Ndugu Wananchi,
KAMA ilivyo ada, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa
kutujaalia uhai na kutuwezesha kumaliza mwezi Mei salama. Kwa kutumia
utaratibu wetu wa kuzungumza kwa njia hii kila mwisho wa mwezi, leo
nitazungumzia mambo matatu.
Mkutano wa G-8
Jambo la kwanza, ni suala la usalama wa chakula na lishe. Duniani,
inakadiriwa kuwa kuna watu milioni 925 wanaokabiliwa na njaa na lishe
duni. Kati ya hao Afrika ina watu milioni 239 ambao ni karibu theluthi
moja ya watu wote wenye tatizo la njaa na lishe duni kote duniani. Nchi
za Afrika zenye tatizo la njaa kiasi cha kuhitaji msaada wa chakula
kutoka nje ni 27. Kati ya hizo 11 zina matatizo makubwa zaidi. Tanzania
siyo miongoni mwa nchi hizo, hata hivyo bado hatujafikia kiwango cha
kujitosheleza kabisa. Hivi sasa tumefikia asilimia 95 na kila mwaka
yapo maeneo nchini yanayopata msaada wa chakula kutoka Serikalini.
Mwaka 2009, katika mkutano wao wa L’Aquila, Italia, viongozi wa nchi
nane tajiri kuliko zote duniani waliamua kuchukua hatua ya kuzisaidia
nchi zinazoendelea duniani kukabiliana na tatizo la njaa na lishe duni.
Katika mkutano ule waliahidi kutoa dola za Marekani bilioni 22 kwa
ajili hiyo. Tanzania tunategemea kupata dola milioni 22.9.
Katika mkutano wa nchi hizo maarufu kwa jina la G-8 uliofanyika Camp
David, Marekani tarehe 19 Mei, 2012, pamoja na mambo mengine
walizungumzia suala la usalama wa chakula na lishe barani Afrika. Nia
yao ni kuchangia katika juhudi zinazofanywa na mataifa ya Afrika zenye
shabaha ya kutokomeza matatizo hayo. Tofauti na walivyofanya L’Aquila,
safari hii waliamua kuchangia katika utekelezaji wa mipango na progamu
za kuendeleza kilimo katika nchi za Afrika hasa zile zinazolenga kujenga
usalama wa chakula na lishe.
Aidha, waliamua kuwa wataanza na nchi tatu na kuendelea kuziongeza
kila baada ya muda fulani, badala ya kuanza na nchi zote mara moja.
Hoja yao kubwa ni kwamba, wanataka kukusanya nguvu zao kwa nchi hizo
chache ili kufanya kazi ambayo itakuwa na matokeo yanayoonekana katika
kutokomeza njaa na kuboresha lishe. Hawakupenda kusambaza nguvu zao kwa
nchi nyingi na kuishia kutokufanya kazi ya maana.
Ndugu wananchi;
Bahati nzuri katika programu na mipango ya nchi iliyokubaliwa kwa awamu
ya kwanza ni Tanzania, Ethiopia na Ghana. Na, jambo la kufurahisha
zaidi ni kwamba mpango wetu wa kuendeleza kilimo katika ukanda wa Kusini
mwa Tanzania ulichukuliwa kuwa ni wa mfano. Maoni hayo ya nchi za G-8
ndiyo maoni ya WEF, Sekretariat ya NEPAD na Umoja wa Afrika, wote
wameona kuwa mpango wetu unafaa kuenezwa barani Afrika kama mkakati
sahihi wa kuendeleza kilimo, kujitosheleza kwa chakula na kupunguza
umaskini.
Katika Bara la Afrika mkakati huo sasa unaitwa Grow Africa
Partnership na tayari nchi saba zimeshajiunga nao. Nchi hizo ni
Tanzania, Msumbiji, Kenya, Rwanda, Ethiopia, Ghana na Burkina Faso.
Katika mkutano wa Camp David, nchi za Marekani, Japani, Uingereza,
Ujerumani, Ufaransa na Urusi zimeahidi kuchangia nchi yetu katika juhudi
zetu za kuendeleza kilimo na hasa zile zenye lengo la kujitosheleza kwa
chakula na kuboresha lishe nchini. Ukichanganya na ahadi iliyotolewa
na Umoja wa Ulaya katika mkutano huo, kiasi cha dola za Marekani milioni
897 zimeahidiwa kutolewa kwa nchi yetu kati ya sasa na mwaka 2015.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2006 tulizindua Programu Kabambe ya Kuendeleza Kilimo nchini
maarufu kwa kifupi kama ASDP. Kwa kirefu kwa lugha ya Kiingereza ni the
Agricultural Sector Development Programme. Programu hii ndiyo mwanzo
wa safari yetu ya uhakika ya kuleta mapinduzi ya kilimo nchini Tanzania.
Jambo la kwanza lililofanyika katika utayarishaji wa Programu hii ni
kutambua vikwazo vinavyozuia maendeleo ya kilimo nchini na kupendekeza
hatua za kuchukua za kuondosha vikwazo hivyo.
Mwaka 2008, katika tathmini iliyofanywa kwa ushirikiano wa Serikali
na Sekta Binafsi kwa uamuzi wa Baraza la Biashara Tanzania, ilidhihirika
kwamba sekta binafsi ambayo ni wadau muhimu, haijahusishwa vya kutosha
katika mikakati, mipango na programu za kuendeleza kilimo nchini. Kwa
pamoja ilikubaliwa kuwa kasoro hiyo iondolewe ili wadau wote
washirikishwe, yaani Serikali, wakulima wadogo, wakulima wakubwa na
sekta binafsi. Vilevile, sote tulikubaliana kutoa kipaumbele cha juu
kwa maendeleo ya kilimo. Kwa pamoja tuliafikiana kuwa mambo mengine
yanaweza kusubiri isipokuwa kilimo. Matokeo ya maelewano hayo ndiyo
yaliyozaa mkakati na kauli mbiu ya “Kilimo Kwanza”.
Ndugu Wananchi;
Tangu wakati huo, sekta binafsi nchini imekuwa inahusishwa na
kushirikishwa kwa karibu katika utekelezajiwa ASDP na kuendeleza kilimo
kwa jumla. Kwa upande mmoja sekta binafsi imekuwa inahusishwa katika
upatikanaji wa zana na pembejeo za kisasa za kilimo kwa wakulima. Kwa
ajili hiyo, wenzetu wa sekta binafsi wamekuwa wanategemewa kuleta na
kuuza matrekta, mitambo na vifaa mbalimbali vya kilimo pamoja na mbegu,
mbolea, dawa za kuua wadudu waharibifu wa mazao na za kukinga na kutibu
maradhi ya mimea na mifugo. Hali kadhalika, wamekuwa wanajihusisha na
ununuzi na usindikaji wa mazao ya mkulima na kuongeza thamani. Tunataka
tuachane na kuendelea kuuza nje mazao ya kilimo kama malighafi na
kununua bidhaa zilizotengenezwa na mazao hayo.
Upande mwingine tuliwategemea wenzetu wa sekta binafsi washiriki
kulima mashamba makubwa. Wasiache kazi ya kilimo kufanywa na wakulima
wadogo peke yao ambao uwezo wao si mkubwa wa kukabili matatizo ya
kuongeza tija. Nafurahi kwamba wito wangu huo waliupokea vizuri na
baadhi yao wameshaanza kufanya hivyo.
Ndugu Wananchi;
Swali kubwa walilouliza ndugu zetu hao siku ile ya tarehe 2 – 3 Juni,
2009 pale Kunduchi Beach Hotel ni kuhusu upatikanaji wa ardhi.
Niliwaeleza kuwa upo utaratibu mzuri wa kuwapatia wakulima wakubwa ardhi
ya kilimo na ufugaji. Utaratibu wenyewe ni kwamba kila wilaya
imetakiwa kutenga ardhi kwa ajili ya wakulima wakubwa. Hilo
likishafanyika, taarifa hutolewa kwa Kituo cha Uwekezaji na kuingizwa
katika kitu kinachoitwa Benki ya Ardhi. Mwekezaji anapojitokeza,
kulingana na aina ya kilimo anachotaka kujihusisha nacho, hugawiwa ardhi
hiyo. Ardhi hiyo ni ile ambayo siyo inayotumiwa na wakulima wadogo.
Katu hawanyang’anywi ardhi wakulima wadogo ili kuwapa wakulima wakubwa.
Hiyo siyo sera wala madhumuni na malengo ya ASDP au Kilimo Kwanza.
Nalifafanua hili kuondoa hofu iliyokuwepo na upotoshaji uliokuwa
unafanywa makusudi wa kuhusisha wakulima wakubwa na uporaji wa ardhi.
Siyo makusudio yake hata kidogo.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2010 tukapanua wigo wa ushiriki wa sekta binafsi kwa kuihusisha
sekta binafsi ya kutoka nje ya nchi. Mwaka huo pia, tukaamua kuipa
sekta binafsi lengo maalum la kutekeleza nalo ni kushiriki katika kilimo
cha kuhakikisha kuwa nchi yetu inajitosheleza kwa chakula na kupata
ziada kubwa ya kuuza nje, kwa majirani zetu na kwingineko. Shabaha yetu
hasa ilikuwa ni kujitosheleza kwa vyakula vikuu vya mahindi, mchele na
sukari.
Aidha, tuliamua pia kuwa, kwa kuanzia tuelekeze nguvu zetu kwenye
mikoa ya Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Iringa na Morogoro kwa vile mikoa hiyo
ndiyo ghala la chakula la nchi yetu. Kwa vile mikoa hiyo ipo ukanda wa
kusini ndio maana ikaja kuitwa Southern Agriculture Growth Corridor of
Tanzania au SAGCOT. Tumeamua tukusanye nguvu za Serikali, wakulima,
sekta binafsi na washirika wetu wa maendeleo kuwekeza katika kuendeleza
kilimo katika mikoa hiyo.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mpango wa kuendeleza kilimo katika ukanda wa SAGCOT una
shabaha kuu mbili: Kwanza kabisa mpango unalenga kuboresha kilimo cha
wakulima wadogo ili kitoke kuwa duni na cha kujikimu na kuwa cha kisasa
na kibiashara. Chini ya mpango huu wakulima wadogo watasaidiwa na
kuwezeshwa kupata na kutumia zana na pembejeo za kisasa za kilimo. Pia
watawezeshwa kupata mikopo kwa ajili ya kilimo na masoko ya uhakika na
yenye bei nzuri kwa mazao yao. Vile vile, huduma muhimu zitaimarishwa.
Hapa tunazungumzia maafisa ugani na miundombinu ya umwagiliaji,
barabara, umeme, maji safi na teknolojia ya habari na mawasiliano.
Pili, kwa pale inapowezekana kwa maana ya upatikanaji wa ardhi na
aina ya mazao, kuihusisha sekta binafsi katika kilimo. Tayari
utekelezaji wa mpango wa SAGCOT umeanza. Kamati ya Utendaji imeshaundwa
na Sekretariati yake imeshateuliwa. Aidha, Mfuko wa Kuchochea
Uwekezaji umeshaanzishwa na unaendelea kuchangiwa fedha.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa malengo ya SAGCOT kwa kilimo cha mpunga na kuongeza
uzalishaji wa sukari yameanza kutekelezwa. Matayarisho yanaendelea kwa
kilimo cha mahindi na mazao mengine.
Mpango huu utakapofanikiwa utakuwa na manufaa makubwa. Nchi yetu
itajitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada kubwa ya kuuza nje.
Inakadiriwa kuwa mapato yatokanayo na kilimo katika ukanda huu yatafikia
dola bilioni 1.2 kwa mwaka, watu 420,000 watapata ajira na watu
2,000,000 wataondokana na umaskini uliokithiri.
Uwekezaji wake ni mkubwa na kwamba kiasi cha dola bilioni 3.4
kinahitajika kwa kipindi cha miaka 20. Kwa ushirikiano uliopo baina ya
Serikali, sekta binafsi na wabia wetu wa maendeleo wakiwemo wa nchi za
G-8, hayo yote yanawezekana.
Ndugu Wananchi;
Tukijitosheleza kwa chakula na kwa maana pana ya chakula chenye lishe
bora tutakuwa tumefanikiwa kupata ufumbuzi wa tatizo kubwa la ukosefu wa
lishe bora miongoni mwa wananchi wa Tanzania. Wanaoathirika sana na
tatizo hili ni kina mama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya
miaka mitano. Ukosefu wa lishe bora huchangia asilimia 20 ya vifo vya
kinamama wajawazito nchini na theluthi moja ya watoto wa umri wa chini
ya miaka mitano. Aidha, asilimia 42 ya watoto wa umri wa chini ya miaka
mitano wamedumaa na asilimia 16 wana uzito mdogo kulingana na umri wao
na asilimia 59 wana upungufu wa damu. Kwa kina mama wajawazito asilimia
41 wana matatizo ya upungufu wa damu. Hali hii sio nzuri hata kidogo
lazima tuibadili na tunaweza kufanya hivyo. Tunao mkakati wa kitaifa wa
kuboresha lishe ambao kwa sehemu kubwa utanufaika sana na kufanikiwa kwa
mkakati wa kujitosheleza kwa chakula.
Mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
Ndugu Wananchi;
Jana tarehe 31 Mei, 2012 nilishiriki katika sherehe za ufunguzi wa
Mkutano wa 47 wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na
Mkutano wa 38 wa Mfuko wa Maendeleo wa Afrika. Hii ni mara ya kwanza
katika historia ya Benki hii tangu ianzishwe mwaka 1964 kwa nchi yetu
kuwa mwenyeji wa mikutano hii inayofanyika kila mwaka. Ni heshima kubwa
sana kwa nchi yetu, nami kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote,
nimemshukuru sana Rais wa Benki hiyo, Dkt. Donald Kaberuka kwa ihsani
kubwa aliyoifanyia nchi yetu.
Kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huu ni jambo lenye manufaa mengi
kwetu. Kwanza husaidia kuitangaza nchi yetu Barani Afrika na
kwingineko duniani. Pili, ni fursa nzuri ya kuzungumza na viongozi wa
Benki kuhusu mipango na miradi yetu ya maendeleo tunayohitaji msaada
kutoka Benki hiyo.
Na, tatu, ni fursa nzuri ya watu wetu kufanya biashara. Mkutano huu
umeshirikisha watu 2,500 ambao wametoka nje ya Tanzania na wanajitegemea
kwa kila kitu. Wenye hoteli, migahawa, vyombo vya usafiri, huduma ya
simu, internet na nyinginezo watakuwa wamefanya biashara nzuri katika
wiki nzima kabla ya tarehe 28 Mei mkutano ulipoanza hadi 2 Juni, mkutano
utakapofungwa. Ni kutokana na manufaa kama haya, ndio maana huwa
tunahangaika kuvutia mikutano mikubwa kuja kufanyikia hapa nchini.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi na shukrani nyingi kwa ndugu
zetu wa Arusha kwa kuwapokea vizuri na kuwakarimu vyema wageni wetu hao.
Nawaomba waendelee na moyo huo mpaka watakapoondoka wote. Naomba
kuwepo kwa mkutano huu kuwakumbushe umuhimu wa mji wenu kuwa tulivu.
Miaka miwili iliyopita isingekuwa rahisi kwa watu au shirika kubwa la
kimataifa kama Benki hii kuamua kufanya mkutano wake Arusha. Isitoshe
hata sisi wenyewe tusingeshawishika kuomba au kukubali maombi ya namna
hiyo. Lakini sasa imewezekana. Naomba kila mmoja wetu aweke azimio
moyoni mwake la kuhakikisha kuwa hali ile haijirudii tena. Nyota ya
Geneva ya Afrika lazima iendelee kuangaza. Yaliyopita si ndwele tugange
yajayo.
Watanzania Wenzangu;
Niruhusuni tena niwashukuru wenzetu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa
mchango mkubwa waliotoa na wanaoendelea kutoa kuchangia maendeleo ya
nchi yetu. Kwa miaka mingi Benki hii imekuwa inatupatia mikopo na
misaada muhimu kwa maendeleo ya sekta mbalimbali nchini pamoja na zile
za elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara, reli, umeme n.k.
Kwa msaada wa Benki hii tunajenga barabara ya Namanga – Arusha,
Minjingu – Singida, Namtumbo – Tunduru, Iringa – Dodoma, Mayamaya –
Babati, na Tunduru – Mangaka – Mtambaswala. Miaka ya nyuma pia
walituwezesha kujenga barabara ya Mutukula – Muhutwe. Aidha, hivi sasa
wanagharamia upembuzi yakinifu na usanifu wa reli mpya tunayotaka
kuijenga kutoka Dar es Salaam hadi Rwanda na Burundi.
Matukio ya Uvunjifu wa Amani Zanzibar
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ninalotaka kuzungumza nanyi leo ni matukio ya wiki
iliyopita huko kwenye Jiji la Zanzibar katika mkoa wa Mjini Magharibi,
Unguja. Kama tujuavyo sote kulitokea ghasia zilizochochewa na viongozi
wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu maarufu kwa jina la
Uamsho. Taasisi hii imeanzishwa kwa madhumuni ya kidini, lakini hivi
sasa viongozi wake wameamua kuyaacha madhumuni hayo na kubeba ajenda za
siasa.
Siku za nyuma, ndugu zetu hawa walikuwa wakitumia muda mwingi
kuilaumu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baada ya kuundwa kwa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa lawama hizo sasa hazisikiki. Lakini, mara
tulipoanzisha mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, mihadhara yao imeelekezwa kupinga Muungano na kuwakashifu
viongozi waasisi wa Muungano na hata waliopo sasa. Isitoshe wamekuwa
wakipandikiza chuki dhidi ya ndugu zao wa kutoka Tanzania Bara na wale
wafuasi wa dini ya Kikristo.
Baya zaidi, katika uchochezi huo majengo na mali za Makanisa mawili
zilichomwa moto, maduka ya watu kuvunjwa na mali zao kuibiwa. Kwa kweli
vitendo hivi ni uhalifu ambao haukubaliki na wala hauvumiliki.
Naungana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kauli yake aliyoitoa jana katika
mkutano wake na waandishi wa habari ya kukemea vikali na kulaani uhalifu
huo.
Ndugu Wananchi;
Ni jambo la kusikitisha na kushangaza kwamba, wenzetu hawa wamefanya
uhalifu huo kwa hoja ya kupinga Muungano. Haiwezekani mtu anayepinga
Muungano, akaitetea hoja yake kwa kuchoma moto makanisa au kuvunja
maduka ya watu na kupora mali zao. Ukristo haukuingizwa Zanzibar na
Muungano, bali ulikuwepo karne kadhaa kabla ya Muungano na wala
haukutokea Tanzania Bara. Na kama alivyoeleza Mheshimiwa Rais Ali
Mohamed Shein jana, ukweli ni kwamba, dini ya Kikristo kama ilivyo ya
Kiislamu imeenezwa Bara kutokea Zanzibar. Kanisa kuu la Anglikan
Zanzibar lilijengwa kuanzia mwaka 1873 na lile la Katoliki kuanzia 1893
ni miongoni mwa Makanisa makongwe kuliko mengi kama siyo yote kwa upande
wa Zanzibar na Bara.
Katika hotuba yake ya jana, Mheshimiwa Rais, Dkt. Ali Mohamed
Shein,pamoja na kueleza kwa ufasaha ukweli huu, pia alisisitiza suala
la haki na uhuru wa Kikatiba wa mtu kuchagua au kubadilisha dini au
imani yake. Katika kutumia uhuru huo, mtu hastahili kuingiliwa au
kulazimishwa na mtu yo yote. Hayo pia ndiyo matakwa ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Kwa kweli yanayofanywa na ndugu zetu wa
Uamsho ya kuchoma moto makanisa siyo sawa hata kidogo. Na,
wanapoyafanya kwa kisingizio cha Muungano ni jambo lisiloeleweka kabisa
na wala halina mantiki. Labda wenzetu wana lao jambo.
Ndugu Wananchi;
Jambo lingine la kushangaza zaidi ni kule kutokea vurugu na ghasia hizi
dhidi ya Muungano wakati ambapo Serikali imetoa fursa sasa kwa watu
kutoa maoni yao kwenye mjadala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kama
tujuavyo sote, Tume ya Katiba imekwishaundwa na inajiandaa kupita kote
nchini kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba mpya waitakayo. Kama
mtu ana maoni yake kuhusu Muungano, hiyo ndiyo fursa ya kufanya hivyo.
Utaratibu mzuri umewekwa kwa ajili yetu sote, vurugu za nini?
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Mimi sioni sababu ya msingi ya kusababisha kuvurugika kwa amani kwa
jambo ambalo limewekewa utaratibu muafaka wa kulishughulikia. Nawaomba
tutumie utaratibu mzuri uliowekwa badala ya kufanya mambo yanayoleta
mifarakano katika jamii na yanayosababisha uvunjifu wa amani na
yanaharibu sifa na sura ya Wazanzibari na Watanzania isivyostahili.
Ndugu zangu,
Haipendezi wala haifurahishi kwa Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya
raia wake. Lakini, kama hapana budi, Serikali lazima ifanye na
haitasita kufanya hivyo. Narudia kuwasihi viongozi na wafuasi wa
Jumuiya ya Uamsho kurejea kwenye madhumuni ya msingi ya jumuiya yao.
Wajiepushe na ajenda za kisiasa na kupandikiza chuki zitakazosababisha
mifarakano baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano na baina ya
Wakristo na Waislamu. Watanzania ni ndugu na wamekuwa wanaishi pamoja
kwa upendo na furaha licha ya tofauti zao za rangi, makabila, dini na
maeneo watokako. Kimeharibika kipi hata leo yatokee haya? Aidha nawaomba
wenye maoni kuhusu Muungano wetu, muundo wake na uendeshaji wake
watumie fursa ya mjadala wa Katiba kutoa maoni yao. Huhitaji kufanya
ghasia kutoa maoni yako!
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia fursa hii pia kuwapa pole wale wote walioathirika na
vurugu zilizotokea. Nawaomba wawe wastahamilivu, hiyo ndiyo mitihani ya
maisha. Serikali zetu mbili zitafanya kila lililo kwenye mamlaka yake
kuwahakikishia wananchi wote usalama wa maisha yao na wa mali zao.
Nawapongeza vijana wetu wa Jeshi la Polisi kwa juhudi kubwa
waliyoifanya ya kudhibiti hali ambayo mwelekeo wake haukuwa mwema.
Nawaomba waendelee kuwa macho ili watu wasioitakia mema nchi yetu na
watu wake wasipate nafasi ya kutuvurugia amani na utulivu wetu. Naamini
tukidumisha utamaduni wetu wa kuheshimiana, kuvumiliana na kuzungumza
pale tunapotofautiana hakuna litakaloharibika. Haya shime tufanye hayo.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment