Thursday, June 21, 2012

Pinda aunda Kamati kuokoa Bajeti Kuu

KAZI YAKE KUTAFUTA VYANZO VIPYA VYA MAPATO, KUONGEZA BAJETI YA MAENDELEO
 
 Neville Meena na Mussa Juma, Dodoma
 WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameunda Kamati Maalum ya mawaziri sita kusaidia mchakato wa marekebisho ya Bajeti ya Serikali ambayo mjadala wake utahitimishwa kesho.Kuundwa kwa kamati hiyo kunazifanya kamati zinazoifanyia kazi Bajeti ya 2012/2013 kufikia tatu.

Ijumaa iliyopita wabunge wa CCM waliunda kamati ndogo kwa ajili ya kusaidi pamoja na mambo mengine kuangalia vyanzo vingine vya mapato na kuona iwapo bajeti ya maendeleo inaweza kuongezwa, kukidhi kiu ya wabunge.

Kamati nyingine ni ile ya Fedha na Uchumi ya Bunge ambayo tayari imetoa maoni yake bungeni kuhusu Bajeti, lakini ikabainisha kuwapo kwa kasoro kadhaa ambazo zinapaswa kurekebishwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alikiri kuundwa kwa kamati hiyo, lakini akakataa kutoa taarifa za kina kuhusu suala hilo kwa maelezo kwamba huo ni utendaji wa kawaida wa shughuli za Serikali.

“Sidhani kama hiyo ni habari kubwa ya kwenda kwenye public (kwa umma). Kwanza siyo kamati ya mawaziri, haiwezi kuwa hivyo, na huo ni utendaji wa kawaida wa ndani ya Serikali maana sisi tuna mambo mengi tunafanya,”alisema Lukuvi na kuongeza:

“Kamati za utekelezaji wa shughuli za Serikali ziko nyingi sana na siyo tu za Bajeti. Kwa hiyo ndio maana nakwambia hilo ni jambo dogo sana ambalo mimi sidhani kama linahitaji kutangazwa, kama lingekuwa hivyo mimi ningekuwa wa kwanza kutaka kulizungumzia,” alisema.

Kazi ya Kamati

Habari ambazo Mwananchi limezipata zinasema kwamba kamati ya mawaziri nayo inafanya kazi ya kubuni vyanzo vingine vya mapato ya Serikali, ili kufidia pengo la baadhi ya kodi ambazo zinatarajiwa kufutwa kutokana na shinikizo la wabunge.

Miongoni wa kodi hizo ambazo huenda zikafutwa wakati Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa atakapohitimisha Bajeti yake kesho, ni ile inayopendekezwa kuongezwa kwenye muda wa maongezi ya simu na ile ya inayopendekezwa kutozwa kwa waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda.

Kadhalika, kamati hiyo ya mawaziri imepewa jukumu la kuona iwapo itaweza kushauri uwezekano wa kuongezwa Bajeti ya sasa ya maendeleo kutoka asilimia 30 inayopendekezwa na Serikali, jambo ambalo pia limekuwa likipigiwa kelele na wabunge wengi.

“Hatuwezi kufumua Bajeti nzima ila kusema kweli ni kwamba lazima kutakuwa na mabadiliko mengi, tatizo kubwa ambalo linatuumiza vichwa, tunajiuliza kama tunaweza kupata hiyo nyongeza ya hizo fedha za maendeleo walau Sh500 bilioni,”alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.

Taarifa zaidi zimewataja wajumbe wanaounda kamati hiyo ambayo ilifanya kikao chake cha kwanza juzi kuwa ni Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Mgimwa, Lukuvi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.

Wengine katika kamati hiyo iliyoundwa kwenye kikao cha kazi cha Baraza la Mawaziri, Jumamosi iliyopita chini ya Pinda, ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Adam Malima na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima.

Habari zaidi zilidai kuwa mawaziri hao watafanya kazi hiyo sasa na hata baada ya Bunge la Bajeti ili ushauri wao uweze kuzingatiwa katika maandalizi ya bajeti ijayo ya 2013/2014.

“Tunawatarajia kwamba watatusaidia hata katika bajeti za kisekta zinazokuja,” alisema mjumbe mwingine wa kikao hicho.

Wasiwasi ulikuwa ni iwapo ushauri wa kamati hiyo utaweza kuzingatiwa katika majumuisho ya Waziri wa Fedha na Uchumi wakati atakapohitimisha Bajeti yake, lakini jana Spika wa Bunge, Anne Makinda alifungua milango inayowezesha Serikali kuongeza vyanzo vipya vya mapato hata baada ya Bajeti Kuu kupitishwa.

Uamuzi wa Bunge

Jana Spika Makinda alisema Bunge limeahirisha kujadili na kupitisha Muswada wa Sheria za Fedha wa mwaka huu, na sasa muswada huo utapitishwa mwishoni kabisa mwa Mkutano wa nane Bunge.

Hatua hiyo ni dalili kwamba Serikali sasa iko tayari kufanya marekebisho makubwa ya Bajeti yake na hata zile za kisekta, hasa katika maeneo ya kuongeza vyanzo vipya vya mapato kadri Kamati za Bunge, wabunge na Kambi ya Upinzani watakavyopendekeza.

Kusogezwa huko pia kumewezesha kuongezwa siku moja ya majadiliano ya hotuba ya Bajeti kutoka siku nne hadi tano, pia unatoa fursa ya Serikali kuongeza vyanzo vyake vya mapato kwa kuzingatia maoni, mawazo na ushauri wa wabunge.

Muswada wa Sheria ya Fedha ulikuwa umepangwa kuwasilishwa kesho kama hitimisho la mjadala wa Bajeti ya Serikali, lakini sasa umepelekwa mbele kutokana na kile Makinda alichosema kuwa ni kutoa fursa kwa wabunge kuishauri Serikali kuhusu vyanzo vipya vya mapato.

Makinda alisema uamuzi huo ulifanywa katika kikao cha Kamati ya Uongozi cha Juni 18, mwaka huu baada ya kuzingatia maoni ya wabunge, Serikali na Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi ambao walitaka kuahirishwa kwake, ili kuruhusu Serikali kuongeza vyanzo vya mapato kadri itakavyoshauriwa na wabunge.

Aliongeza kuwa Bunge limeridhika kwamba licha ya kutopitishwa kwa muswada huo mapema kama inavyotakiwa, bado Serikali itaweza kukusanya kodi kwa kutumia sheria nyingine za nchi zilizopo.

Mabadiliko hayo ni mwanzo wa mchakato wa mabadiliko ya Kanuni za Bunge ili kuwezesha vikao vya Bunge la Bajeti kufanyika mapema na kuhitimishwa Juni 30, ili kuruhusu Serikali kuanza mwaka wa fedha baada ya Bajeti nzima na Sheria ya Fedha kuwa vimepitishwa.

“Mabunge mengi ya Jumuiya ya Madola yana utaratibu wa kupitisha Muswada wa Sheria ya Fedha na Muswada wa Mutumizi mwishoni kabisa mwa mjadala wa Bajeti. Lakini tumefuatilia na kubaini kuwa mchakato wa kupitia Bajeti ya Serikali huanza mapema na kumalizika kabla ya mwaka mpya wa fedha kuanza,”alisema Makinda na kuongeza:

“Bunge letu lingepaswa liwe linakutana na kuanza mchakato wa kupitia Bajeti ya Serikali mapema, ili inapofika Juni 30, mkutano wa Bajeti uwe umemalizika na Muswada wa Sheria ya Fedha kuanza kutumika ifikapo Julai Mosi ambapo mwaka mpya wa fedha unaanza”.

Alisema kutokana na hali hiyo Kanuni za Bunge zitaendelea kufanyiwa marekebisho ili mikutano ya Bunge la Bajeti iweze kuanza mapema kama ilivyo katika nchi nyingine za Jumuiya ya Madola.

Kwa upande Lukuvi, alisema uamuzi wa Serikali kukubali hoja ya kusogezwa mbele muswada huo, ni kutoa fursa ya kuzingatiwa kwa maoni ya wabunge na kuendelea kuibuliwa kwa vyanzo vipya vya mapato.

“Kama Serikali isingekubali, basi ujue hilo la kuahirisha muswada lisingewezekana kabisa, maana ukishapitisha Muswada wa Sheria ya Fedha hata maoni yatakayoendelea kutolewa kwenye bajeti nyingine yangekuwa hayana maana,” alisema Lukuvi.

Mbunge alipua mawaziri

MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), amewataka wabunge kumsaidia Rais Jakaya Kikwete kuikataa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/13, kwa kuwa mawaziri wake wameshindwa kumsaidia kuleta Bajeti ambayo inajibu matatizo ya Watanzania.

Alitoa kauli hiyo wakati akichangia kwenye mjadala wa Bajeti na baadaye kutoa ufafanuzi wa kauli yake nje ya Bunge, kuwa mawaziri wa Kikwete wameshindwa kumsaidia, kwani wametenga fedha nyingi katika matumizi mengineyo na kutelekeza mpango wa Serikali wa Miaka Mitano.
 

No comments: