Monday, June 25, 2012

Mgomo wa madaktari wazorotesha huduma

HUDUMA za matibabu kwa wagonjwa jana ziliendelea kuzorota katika baadhi ya hospitali, hali iliyotajwa kuwa inatokana na mgomo uliotangazwa na madaktari.Madaktari walitangaza mgomo wa kutotoa matibabu nchi nzima kuanzia juzi, wakishinikiza Serikali kutekeleza madai yao likiwamo la kuboreshewa mishahara na mazingira ya kazi.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),Taasisi ya Mifupa (MOI) na hospitali nyingine za Jiji la Dar es Salaam, umebaini kuzorota kwa utoaji huduma.

Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, uchunguzi ulibaini mbali na ulinzi kuimarishwa, huduma za matibabu kwa wagonjwa zilizorota, na katika baadhi ya wodi wagonjwa walikuwa hawajatembelewa na madaktari tangu Ijumaa.

Mmoja wa watu ambao wanauguza mgonjwa wao katika wodi namba 4 katika Jengo la Mwaisela, Vicky Rehani alisema mgonjwa wao alipelekwa hospitalini Ijumaa na hadi jana, alikuwa hajapata huduma yoyote akiwa wodini.

"Mapokezi kweli alionana na daktari akamuandikia dawa na kulazwa katika wodi hii, lakini cha ajabu hadi sasa hakuna huduma yoyote ambayo ameipata," alisema .

Katika wodi zilizopo katika Jengo la Kibasila baadhi ya wagonjwa walidai kuwa, kuna madaktari ambao wamefika wodini, lakini hawakufanya mzunguko kama ilivyo kawaida, na hawakuwa na wasaidizi wao ambao ni wanafunzi wanaokuwa katika mafunzo kwa vitendo.

Daktari mmoja aliyekutwa katika wodi ya Sewahaji (alikataa kutaja jina lake), alipoulizwa kuhusiana na kuwapo kwa mgomo alikataa kusema lolote kwa madai kuwa si Msemaji wa MNH.

"Siwezi kusema lolote, kwani hata mimi mwenyewe nimefuata matibabu," alisema daktari huyo na kuongeza kuwa kama mwandishi anataka kujua kama kuna mgomo au la, basi aende hospitalini hapo kesho.
Hata hivyo, uchunguzi zaidi hospitalini hapo umebaini kupigwa marufuku kwa mikusanyiko ya aina yoyote na hata bustani inayotumiwa na wagonjwa na jamaa zao ambayo ipo mbele ya Jengo la Mwaisela, ilikuwa chini ya ulinzi.

"Hapa haruhusiwi mtu yeyote kukaa, amri hiyo imetoka tangu jana (juzi)," alisema mlinzi aliyekutwa eneo hilo na kuongeza kwamba hata mikusanyiko ambayo haieleweki imepigwa marufuku ndani ya eneo la hospitali.
Hali hiyo pia iliwakuta baadhi ya waandishi wa habari ambao walifika hospitalini hapo na kujikuta wakizuiwa na walinzi kuingia katika baadhi ya wodi.

Msemaji wa Hospitali hiyo, Aminieli Eligaesha wakati wote simu yake ilipokuwa ilikuwa inaita bila kupokelewa, hali ambayo ilijitokeza pia juzi Jumamosi.

Wakati hali ikiwa hivyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Moi, uchunguzi uliofanywa katika Hospitali za Mwananyamala, Amana na Temeke ulibaini kuwa huduma ziliendelea kwa kusuasua huku baadhi ya wahudumu wakisisitiza hatma ya mgomo huo itafahamika leo.

“Ukitaka kujua sura ya mgomo subiri kesho (leo) itadhihirika kama kweli madaktari wamegoma au la, lakini kwa leo huduma zinaendelea kwa kusuasua, bado tunaangalia Serikali itatoa majibu gani,” alisema mmoja wa madaktari katika Hospitali ya Amana, ambaye hakutaka jina lake kutajwa.
Aliongeza kuwa jana haikuwa siku ya kugoma, bali ni kushinikiza Serikali kutekeleza madai yao na kwamba, kama itaendelea na msimamo wake huduma zote zikiwamo za dharura zitasitishwa.

Hata hivyo, huduma katika Hospitali ya Amana jana zilikuwa zikiendelea huku baadhi ya wagonjwa wakisema kasi ya upatikanaji matibabu ni tofauti na kipindi ambacho mgomo ulikuwa haujatangazwa.
Katika Hospitali ya Mwananyamala, hali ya matibabu pia iliendelea kwa kusuasua na ulipotafutwa uongozi wa hospitali hiyo kuzungumuzia hali hiyo juhudi hizo hazikuzaa matanda.

Katika Ofisi ya Utawala, mwandishi alikutana na mmoja wa wafanyakazi ambaye alikataa kutaja jina na kueleza kuwa Mganga Mkuu alikuwa amekwenda kutembelea wagonjwa wodini.

“Mimi si msemaji. Hili anaweza kuzungumza Mganga Mkuu, lakini amekwenda kutembelea wagonjwa wodini na ameniambia akimaliza kazi hiyo anakwenda kufanya shughuli ya upasuaji, hatakuwa na muda wa kuzungumza nanyi,” alisema ofisa huyo.

Wakati hali ikiwa hivyo Mwananyamala, katika Hospitali ya Temeke pia huduma ziliendelea kutolewa huku baadhi ya watu waliokwenda kuhudumia wagonjwa wao wakibainisha kuwa kasi imepungua.
Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Edwin Chitage alisisitiza, “Sisi tunaendelea na mgomo kama kawaida, tutafanya hivyo hadi Serikali itakapotekeleza madai yetu, na hadi sasa hatujapata taarifa zozote kutoka serikalini,” alisema Chitage.

KCMC vuguvugu laendelea
 Katika Hospitali ya Rufaa KCMC Moshi, madaktari ambao hawako zamu wamekubaliana kufanya kikao cha dharura kuhakikisha hakuna daktari atakayeingia kazini leo.

Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya madaktari ambao hawakupenda majina yao yaandikwe gazetini, walisema wamepanga kufanya kikao cha pamoja ambacho kitaweka mikakati ya jinsi ya kufanya mgomo mkali leo, tofauti na ilivyokuwa juzi na jana.

“Mgomo uko palepale kama unavyoona walioko kazini ni wale wenye zamu, tumewataka wasaini, lakini kesho hakuna atakayeingia kazini na mgomo utakua mkali, tumekuwa wapole sana, lakini Serikali imetupuuzia,” alisema mmoja wa madaktari.

Chama cha Tiba Asilia
Kwa upande wa Chama cha Watabibu wa Dawa za Asili (ATME), kimewataka madaktari kuacha kugoma na badala yake waendeleze mazungumzo na Serikali ili waweze kufikia muafaka.

Chama hicho kupitia Mwenyekiti wake, Abudulhaman Simba, kimesema mgomo wa madaktari unahatarisha uchumi wa taifa na haki za wagonjwa, hasa wale wenye kipato cha chini.

Mkoa wa Mwanza
Mkoani Mwanza madaktari walio kwenye mafunzo na wale walioajiriwa waliendelea na mgomo wao jana.

Mmoja wa madaktari bingwa wa Hospitali ya Rufaa Bugando ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema mgomo huo kwa sasa haujaonyesha athari kubwa kutokana na kuwa siku za mapumziko.

"Leo (jana) na jana (juzi), hapajatokea athari za mgomo, tunadhani athari itakuwa kubwa katika siku za kesho (leo) na kuendelea kwani wakigoma hawa wa mafunzo na hao wengine, kazi inakuwa kubwa kwetu," alisema.

Katika hatua nyingine, mgomo huo haukugusa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwani huduma ziliendelea kama kawaida.

Gazeti hili jana lilishuhudia wagonjwa wakipewa huduma za matibabu pamoja na mgomo uliotangazwa kudai maslahi yao.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk Omary Chande alisema pamoja na kutangazwa mgomo wa madaktari, Mount Meru haijaathirika na mgomo huo.

Wagonjwa waondolewa Mbeya
Katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, mgomo uliendelea na kusababisha baadhi ya wagonjwa kuanza kuondolewa hospitani hapo pia na ile ya wazazi, Meta, kwa ajili ya kwenda kutafuta matibabu kwenye hospitali nyingine za watu binafsi.

Mwananchi jana lilishuhudia baadhi ya wagonjwa wakipandishwa kwenye magari na kuondoka kwenda kutafuta matibabu hospitali za watu binafsi.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk Eliuter Samky alipoulizwa alikiri kuwepo kwa mgomo wa madaktari walio kwenye mafunzo ya vitendo wanaofikia 70.
Hata hivyo, Dk Samky alisema anao uhakika kuwa madaktari 10 bingwa waliojariwa na Serikali wataendelea kufanya kazi, na hivyo huduma kwa wagonjwa hasa wale walio katika hali ngumu na wale wa dharura zitaendelea kupatikana.

Ombi la wagonjwa
Wagonjwa jijini Tanga,wameiomba Serikali kutekeleza kwa vitendo ahadi iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa madaktari ili kuondoa misunguano iliyojitokeza.

Ombi hilo walilitoa jana walipokuwa wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi katika wodi za majeruhi na watoto katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo.

"Tunamuomba Rais atekeleze ahadi yake aliyotoa kwa madaktari, wanapogoma sisi walalahoi ndo tunaokufa na wengine kupata madhara zaidi, lakini wao wanapougua wanakwenda hospitali za nje ya nchi," alisema Adamu Abdurahman aliyelazwa katika wodi ya majeruhi ya
Galanosi.

Madaktari waliokuwa zamu katika wodi za Hospitali hiyo walisema hawaamini kama kweli Serikali haina fedha za kuwalipa, kwani kunapotokea masuala mengine imekuwa ikitoa bila ya matatizo.

Joseph Zablon na Geofrey Nyang’oro, Rehema Matowo, Nora Damian, Godfrey Kahango Mbeya, Filbert Rweyemamu, Arusha na Burhani Yakub,Tanga

Source: www.mwananchi.co.tz

No comments: