Na Raymond Kaminyoge
WAKATI Mbunge wa Bahi, Omar Badwel anatarajiwa
kufikishwa mahakamani leo kwa tuhuma za kupokea rushwa, Mbunge wa Kigoma
Kusini, David Kafulila ameilipua Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa
(LAAC) kuwa imekithiri kwa rushwa.
Kutokana na tuhuma hizo, Kafulila amemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda kuvunja kamati hiyo, vinginevyo yeye atajiondoa.
Pia
mbunge huyo ameitaka Kamati ya Maadili kulitumia Bunge kumvua ubunge,
Badwel, kutokana na tuhuma za kupokea rushwa zinazomkabili.
Kafulila
alisema hayo jijini Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa
habari huku akisisitiza kuwa, wananchi hawatakuwa na imani tena na
kamati hiyo.
“Ikumbukwe Juni 13, 2011 nilieleza bungeni namna
wabunge wa Kamati ya LAAC wanavyoomba rushwa kwa watumishi wa Serikali,
huku nikimtaja kwa jina Mbunge wa Bahi, Omary Badwel kuwa ni miongoni
mwao,” alisema Kafulila ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi ya Takukuru, Alex Mfungo alisema juzi kuwa mbunge huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema hana taarifa zozote za mbunge huyo kukamatwa.
“
Sina taarifa za mbunge kukamatwa na Takukuru, kama ni kweli tutaletewa
taarifa rasmi ndipo ninaweza kuzungumzia suala hilo,” alisema Makinda
kwa simu.
Awali, Kafulila alisema licha ya kutoa taarifa hiyo
bungeni na kumwandikia Spika kuhusu vitendo vya rushwa vya baadhi ya
wajumbe, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
“ Nilijitoa mhanga
kwa kutaja majina ya wabunge wanaoomba rushwa kwa watumishi wa Serikali,
lakini hatua hazikuchukuliwa, sasa leo Takukuru wamemtia mbaroni mmoja
wao, bado hamuamini,” alisema Kafulila.
“ Sasa naomba niweke
wazi kwamba kama Spika hataivunja kamati hii na kuunda nyingine
nitajiondoa kwenye kamati kwa sababu itakuwa imepoteza imani kwa
wananchi,” alisema Kafulila.
Alisema kamati hiyo imepoteza
uhalali na sifa za kuendelea kuzikagua hesabu za serikali za mitaa kwa
sababu wajumbe wake wanatuhumiwa kwa rushwa.
Kafulila alisema ni wajibu wa Spika kutafakari upya kuhusu hadhi ya kamati hii na kuipanga upya kwa kuzingatia masilahi ya umma.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema, ndiyo yenye jukumu la kusimamia hesabu za serikali za mitaa.
“Serikali
legelege ni matokeo ya Bunge legelege kwa kuwa ni kazi ya Bunge
kusimamia na kuidhibiti Serikali kikatiba,” alisema Kafulila.
Mbunge huyo wa Kigoma Kusini aliitaka Bunge kuweka azimio la kumvua ubunge Badwel kwa vitendo vyake vya rushwa.
“
Kamati ya Maadili ya Bunge ifanye hivyo ikiwa ni hatua za kinidhamu
kuchukuliwa kwa mbunge huyo kwa tukio hilo la aibu,” alisema.
Kafulila
alisema hata mabunge ya Jumuiya za Madola ambalo Tanzania ni miongoni
mwao, huchukua hatua za kinidhamu za kuwavua wabunge wanaotuhumiwa kwa
makosa ya aibu kabla ya mahakama hazijatoa uamuzi.
Kwa mujibu wa
Kafulila, Bunge la Uingereza limeshachukua hatua za kuwavua ubunge
watuhumiwa zaidi ya 59 ili kujenga imani ya wananchi kwa Bunge lao.
“Kwa
hiyo nafahamu kwa kutumia azimio, Bunge lina uwezo wa kumvua madaraka
mbunge yeyote ambaye amefanya vitendo vya aibu vya kuliaibisha Bunge,”
alisema.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Ibara ya 71(1) (d) Mbunge anaweza kupoteza nafasi yake ikiwa
itathibitishwa kwamba amevunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi
wa Umma.
Mbunge huyo wa Bahi, Badwel, na Mbunge wa Mbozi
Mashariki, Godfrey Zambi wote wa CCM ni miongoni mwa wabunge waliotajwa
na Kafulila (NCCR-Mageuzi) katika Bunge la bajeti mwaka jana kwamba
aliwakuta wakiomba rushwa kwa viongozi wa halmashauri ambayo hakuitaja.
Juzi
saa 9.00 alasiri, Badwel alikamatwa na Takukuru akidaiwa kupokea rushwa
kutoka kwa watumishi wa Serikali katika Hoteli ya Peacock jijini Dar es
Salaam.
No comments:
Post a Comment