NI MAASKOFU, MASHEHE, WASEMA WIZI UPO KWENYE MISAMAHA YA KODI, MAGENDO
Fredy
Azzah na Raymond Kaminyoge KAMATI ya Viongozi wa Dini, imetoa ripoti
yake ya utafiti kuhusu uchumi wa nchi na kusema Serikali inapoteza
Sh1.7trilioni kutokana na ukwepaji kodi, misamaha ya kodi na utoroshwaji
wa mali na fedha nje ya nchi.
Matokeo ya utafiti wa kamati hiyo
yametolewa wakati kesho Serikali inatarajiwa kusoma Bajeti Kuu kwa
mwaka 2012/13, huku ikitegemea misaada kutoka nchi wahisani wanaochangia
katika Mfuko Mkuu wa Bajeti (GBS). Utafiti huo uliofanywa na Kamati ya
Masuala ya Uchumi na Haki za Binadamu (ISCJIC) na kupewa jina la ‘The
one billion dollar question: how can Tanzania Stop losing so much tax
revenue’ (Suala la dola bilioni moja: Tanzania inawezaje kuzuia upotevu
wa kiasi hicho cha kodi?) ilizinduliwa jana jijini Dar es Salaam.
Ripoti
hiyo ambayo imetokana na utafiti uliofanywa kwa kutumia nyaraka
mbalimbali za Serikali zikiwamo za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na
mashirika ya kimataifa; Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani
(IMF), imebainisha kuwa Serikali inapoteza Dola za Marekani bilioni moja
kila mwaka kutokana na misamaha ya kodi, ukwepaji wa kulipa kodi hiyo
na utoroshwaji wa mali na fedha nje ya nchi. ISCJIC inajumuisha viongozi
wa Baraza la Kuu Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Tanzania (Tec).
Mtafiti na
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper Ngowi akifafanua kuhusu
utafiti huo alisema walitumia vyanzo 167 kupata takwimu hizo na kuwa
upotevu uliotajwa kwenye taarifa hiyo wamechukulia ule wa kiwango cha
chini zaidi. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Askofu Paul Ruzoka alisema
endapo kiasi hicho cha fedha kingekusanywa, kingesaidia Bajeti Kuu ya
Serikali na kuondokana na utegemezi wa fedha za wahisani ambazo mara
nyingi huambatana na masharti.
Askofu huyo wa Jimbo Katoliki la
Tabora, alisema katika utafiti huo walibaini moja ya mambo yanayochangia
upotevu huo kuwa ni sera mbovu za Serikali na uzembe katika ukusanyaji
wa kodi. “Ipo haja ya kuwa na mipango mizuri ya kukusanya kodi,
kuyadhibiti makampuni yanayotosha fedha na pia kubana kama siyo kuondoa
kabisa misamaha ya kodi,” alisema Askofu Ruzoka.
Mwenyekiti huyo
wa kamati alisema ni vyema Serikali ikatazama njia nyingine ya kuvutia
wawekezaji badala ya kuweka misamaha ya kodi jambo ambalo linawaumiza
wananchi. Alisema wakati huu ambao utafiti juu ya upatikanaji wa mafuta
na gesi unaendelea, hawana imani kama wananchi watatendewa haki, huku
akitolea mfano wawekezaji walio kwenye sekta ya madini jinsi
walivyoshindwa kuwasaidia wananchi. Kutokana na hali hiyo, aliwataka
wabunge na Serikali kutumia Bunge la Bajeti linaloendelea kujadili jinsi
wanavyoweza kukabiliana na hali hiyo.
Ripoti Ripoti hiyo
inafafanua kuwa kwa makadirio ya chini, kila mwaka Serikali inapoteza
kati ya Dola za Marekani 847 milioni na 1.29 bilioni (Sh1.35 trilioni na
2.05 trilioni), huku akifafanua kuwa makadirio ya kati ni Dola za
Marekani 1.07 bilioni sawa na Sh1.7 trilioni.
Kuhusu utoroshaji
wa fedha nje ya nchi, alisema baadhi ya kampuni ambazo zina ofisi katika
nchi zaidi ya moja, zimekuwa zikitoa taarifa za uongo kuhusu ununuzi
wake kwa lengo la kukwepa kodi. Akitoa takwimu ambazo chanzo chake ni
Benki ya Dunia (WB) katika ukanda wa Afrika Mashariki, alisema kampuni
za Tanzania zinaongoza kwa kutoa taarifa za ukweli.
“Asilimia 69
ya kampuni zilizopo nchini hutoa taarifa sahihi, Uganda ni asilimia 77
na Kenya asilimia 86,” imesema sehemu ya ripoti hiyo... “Kwa maana hiyo,
Tanzania ndiyo tunaoongoza kwa udanganyifu lakini wenzetu Kenya angalau
wako juu katika kulipa kodi katika mauzo wanayofanya.”
Alisema
kampuni 400 ndizo zinazolipa kodi kwa asilimia 70 huku wafanyabiashara
ndogondogo wakilipa asilimia 30. “Kampuni kubwa ndizo zinazochangia kwa
kiasi kikubwa katika ulipaji wa kodi lakini, kampuni ndogo ni wakwepaji
wakubwa wa kodi,” alisema.
Alisema kampuni ndogondogo ndizo
zinazoongoza kwa kukwepa kodi kwani ni asilimia 17 pekee ya mauzo ndiyo
hutolewa taarifa kwa ajili ya kulipa kodi. Kwa upande wa kampuni ya
uchimbaji madini Dk Ngowi, alisema asilimia 65.4 ya kodi inayolipwa na
kampuni hizo, inatokana na makato ya kodi kwenye mishahara ya
wafanyakazi wake (PAYE).
“Ukiona kampuni za madini zinasema
zinalipa kodi ufahamu kwamba zaidi ya nusu ya fedha hizo ni kodi za
wafanyakazi, siyo kodi inayotokana na mapato ya madini hayo,” alisema Dk
Ngowi. Alisema kodi inayolipwa na kampuni za madini zinazomilikiwa na
wawekezaji wa kigeni, zinalipwa na wafanyakazi kupitia kodi ya mishahara
yao.
Alisema kampuni ndogondogo ndizo zinazoongoza kwa kukwepa
kodi kwani ni asilimia 17 pekee ya mapato ndiyo hutolewa taarifa ili
ziweze kulipa kodi. Mhadhiri huyo alipendekeza Serikali itumie utafiti
huo kuweka mikakati ya namna ya kupata fedha hizo zinazopotea.
“Fedha hizi zikipatikana tunaweza kuondokana na utegemezi wa misaada kutoka kwa wafadhili,” alisema Dk Ngowi.
No comments:
Post a Comment