Friday, June 8, 2012

Swali Na Jibu Kuhusu Katiba Mpya

Habari za kazi?

Nina maswali ambayo yananitatiza kidogo. Hivyo si vibaya nikashare na
wengine na kama ni wasiwasi wangu tu basi nifahamu hivyo. Najiuliza
maswali
kadhaa kuhusu mchakato mzima wa kuandika katiba mpya.

Swali la kwanza: Je kwa mwendo huu tutaweza kuwa na katiba mpya ifikapo
2015, kabla ya uchaguzi?
Hali inavyokwenda sasa inanipa tabu kuamini kuwa katiba mpya itakuwa
imepatikana by 2015. Kwa nini nina wasiwasi? Mpaka hivi sasa Tume
haijaanza
kazi! Ni lazima tukumbuke ukubwa wa nchi yetu na mambo mengine makubwa
yanayoendelea kama vile sensa n.k. Aidha kuna mvutano wa kisheria juu ya
Tume ya Katiba kuweza kufanya kazi Zanzibar kabla ya kuidhinishwa na
Baraza
la Wawakilishi. Pili baadhi ya Wazanzibari tayari wanaona tuwe na process
tofauti, yaani kwanza tuwe na kura ya maoni kuwauliza wananchi iwapo
wanautaka muungano ama hawautaki. Hii nayo ni changamoto nyingine
itakayoleta mjadala mrefu.


Bado haujapatikana muafaka wa namna Bunge maalum la kutunga katiba
litakavyoundwa. Suala hili linaweza kuleta malumbano ya muda mrefu. Na kwa
uzoefu wetu serikali yetu hukubali kupokea maoni pale inapokuwa
imeshinikizwa kila kona na kila upande. Mashinikizo haya yatachelewesha
process.

Bado haujapatikana muafaka juu ya namna ya kuendesha zoezi la kura
ya maoni. Aidha hakuna muafaka juu ya nani atasimamia zoezi hili la kura
ya
maoni.

Pia zipo tofauti nyingine ambazo bado hazijapatiwa muafaka kama vile
iwapo watanzania wengi wataikataa katiba mpya katika kura ya maoni, basi
katiba ya zamani itaendelea kutumika. Hili bado nalo lina utata na
linahitaji majadiliano ambayo yatachukua muda na kulifanya zaoei la katiba
mpya kuweza kuchelewa sana.
Hata suala la ni asilimia ngapi itakuwa considered kuwa imeshinda ni
utata mtupu. Wapo wanaona kuwa asilimia iliyowekwa ni ndogo sana. Hivyo
katiba inaweza kupita wakati imekatiliwa na nusu ya Watanzania. Iwapo hili
litatokea huwezi kuita hiyo ni katiba Watanzania. Hili nalo lina utata na
linaweza kuleta mjadala mrefu, kubadilisha sheria n.k. Natoa sababu hizi
kuonyesha ni namna gani tunaweza tukafika 2015 hatuna katiba mpya kama
ambavyo tunatarajia. Na iwapo itakuwa hivyo, maana yake nini? Hili
linanipeleka katika swali langu la pili.


Je tupo tayari kuingia katika uchaguzi wa 2015 na katiba hii iliyopo?
Nina hakika Chama tawala kitafurahi kweli na kinaweza kudelay process ili
tusipate katiba mpya by 2015 na tuingie katika uchaguzi tukiwa na katiba
hii
ya kisultani na watakwepa kuwajibika kwa hilo kwa kutoa visingizio
mbalimbali. Je tupo iwapo itakuwa hivyo, tutakuwa na uchaguzi huru na wa
haki? na jee haliwezi kutupeleka katika machafuko? Je tupo tayari kuingia
katika uchaguzi na Tume hii ya uchaguzi?

Katika siku za mwanzoni, wapo waliopendekeza kuwa ni vyema mchakato wa
kuandika katiba usiharakishwe, badala yake upewe muda wa kutosha, isiwe
lengo 2015 tuwe na katiba mpya. Ili tuwe na uchaguzi huru na na wa haki
2015, Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ipeleke mswada wa kuunda Tume
huru ya Uchaguzi, Ofisi huru ya msajili wa vyama vya siasa na ifanye
marekebisho yote ya kisheria ili tuwe na uwanja sawa wa ushindani 2015,
huku
tukijipa muda wa kutosha kuandika katiba mpya. Watu kama kina Jenerali
Uimwengu ndio walikuwa na mawazo haya. Nadhani kwa hali inavyokwenda
mawazo
yao tunaweza sasa kuanza kuwaelewa kwa nini walifikiria hivyo.

Swali langu la mwisho: iwapo 2015 hatuna katiba mpya ni nani atawajibika
kwa
hilo? Serikali? wanasiasa wote kwa ujumla? au nani? Tukumbuke kuwa
tumeingia
katika mchakato wa kuandika katiba mpya huku tukikabiliwa na mambo
yafuatayo: ombwe la uongozi, hatuna uongozi ambao unaaminika una ushawishi
na unakubalika; tuna tofautiana katika mambo mengi sana ambayo tulitakiwa
tuwe na muafaka wa kitaifa juu ya mambo hayo miaka mingi iliyopita, lakini
tulifanya ajizi na sasa mambo hayo yamekuwa ni magumu zaidi, yaani ni kama
kidonda ndugu. Mambo haya yanaleta changamoto nyingi sana katika mchakato
wa
kuandika katiba. Hii imetokana na tabia ya serikali kutokushughulikia
masuala kwa wakati na kuyaacha yakiota mizizi huku wakifikiria kuwa
yatajitatue yenyewe. Akili ya mbuni kuficha kichwa chake katika mchanga
pindi anapomuona adui. Mathalani chukua suala la muungano na suala la
kadhi,
haya tu yanaweza kutupa changamoto kubwa sana katika zoezi hili. Na kwa
maoni yangu tulitakiwa tuwe na muafaka wa kitaifa zamani sana juu masuala
kama haya na mengine.

Jamani nafikiria tu kwa sauti. Yawezekana huo ni wasiwasi wangu tu. Naomba
kusikia kutoka kwenu.

Selemani Rehani

MAJIBU YA DEUS KIBAMBA WA JUKWAA LA KATIBA
Ndugu Zangu, Watanzania wenzangu,

Nimesoma waraka wa Ndugu Selemani Rehani kwa umakini mkubwa sana. Mimi
nimekwishatoa kauli kuwa Mchakato wa Kupata Katiba Mpya hautaweza
kukamilika kabla ya 2015. Sababu kubwa ni nyingi lakini mbili tu kwa sasa,
Kwanza tumetumia mwaka mmoja na zaidi kujadili na kupitisha sheria ndogo
tu ya mabadiliko ya Katiba, joto likipanda na kushuka! Pili, utata wa
ibara ya 132(2) ya Katiba ya Zanzibar kwa marekebisho ya 2010 hata
haujaguswa. Kulingana na ibara hiyo, sheria ya mabadiliko ya katiba
italazimika kwenda baraza la wawakilishi ikapitishwe na kuridhiwa ndipo
iweze kutumika Zanzibar. Hili lingefanyika miezi kadhaa iliyopita
kusingekuwa na shida kubwa. Baada ya joto la mihadhara, sioni BLW
likiipitisha sheria hii.

Hoja nyingine zinazoonesha haja ya haraka ya kufanyia marekebisho katika
sheria ya mabadiliko ya katiba nimezitoa katika mada zangu za hivi
karibuni kwa wahariri wote wa vyombo vyote vya habari, Nashera Hotel,
Morogoro na kwa Maaskofu na wachungaji wa CCT, Dodoma wiki hii.

Nimehariri hoja hizo na kupeleka The Citizen kwa uchapishaji katika Sunday
Citizen kesho kutwa.

Kwa sasa, mchakato huu uko njia panda ya aina yake. Hata hivyo, kuna
hatari kubwa ya mchakato huu kusuasua. Watanzania wengi hawana imani na
vyombo vingi sana vya kisiasa kwa sasa. Tume ya uchaguzi ni mojawapo!

Ingawa ningependa tujipe muda wa kutosha kuandika Katiba Mpya hata kama
deadline itavuka 26 April 2014 iliyotangazwa na serikali ya Tanzania,
sipati picha tutakavyoendesha uchaguzi wa 2014 na ule wa 2015 kwa Katiba
hii hii, sheria hizi hizi na Tume ya uchaguzi hii hii.

JUKWAA LA KATIBA TANZANIA linaandaa tukio kubwa kutoa fursa kwa watanzania
kutathmini na kutafakari tulikotoka, tulipo na tuendako kuhusu mchakato wa
Katiba Mpya Tanzania.

Nyote mtajulishwa na kualikwa rasmi! Nafurahia mjadala huu.

Wasaalam,
Mjadala huu umetokea kwanza wanabidii

No comments: