Na Kenny Ngomuo
Kikundi cha waraghbishi kutoka Mtandao
wa Jinsia Tanzania (TGNP), walifanya mchakato shirikishi wa uraghbishi kuanzia
tarehe 21 hadi 31 Mei 2012, katika vijiji vya Nsongwi Juu, Ifiga, Iwalanje,
Nsongwi Mantanji na Ntangano Ijombe, Kata ya Ijombe, Wilaya ya Mbeya Vijijini
mkoani Mbeya. Wakazi wa Kata ya Ijombe wameelezea kero mbalimbali ikiwemo
tatizo la mimba za utotoni kutokana na ukosefu wa mabweni kwa wasichana
wanaosoma katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Iwalanje. Shule ya Iwalanje
imekuwa mbali sana na makazi ya wanafunzi walio wengi. Wanafunzi wanatembea
umbali wa kati ya kilometa 4 hadi 8 kutoka vijiji vinavyotumia shule hiyo.
Waraghbishi
toka TGNP wakiwa katika mazungumzo ya pamoja na Wasichana
wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Iwalanje, Mei
2012
Katika kuchambua na kufuatilia kero
ya
kuongezeka kwa wasichana wanaobakwa na mimba mashuleni wanawake na wanaume wa Kata ya Ijombe wilaya
ya Mbeya vijijini walitoa kilio chao katika warsha iliyoendeshwa na Mtandao wa
Jinsia Tanzania (TGNP) . Akizungumza kwa uchungu, Bi Siza Mistoni anasema shule
ya Kata ya Iwalanje imekuwa mbali sana na makazi ( kilimeta zaidi sita toka
kijiji cha Matanji) tatizo lililopelekea
baadhi ya wanafunzi kutafuta vyumba vya kukodisha kwa jina maalum ‘GHETO’. …
‘Wanafunzi wamekuwa wakiishi kwenye magheto kwa muda mrefu na kupelekea
wasichana wengi kutokufanya vizuri katika
masomo yao kwani wao, wamegeuka kuwa wapishi , wanasaka maji, kuni kwa ajili ya kujipikia chakula.
Baadhi ya wanafunzi , kata ya Ijombe
Mbeya vijijini, wakitoka kusaka maji hali inayowapelekea kukosa vipindi vya masomo yao.
Kwa maana hiyo wasichana wamekuwa
wakitumia muda wao mwingi zaidi kufanya kazi
zilizo nje ya masomo tofauti wa watoto wa kiume ambao muda mwingi
wamekuwa wakijisomea. Wasichana wengi
wamepata mimba za utotoni na kuwapotezea
ndoto zao za baadae. Wakazi hawa wamedai kuwa baadhi ya magheto wanayoishi wapo
watoto wa kike na wakiume’, sambamba na
hilo kuna uwezekano mkubwa na hatari ya kuongezeka kwa maambukiza ya magonjwa hatarishi kama vile Ukimwi.
Baadhi ya wanawake walioshiriki
katika warsha ya uraghbishi wamewaasa wanawake na wanaume kuvuta nguvu za
pamoja na kuwa mabalozi wa kuwafundisha watoto wao popote pale walipo kujua
madhara ya mimba za utotoni. Wanafunzi waepuke tabia ya kubweteka kwa
utandawazi ulioingia hapa nchini kwa kasi kubwa. Wanakijiji waliweza kuchambua
mazuri ya utandawazi kama ukitumika vizuri ni njia mojawapo ya kujielimisha. Mfano wanafunzi wanaweza kupata
taarifa sahihi kuhusiana na masomo yao, kuangalia taarifa za habari na kujua
masuala mbalimbali yanayoendelea Tanzania, Afrika na Duniani kwa ujumla. Lakini
wanafunzi hao hao wanatumia television kinyume na maadili kwa kuangalia picha za ngono .
Wanakijiji hawa wamebainisha pia kuwa kumekuwepo na ulevi wa kupindukia katika Kata
ya Ijombe ambao unaathiri si tu maadili ya watoto bali hata wanaume ambao mara
nyingi hupelekea kufanya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa kike. ‘ Mwanaume anakuja saa tano usiku anaaza
kupiga kelele kudai chakula na anapokikosa kwa sababu hakuacha pesa matokeo yake ni kipigo kwa mwanamke’ alisema
Bi Mage John wa kijiji cha Iwalanje.
Vile vile ilibainika kuwa wasichana
wengi wanajiingiza katika vitendo viovu kwa kukosa msaada wa pesa kutoka kwa
wazazi wao kwa ajili ya mahitaji yao shuleni kama chakula na vitabu.
Wanakijiji hao wameongeza kuwa shule za Kata zilizoanzishwa hazina
walimu wa sayansi na vifaa vya
maabara, kitendo kinachozima ndoto zao za baadae. Wakazi wa Kata ya Ijombe wamedai
pia kuwa shule hizi zinachangisha pesa
kila mwaka wanatoa elfu kumi ( 10,000/-) mbali na ada ya shilingi elfu
ishirikini (20,000/=) kwa mwaka hawa ni wale wanaoishi nyumbani na kwenye magheto.
Kwa wanafunzi wanaoishi mashuleni wanalipa laki nne na nusu (450,000/-kwa
mwaka).
Hata hivyo, wazazi hawa wamedai
kuwa kuna michango mingine kama fedha za madawati, vitambulisho, bima za afya,
tahadhari na rimu. Michango hii inakuwa
ni kikwazo kwa wazazi ambao kipato chao ni kidogo. Wanawake pia wamedai kuwa
mara nyingi mzigo wa kulipa ada unawaangukia wao kutokana na wanaume wengi kuwa
walevi na kusahau familia zao.
Kwa upande wake mwanafunzi wa
kidato cha nne Annety Bora anasema changamoto kubwa iliyopo katika shule ya
Iwalanje ni ukosefu wa mabweni ya wasichana ambapo inapelekea baadhi ya
wasichana kuishi kwenye madarasa kutokana na mabweni ya wasichana kutokuwepo
shuleni hapo. Pia ameuomba uongozi wa shule uweze kufuatilia na kusimamia vyema uwepo wa walimu wa sayansi pamoja na vifaa vya kufundishia kwa ajili masomo ya
sayansi kwani vilivyopo havikidhi mahitaji ya wanafunzi hao
Hata hivyo wananchi wanaolizunguka
eneo la shule hiyo, wameuomba uongozi wa serikali katika ngazi ya Kata kuchukua
hatua za haraka hasa kuhakikisha
michango isiyokuwa ya lazima inaondolewa, kupata waalimu wenye sifa za
kufundisha na siyo ‘yebo yebo’ na pia kulinda
maadili na usalama wa watoto wetu.
No comments:
Post a Comment