalisi ya uchumi wa watu wake.



Mjadala wapamba moto

Wakati wa mjadala wa bajeti hiyo, Mbunge wa Singida Masahari, Tundu Lissu (Chadema) na Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi- CCM), jana walichafua hali ya hewa bungeni kutokana na maneno makali waliyotoa huku wakionyesha wazi kila mmoja anatetea maslahi ya chama chake.

Wakati Lissu alisema wabunge, Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanapaswa kuona aibu kutokana na udanganyifu wanaowafanyia Watanzania kwa kupanga mambo wanayojua hawatayatekeleza kupitia bajeti, akisema ni upuuzi, Mwigulu alisema wapinzani ni wanafiki, waongo, wana mapepo na wanapaswa kuombewa.

Wakati Lissu alielezwa kuwa ametumia maneno ya kuudhi, Nchemba alitakiwa kufuta maneno yake.

Wakati hao wakitoa lawama hizo, Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John  Komba aliwaita wapinzani vichaa ambao hawafai kuwepo bungeni bali hospitali ya vichaa ya Mirembe, iliyopo Dodoma.

"Ni vizuri mheshimiwa Mwenyekiti tukapimwa akili kabla ya kuingia humu (bungeni) ili wa kwenda Mirembe waende na wakubaki humu wabaki," alidai Kapteni Komba wakati akibeza hoja za wapinzani za kuikataa bajeti.

Komba alisema bajeti ya mwaka huu ambayo inapingwa, wabunge wa Kenya na Uganda wamekuwa wakiipongeza.

Akitumia ripoti iliyotolewa na viongozi wa dini hivi karibuni, Lisu alielezea jinsi serikali inavyoacha mianya ya ulipaji kodi, kusamehe kodi kwa wachimba madini wakubwa wa nje, na gesi asilia kutotumiwa kwa manufaa ya Watanzania.

Alisema hiyo ni aibu na upuuzi na kumfanya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu, Bunge), William Lukuvi kuja juu na kusema ametoa lugha ya maudhi kinyume na taratibu za Bunge.

Lissu alifuatiwa na Nchemba ambaye alisema wapinzani ni waongo, wana mapepo na anashangaa kwamba Tanzania kuna watu wanawaunga mkono wakati wanapaswa wawe wanatibiwa katika hospitali ya Mirembe.

Neno pepo liliifanya Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mabumba kumtaka alifute na yeye akasema: "Nalifuta kwa humu ndani lakini naomba wakaombewe."

No comments: