BAJETI ya Serikali ya mwaka 2012/2013 inatarajiwa kutumia Sh15
trilioni katika vipaumbele saba ikilinganishwa na Sh13.5 trilioni
zilizotengwa mwaka 2011/12.Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa
aliileza Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi kuwa matumizi ya kawaida ya
Serikali yanatarajiwa kuwa Sh10 trilioni na fedha za maendeleo ni Sh5
trilioni.
Dk Mgimwa alimweleza mwandishi wetu kuwa kipaumbele cha kwanza katika Bajeti yake ya kwanza tangu kuteuliwa hiyo ni miundombinu.
Kwa
mujibu wa waziri huyo, miundombinu imegawanyika katika makundi manne ya
reli, umeme, maji salama, usafirishaji na uchukuzi ambavyo vimetengewa
jumla ya Sh4.5 trilioni.
Vipaumbele vingine vya Serikali ni kilimo,
viwanda, rasilimali watu, huduma za jamii, utalii, biashara ya ndani na
nje na huduma za fedha.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho
zilisema kuwa katika bajeti hiyo, fedha zilizopelekwa Wizara ya Uchukuzi
kwa ajili miradi ya maendeleo ni Sh252 bilioni huku sekta ya usafiri wa
reli ikitarajiwa kutumia Sh130 bilioni.
Katika Bajeti hiyo ya
maendeleo, Wizara ya Ujenzi imetengewa Sh693 bilioni, wakati sekta ya
nishati ikiwa nayo imepewa umuhimu na mradi wa ujenzi wa bomba la gesi
kutoka mikoa ya kusini umetengewa Sh325 bilioni.
Mwelekeo huo wa bajeti unaonyesha pia kwamba, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetengewa jumla ya Sh364 bilioni.
Kuuza mashangingi
Taarifa
kutoka ndani ya kikao hicho, zilisema katika mkakati wa kubana
matumizi, Serikali itapunguza matumizi ya magari ya kifahari kwa kiwango
kikubwa.
Katika hatua hiyo, inatarajiwa pia kupiga mnada baadhi
ya magari hayo yanayotumiwa na mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu
na wakurugenzi na kununua magari madogo yenye gharama nafuu.
Hata
hivyo, chanzo chetu kilisema waziri huyo hakufafanua suala hilo akisema
atalizungumza zaidi wakati wa kuwasilisha Bajeti hiyo Mjini Dodoma.
Takwimu
za Serikali za mwaka juzi, zilionyesha kuwa Serikali Kuu hadi na Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ilikuwa ikimiliki magari
40,000, kati yake 11,000 yakiwa ya kifahari.Tayari Wizara ya Ujenzi
kupitia timu ya wataalamu mwaka Aprili, 2007 ilitoa ripoti ya namna bora
ya kupanga matumizi ya magari ya Serikali kwa kuangalia kila daraja la
kiongozi, lakini ripoti hiyo iliishia mezani kwa aliyekuwa Katibu Mkuu
Kiongozi, Philemon Luhanjo.
Zitto aomba ushauri
Waziri Kivuli
wa Fedha, Zitto Kabwe amesema Bajeti yake mbadala kwa mwaka fedha
2012/13 itajikita katika kuongeza mapato ya ndani, kupunguza misamaha ya
kodi na matumizi ya Serikali yasiyokuwa ya lazima.
Katika kuboresha
bajeti hiyo, Zitto kupitia vyombo vya habari na mitandao mbalimbali
amewaomba wadau wamshauri jinsi ya kuiboresha ili ikidhi mahitaji ya
Watanzania.
“Naomba kila mtu atakayeweza, atoe mchango wake wa
juu ya nini kinatakiwa kipewe kipaumbele zaidi katika bajeti ya mwaka
huu wa fedha, maoni yenu yatajumuishwa katika kuboresha bajeti ya
upinzani ili kuishawishi Serikali kuifuata,” alisema Zitto.
Alisema
baadhi ya maeneo yatakayotazamwa kwa umakini katika bajeti hiyo ni
pamoja na pamoja na mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira.
Eneo
jingine ambalo Zitto atalipa kipaumbele ni jinsi ya kupunguza uagizaji
wa bidhaa kutoka nje na kuangalia namna ya kuongeza mauzo ya bidhaa ya
nchi.
Akitolea mfano wa takwimu zinazoishia Machi mwaka huu,
alisema Tanzania iliagiza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani 12
bilioni na kuuza nje zenye thamani ya dola 6.9 bilioni.Zitto atalenga
katika kupunguza deni la taifa ambalo kwa sasa limefikia Sh22 trilioni
kutoka Sh7 trilioni mwaka 2009 na Sh11 trilioni mwaka 2010.
Wabunge kuwabana mawaziri
Baadhi
ya wabunge wa CCM wanatarajia kuibana Serikali katika Bunge lijalo
wakidai kuwa imeshindwa kutekeleza kwa ukamilifu Bajeti ya mwaka jana
pamoja na kuwawajibisha baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi.
Katika
mkutano uliopita, wabunge waliibana Serikali wakitaka mawaziri wanane,
manaibu waziri wawili na watumishi wengine wa umma waliotajwa katika
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), wawajibishwe.
Lakini wabunge hao wamesema Rais Jakaya Kikwete aliwafuta kazi mawaziri
sita na kuwahamisha wizara wawili na kuwang’oa manaibu waziri wawili
miongoni mwa waliotajwa na hawajaona juhudi za kuwawajibisha watuhumiwa
wengine.
Mawaziri waliofutwa kazi ni William Ngeleja (Nishati na
Madini), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omari Nundu (Uchukuzi), Dk
Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Cyril Chami (Viwanda na
Biashara) na Mustafa Mkulo (Fedha).
Waliohamishwa wizara ni
Profesa Jumanne Maghembe (Kilimo) kwenda Maji na George Mkuchika
(Tamisemi) kwenda Ofisi ya Rais, Utawala Bora. Manaibu Waziri waliotemwa
ni Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Athumani Mfutakamba
(Miundombinu).
Tayari Maige amekaririwa wiki hii akiwa katika
ziara ya kutembelea jimbo la Msalala, mkoani Shinyanga, akiweka wazi
kuwa atawasha moto atakapoingia bungeni akiwa mbunge wa kawaida wiki
ijayo, kwani uwaziri wake ulikuwa unamzuia kuibana Serikali.
Filikunjombe anena
Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Deo
Filikunjombe, alisema juzi kuwa tatizo kubwa la Serikali ni kuchelewa
kuchukua hatua hata inapoonekana dhahiri kuwa kuna tatizo.
Kuhusu
Bajeti alisema kitendo cha Serikali kuahidi kutoa fedha kwa wizara
fulani na kutofanya hivyo ni moja ya matatizo makubwa yanayosumbua kwa
sasa na atalikemea kwa nguvu zote. “Hatuwatendei haki wananchi kwa kukaa
bungeni miezi mitatu na matunda yasionekane. Ukisema sehemu fulani
fedha zinahitajika, Serikali inasema itazitoa, lakini mwisho wa siku
hazionekani, hii siyo haki,” alisema Filikunjombe.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Augustine Mrema,
alisema licha ya Rais Jakaya Kikwete kujitahidi kusafisha wizara, bado
kuna watendaji wabovu katika halmashauri ambao wanazidi kumwangusha.
“Baada
ya kelele za wabunge katika kikao kilichopita na Rais kuwawajibisha
mawaziri, isingetarajiwa halmashauri kama za Mafia na Rufiji kutuletea
uchafu na hesabu ambazo hazijahakikiwa na hazieleweki,” alisema Mrema na
kuongeza:
“Sisi tunazidi kumwambia Rais na Waziri Mkuu kwamba,
bado kuna halmashauri sugu, hazitaki kabisa kujirekebisha, kuna wakuu wa
wilaya na wakurugenzi ambao bado wanawaangusha, wanafanya madudu huko.”
Kwa
upande wake, Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Lugola alisema atakufa na
Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii akidai kuwa waziri
aliyetangulia amewafanyia madudu Watanzania. Mbunge huyo alieleza sababu
za kutounga mkono bajeti hiyo.
“Pale bungeni walionyesha Bajaji
nzuri ambazo tulizikubali, lakini walinunua Bodaboda ambazo kipindi cha
mvua mgonjwa haendi…” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti
Maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema hakuna mtu wa kumfunga mdomo kwa
kuwa anatetea maslahi ya Watanzania: “Siku zote mimi nasema asiyefanya
kazi asile… kwa mazuri, lazima tuiunge mkono serikali, lakini kwa uzembe
hakuna kulala mpaka kieleweke,’’ alisema Bulaya.
Mbunge wa Kahama
(CCM), James Lembeli alisema: “Nataka uwajibikaji siyo mambo ya
propaganda. Huu ni wakati wa kuwajibika na atakayefanya hivyo ni rafiki
yangu, lakini wazembe tutabanana nao ukumbini kuanzia wiki ijayo.’’
Imeandikwa na Edwin Mjwahuzi, Fidelis Butahe na Fredy Azzah, Dar na Habiel Chidawali, Dodoma
No comments:
Post a Comment