Friday, June 8, 2012

Mwakyembe: Nimemng’oa bosi ATCL kwa ufisadi

ASEMA WANAOUNUNG’UNIKA WAKO HURU KUJIONDOKA

Na Fidelis Butahe
SIKU nne baada ya kung’olewa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Paul Chizi, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ameamua kuanika tuhuma za ufisadi zinazodaiwa kufanywa na kigogo huyo.Miongoni mwa tuhuma hizo ni kuingia mkataba wa kununua ndege bila kumhusisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG) na kununua sare 15 za watumishi wa ndege kwa dola 50,000 za Marekani.

Juni 5, Dk Mwakyembe alitengua uteuzi wa Chizi na kumteua rubani wa muda mrefu, Kapteni Lusajo Lazaro kukaimu nafasi hiyo, akisema uteuzi ulikiuka Sheria za Utumishi wa Umma.

Mbali na kutengua uteuzi huo, pia alitangaza kuwasimamisha kazi vigogo wengine wanne wa shirika hilo, hatua ambayo ilianza kuibua malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi kwamba hatua hiyo ilitokana na majungu na ukabila.

Waliosimamishwa kazi na Dk Mwakyembe ni Kaimu Mkurungenzi wa Uhandisi, Jonh Ringo, Mwanasheria  ,Amini Mziray, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Justus Bashara na Josephat Kagirwa ambaye alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Biashara.

Jana, waziri huyo wa uchukuzi aliamua kufafanua tuhuma moja hadi nyingine zinazomhusu kigogo huyo na wenzake na kusema, mbali ya tuhuma za Chizi, wakurugenzi wawili wa shirika hilo walikwenda kushonesha sare 15 za wahudumu wa ndege nchini China kwa gharama ya dola 50,000 za Marekani (karibu Sh80 milioni).

Akizungumza na wafanyakazi wa shirika hilo katika Uwanja wa Ndege wa zamani (Terminal One) jijini Dar es Salaam, Dk Mwakyembe alisema kutokana na hali hiyo, ameagiza kujazwa kwa nafasi zilizo wazi na kuwaonya watakaozichukua, kuhakikisha wanachapa kazi ili ATCL ipige hatua na kama wakishindwa watakuwa wamejiondoa wenyewe.

Dk Mwakyembe alitoa miezi mitatu kwa shirika hilo kuanza kujiendesha kwa faida, ikiwa ni pamoja na kupata fedha za kuwalipa wafanyakazi wake.

“Kwa kasi niliyoanza nayo watu kama Chizi ni lazima wakae pembeni, ni mtaalam katika masuala haya, lakini tatizo lake hakuwa muwazi,” alisema Dk Mwakyembe.Chizi hakupatikana jana kuzungumzia tuhuma hizo, wakati wote Mwananchi ilipompigia simu yake ya kiganjani, ilikuwa imezimwa.

Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, alitumia Saa 1:17 kuzungumza na wafanyakazi hao na kufafanua kwamba Serikali imechoka kutoa fedha za kuliendesha shirika hilo, akihoji iweje mashirika mengine ya ndege yaweze kusimama yenyewe, lakini  ATCL iishindwe.

“Tunaipenda ATCL iendelee na tunachukua hatua za kila aina ila tukiona tunashindwa tutaachana nalo ili, fedha zinazotumika hivi sasa zipelekwe kufanyia mambo mengine ya maendeleo,” alisema Dk Mwakyembe.

Tuhuma
Akichambua tuhuma moja hadi nyingine za ukiukwaji wa sheria na taratibu, Dk Mwakyembe alianza kwa kutolea mfano mkataba tata baina ya shirika hilo na Air Bus ambao umeifanya nchi kudaiwa Sh69 bilioni na kusisitiza kuwa, kutokana na hali hiyo Serikali haikuwa tayari kufumbia macho mambo mengine ya ovyo yaendelea katika shirika hilo.

Alisema wafanyakazi wote wa ATCL ambao wananung’unika baada ya kutengua uteuzi wa Chizi wako huru kuondoka katika shirika hilo, huku akionya atawatimua wengi watakaofanya mambo kinyume.

“Nilipoteuliwa kuwa waziri wa uchukuzi siku chache baadaye nilisikia ATCL wanaleta ndege mpya, nilimwita Katibu Mkuu wa wizara anipe ufafanuzi wa jambo hilo, lakini, akaniambia hafahamu lolote,” alisema Dk Mwakyembe.

Aliongeza, “Ndege hiyo ilikodishwa na kutua nchini kwa mara ya kwanza mwezi uliopita kutokana na iliyokuwapo kuanguka mkoani Kigoma. Ndege hiyo aina ya Boeing 737-500 imekodishwa kutoka Kampuni ya Aero Vista ya Dubai.”

Dk Mwakyembe kwa sauti ya ukali alisema, “Niliamua kuwaita wakurugenzi wa ATCL ofisini kwangu saa 3 asubuhi, lakini wakaja saa nne na nusu, pamoja na hayo walinieleza kuwa jambo hilo liko safi na limeshafika kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”

Alisema baada ya siku moja, alipata taarifa kutoka ofisi ya AG ikieleza kwamba hawana mkataba huo.

“Nikaona jambo zito kidogo, nikaamua kukutana na wale wawekezaji ambao walinionyesha mkataba ule ambao ulipitishwa bila wizara kujua, jambo hilo nililihoji pia…, nawambia ukweli mkataba huu niliuona upande wa pili sio kwa viongozi wa shirika,” alisema Dk Mwakyembe.

Alisema hivi sasa mchakato wa kuchunguza mikataba hiyo umeshaanza na kusisitiza kuwa, hiyo ndio ilikuwa moja ya sababu ya kumng’oa Chizi.


Dk Mwakyembe alisema, “nchi haiwezi kuendelea kwa kukiukwa kwa sheria za ununuzi na ajira. Hata Kapteni Lazaro naye ameponea chupu chupu maana kabla ya kuwang’oa wakurugenzi tulipitia mafaili yao.”

“Msitegemee kubebwa ndugu zangu, nawaomba mchape kazi, mishahara yenu sio mizuri, lakini mkiweza kusimama mtakuwa na uwezo wa kujipangia hata mishahara,” alisema Dk Mwakyembe.

Alisema kwa kutambua mchango wa ATCL, Serikali imepata Sh4.9 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya ndege ya shirika hilo na kuwataka kuzitumia kwa ufanisi fedha za shirika hilo.“Hivi sasa inatakiwa kila baada ya miezi mitatu tunakutana na kuzungumza,” alisema Dk Mwakyembe.

Kapteni Lazaro aahidi ushirikiano
Kwa upande wake, Kapteni Lazaro aliahidi kuyazingatia yote yaliyozungumzwa na waziri huyo, huku akiomba shirika hilo kuongezewa muda zaidi kwa kuwa miezi mitatu ni michache ili liweze kujitegemea.


Kupanda/kushuka  ATCL
ATCL ni kampuni iliyoanzishwa baada ya Shirika la Ndege la Tanzania ATC kuingia ubia na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) mnamo mwaka 2002.

ATCl ni moja ya mashirika ya ndege yaliyoonyesha kukua kwa kasi miaka ya 1980 na 1990, lakini lilianza kuyumba kutokana na uendeshaji mbovu na hali ikawa mbaya zaidi baada ya kuingia ubia na SAA.

Serikali iliingia mkataba wa ubia na SAA mwaka 2002 kwa matumaini kwamba itakua na kuwa moja ya mashirika makubwa ya ndege Afrika, lakini hali ikawa kinyume chake.

Kwenye mkataba huo, Serikali ikibakia na hisa 49 huku SAA ikiwa nazo 51, ambazo zilimfanya mbia huyo kuwa na nguvu ya kuamua mambo mengi.

Serikali ilivunja mkataba na SAA Septemba 2006, baada ya kubaini kuwa ATCL inazidi kudidimia kiuchumi huku madeni yakiwa yanaongezeka kadri muda ulivyokuwa unaenda.

No comments: