MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amesema moto uliowashwa na chama
hicho katika Operesheni Sangara utaendelea nchi nzima, lengo likiwa ni
kuiondoa CCM madarakani na iwapo itasalimika mwaka 2015, atajiuzulu
siasa.
Mbowe alitoa kauli hiyo juzi alipohutubia mamia ya wakazi
wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wakati chama hicho kilipofanya mkutano
mkubwa kwenye uwanja wa mpira wilayani humo.
Alisema CCM kimepoteza
mwelekeo wa kuongoza taifa na ndiyo sababu maisha ya Watanzania yamezidi
kuwa mgumu kadri miaka inavyozidi kusonga mbele.
“Wajibu wa
Serikali kokote duniani ni moja tu, kuwezesha watu wake kutoka katika
hali ngumu za maisha na kuwapeleka kwenye heri, leo CCM wameligawa Taifa
katika vipande, wanauza rasilimali za nchi na kuwadidimiza watu wa
kipato cha chini wengi wao wakiwa ni wakulima,” alisema Mbowe na
kuongeza:
“Ndugu zangu ngojeni niwaulize swali, wakati wa utawala
wa Mwinyi na Mkapa (marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin
Mkapa), ni kipindi gani maisha yalikuwa mazuri?” Wananchi wakajibu
(kipindi cha Mwinyi). Miaka 10 ya uongozi wa Mkapa na miaka saba ya
Kikwete, ni kipindi gani maisha yamekuwa magumu zaidi?" Wakajibu
(Kikwete); Je, 2015 wanakuja tena kutuomba kura huyo atakayekuja si
ndiyo itakuwa mbaya zaidi, Chadema hatuwezi kukubali na moto huu
tuliowasha utaendelea nchi nzima hadi Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kama CCM
itasalimika nitajiuzulu siasa.”
Mbowe alikishambulia CCM akidai
kimepoteza mwelekeo uliowekwa na waasisi wake, chini ya uongozi wa
Mwalimu Julius Nyerere wa kuzingatia usawa, udugu huku kikijikita katika
msingi wa kutetea wakulima wanyonge na wafanyakazi lakini sasa
kimewagawa wananchi katika matabaka ya walio nacho na wasio nacho.
“CCM
ya Mwalimu Nyerere ilijali wakulima na wafanyakazi wa kipato cha chini,
ilijenga mshikamano baina ya Watanzania wote bila kujali ukabila.
Tanzania ina makabila zaidi ya 120, lakini tunaishi kama mtu na ndugu
yake, leo taifa limegawanyika vipande huku maadili ya uongozi
yakiporomoka,” alisema Mbowe.
Katika mkutano huo uliokutanisha
viongozi wote wa kitaifa wa chama hicho, Mbowe alisema kwa sasa CCM
kimevuruga hata mitalaa ya elimu huku akituhumu watunga sera kuwa
wanafanya hivyo makusudi kwa kuwa watoto wao hawasomi katika shule hizo.
“Mwalimu
alijenga CCM iliyozingatia usawa, watoto wote walisoma shule moja, mimi
nilisoma na watoto wa Mwalimu Nyerere, mawaziri na wakulima katika
shule hiyo, leo watoto wa mkulima wanasoma shule za kata ambazo hazina
walimu, vitabu, maabara wala library (maktaba), wakati watoto wa vigogo
wakisoma nchi nje na wale wa wakuu wa wilaya wakisoma shule za
(academy),” alisema Mbowe.
Aliwataka wakazi wa mikoa ya kusini, Lindi
na Mtwara kuunganisha nguvu kwa lengo la kukiondoa CCM madarakani
katika chaguzi zote ukiwamo mkuu wa 2015.
“Ndugu zangu wa Masasi,
mimi Mbowe ninatimiza miaka 21 nikiongoza siasa za upinzani zenye lengo
la kuleta ukombozi wa kweli kwa Taifa hili, nimefunguliwa kesi za
uchochezi tisa hadi leo, lakini sitaacha harakati hata wakinifunga, bado
nitaendelea na harakati za ukombozi hadi Watanzania watakapofikia
kwenye uhuru wa kweli,” alisema Mbowe.
Kwa upande wake, Katibu
Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alieleza kusikitishwa kwake na
umaskini unaoukabili Mkoa wa Mtwara licha ya kuwapo rasilimali nyingi
zinazouzunguka ikiwamo gesi na korosho.
Alisema kumekuwa na
ufisadi mkubwa unaofanywa katika ununuzi wa korosho na licha ya wananchi
kukatwa Sh30 katika kila kilo wanayouza, bado mikoa hiyo ya kusini
inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji, huduma muhimu za kijamii
kama zahanati na shule.
“Taifa linaweza kuendelea ikiwa
rasilimali za nchi ambazo zinatoka kwa wananchi zitawarudia na kutumika
katika kuendeleza miradi ya maendeleo. Leo mnakatwa Sh30 katika kila
kilo moja ya korosho mnayouza, tumetafuta ni kiasi gani cha korosho
kimepatikana kwa mwaka hapa nchini lakini taarifa hizo hatuzipati.”
“Lakini
taarifa tulizopata Ulaya zinasema Tanzania imeuza tani 157,000 kwenye
soko la dunia, haya mabilioni ya fedha mnazokatwa kwa ajili ya miradi ya
maendeleo zinatumika wapi?” alihoji na kuongeza kuwa fedha hizo
zinastahili kudaiwa.
No comments:
Post a Comment