Kambi
ya upinzani Bungeni inayoundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) imetaja vipaumbele vya bajeti yake kwa mwaka wa fedha wa
2012/2013, huku ikiahidi kuibana serikali kuhusiana na masuala
mbalimbali.
Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe, alitaja vipaumbele hivyo
jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema katika bajeti mbadala ya 2012/13, Kambi ya Upinzani itajikita
katika maeneo ya kuendelea kushinikiza kupunguzwa kwa misamaha ya kodi
kutoka asilimia nne hadi asilimia moja ya Pato la Taifa.
Kwa kujibu wa Zitto, kipaumbele kingine ni kuelekeza rasilimali fedha
kwenye maendeleo vijijini hasa kujenga miundombinu kama barabara za
vijijini na umeme vijijini na pamoja na kuelekeza fedha za kutosha
kukarabati reli ya kati na kufufua njia za reli za Tanga, Moshi na
Arusha.
Alisema vipambele vingine ni kuongeza wigo wa kutoza tozo la ujuzi
(Skills Development Levy), ambapo sasa waajiri wote walipe ikiwemo
serikali na mashirika ya umma.
“Pia kupunguza tozo hii mpaka asilimia nne ambapo 1/3 itaenda VETA na
vyuo vya ufundi na 2/3 itaenda Bodi ya Mikopo ili kukabili changamoto ya
mikopo kwa wanafunzi,” alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, kipaumbele kingine ni kushusha kima cha chini cha
Kodi ya Mapato (PAYE) mpaka asilimia 9 ili kuwezesha wananchi wa hali ya
chini kubaki na fedha za kutumia na kukuza uchumi.
Alitaja kipaumbele kingine kuwa ni kuongeza mapato ya ndani na kupunguza
mikopo ya kibiashara kwa kuhakikisha mapato ya ndani yanafikia asilimia
20 ya Pato la Taifa, kuongeza nguvu za kisheria na udhibiti ili Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) ikusanye mapato zaidi kwenye kampuni za simu
na kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, mafuta na gesi.
Pia, kutayarisha Taifa kuwa na uchumi wa gesi, kupunguza, kufuta kodi
kwenye bidhaaa za vyakula kwa muda maalum ili kushusha mfumuko wa bei.
Vile vile kuweka mfumo mpya wa elimu kwa kushirikisha sekta binafsi
katika kutoa elimu kwa ubora zaidi, ikiwemo kuundwa kwa chombo cha
udhibiti wa elimu.
“Kutoa vipaumbele na unafuu vya kikodi kwa viwanda vya ndani
vinavyotumia malighafi za nchini hasa za kilimo na zenye kuongeza ajira
kama korosho, pamba na mkonge,” alisema Zitto.
Alisema kambi hiyo itaendelea kufuatilia kwa karibu suala la kukua kwa
deni la Taifa ambalo limefikia Sh. trilioni 22 na kutaka ukaguzi maalum
kuhusu akaunti ya deni la Taifa.
Zitto aliahidi kuwa, kambi yake itaibana serikali wakati wa kikao cha
Bunge kitakachoanza Juni 12, mwaka huu, kutokana na kuongezeka kwa deni
la Taifa na kutaka ukaguzi maalum kuhusu akaunti ya deni hilo.
Zitto alisema hatua hiyo inatokana na deni la Taifa kuwa sawa na asiliami 48 ya Pato la Taifa.
Alisema serikali imeshindwa kushusha misamaha ya kodi ya asilimia tatu
ambayo ni Sh. Trioni 1.03 sawa na fedha zote ambazo serikali ya Tanzania
inapata kutoka kwa wahisani wanaochangia katika bajeti ya serikali.
Alisema Watanzania lazima wafahamishwe fedha zinazokopwa zinawanufaisha katika mambo gani au zinaishia kwa watu.
“Bungeni tutakwenda kuhoji serikali iweze kutupa majibu kwanini
imeshindwa kushusha misamaha ya kodi kama ambavyo aliyekuwa Waziri wa
Fedha, Mustafa Mkulo, aliahidi kwamba serikali itashusha hadi kufikia
asilimia moja, lakini hadi sasa hakuna utekelezaji,” alisema Zitto.
Alisema kama Tanzania ingekuwa na misamaha sifuri kusingekuwa na haja ya
misaada toka kwa wahisani na kwamba kambi ya upinzania bungeni
itaendelea kusisitiza hivyo kwa kuhakikisha inashuka kutoka asilimia
tatu hadi kufikia moja.
Zitto pia alisema wakati wa kikao cha Bunge, Kambi ya Upinzani Bungeni
itakwenda kuibana serikali kuuzwa kwa hisa asilimia 26 ilizokuwa
inamiliki katika kampuni ya simu ya Tigo ambazo zimeuzwa kwa bei ya
kutupa.
“Serikali ilikuwa na hisa asilimia 26, lakini mwezi Februari 2004
iliziuza kwa thamani ya Dola za Kimarekani 700,000 ambazo ni chini ya
Shilingi bilioni moja wakati hivi sasa kampuni ya Tigo mapato yake kwa
mwezi ni Sh. bilioni 20,” alisema Zitto.
Alisema tathmini iliyofanywa na kamati LAAC ilibaini kuwa kuna upotevu
wa kodi zaidi ya Sh. bilioni 250 katika makampuni ya simu na hii
inatokana na Mamlaka ya Mawasilianio Tanzania (TCRA) na Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) kutoshirikiana katika suala la ukusanyaji wa
mapato.
Zitto alisema ili kuhakikisha makampuni ya simu hayakwepi kulipa kodi ya
serikali, kuna haja ya kuiongezea nguvu sheria ili kuhakikisha
makampuni hayo yanalipa kodi inavyostahili.
Aliongeza kuwa, Machi na Aprili mwaka huu, TRA imefanikiwa kuongeza
ukusanyaji wa mapato katika makampuni ya madini, lakini hata hivyo, bado
kuna ukwepaji mkubwa wa kodi katika makampuni ya mafuta.
“Nchi yetu hivi sasa ina meli nyingi zinazosafirisha mafuta, lakini
hayalipiwi kodi, suala hili kama kambi ya upinzani tutakwenda kuisimamia
kuhakikisha makampuni hayo yanalipa kodi,” alisema Zitto.
POAC YABAINI MADUDU CHC
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) imebaini
“madudu” na wizi wa mabilioni ya fedha na mali kupitia mchakato wa
kuuza mashirika ya umma ambapo imeshtushwa kuambiwa kwamba Shirika la
Usagishaji la Taifa (NMC) bado lipo hai licha ya Watanzania wengi
kufahamu kwamba lilishakufa.
POAC imeambiwa kwamba NMC lipo hai na lina mfanyakazi mmoja ambaye ni
mkurugenzi na anakusanya fedha kutoka kwenye vitega uchumi mbalimbali
vya shirika hilo, yakiwemo majengo na kujilipa mshahara na kwamba hakuna
mtu anayejua anapata kiasi gani cha fedha, anazipeleka wapi na hajawahi
kukaguliwa na taasisi yoyote ya serikali tangu mwaka 2008.
Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe, alisema wajumbe wa kamati yake
walishtushwa na taarifa hiyo kwamba NMC bado linafanya kazi ambapo
ameunda tume ndogo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina ili kujua mali
halisi zilizopotea kupitia mchakato wa kuuza mashirika ya umma nchini.
Zitto alisema kamati itakayoundwa itaanza kufanya kazi yake baada ya kupata kibali rasmi cha Spika la Bunge , Anne Makinda.
Alisema kamati yake imeshindwa kuendelea na shughuli za kuhoji mchakato
huo wa kuuza mashirika ya umma kutokana na unyeti wa suala hilo na
kwamba kwa haraka haraka wamebaini “madudu” ya kutisha.
Kamati ya Zitto iliyasema ha jana baada ya kukutana na uongozi wa
Shirika la Consolidated Holding (CHC) ambalo zamani lilikuwa
likijulikana kama PSRC.
“Kwa kweli hata wajumbe hawa wa Kamati yangu baada ya kusikia taarifa
hii kutoka CHC wamejiuliza maswali mengi kama mnayojiuliza kuhusiana na
hali hii ilivyo kwamba inawezekana vipi NMC iwepo na kubakia na
mfanyakazi mmoja ambaye hajawahi kukaguliwa wala hafahamiki kwa serikali
wala kwa taasisi yoyote ya serikali,” alisema Zitto.
Alifafanua kuwa kamati itakayoundwa ndiyo itakayoeleza kwa kina ni kitu
gani kilikuwa kikifanyika tangu serikali ilipofanya uamuzi wa kuuza
mashirika yake na ni mali gani zilizobakishwa na zipo wapi na
zinaangaliwa na nani.
“Tusipokuwa makini na suala hili, nchi itapoteza mali nyingi huku
zikipotelea mikononi mwa watu wachache ambao hawataki kusema ukweli
wanashikilia mali gani za serikali',” alisema Zitto.
Alisema ufisadi katika mchakato huo ni zaidi ya uliowahi kutolewa
taarifa kwa umma ukiwemo wa kuuza baadhi ya viwanja vya badhi ya
mashirika yaliyouzwa.
Aliongeza kuwa kikao cha kamati yake na CHC jana kilimalizika bila
kufikia mwafaka wowote na kwamba kamati itakayoundwa ndiyo itayoibua
uozo wote tangu mchakato wa uuzaji wa mashirika ya umma ulipoanza.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment