Friday, June 22, 2012

Walemavu wataka uwakilishi Tume ya Katiba mpya

JAMII ya Walemavu wasiosikia (viziwi) wameiomba Serikali kuweka wawakilishi wao katika Tume ya mchakato wa Katiba mpya ili waweze kuingiza maoni yao kwa kina mara watakapoanza kukusanya maoni juu ya upatikanaji wa Katiba mpya itakayo kuwa na tija kwao pamoja na walemavu wengine.

Wito huo ulitolewa na mmoja wa walemavu hao John Ogonya alipokuwa akichangia mjadala katika mdahalo ulioandaliwa na asasi isiyo ya kiserikali ya Mra Development Forum kuhusu utawala bora na uwajibikaji katika mchakato wa kupata katiba mpya uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Anglican mjini hapa.
Alisema Walemavu viziwi wamekuwa wamekuwa wakitengwa katika masuala mbalimbali ya kijamii na kupelekea kukosa ufahamu wa mambo kutokana na ulemavu wa kutokusikia waliokuwa nao.

John alidai kuwa katiba mpya inapaswa kuwa mkombozi wao kwa kuingizwa vipengere vitakavyoweza kuwasaidia kupata wataalamu wa lugha za alama katika huduma mbalimbali za jamii ikiwa ni pamoja na katika hudumaa afya,mahakama na katika ofisi mbalimbali za umma na vyombo vya habari.

Ameeleza ushilikishwaji kwa walemavu wasio sikia umekuwa mdogo na hata wanapoelekea katika mchakato wa kupata katiba mpya hata ile iliyopo mpaka sasa hawaifahamu na hivyo kukosa cha kutolea maoni bali wameomba kuwepo na uwakilishi katika Tume ya Katiba ili aweze kuingiza maoni yao.

Hata hivyo Walemavu walioshiriki katika mdahalo huo wameishukuru asasi ya Mara Development Forum kwa kuandaa mdahalo huo na kuwawekea wataalamu wa lugha za alama na kupelekea kuelewa kwa kina kile kilichokuwa kikizungumzwa na kuchangiwa kuhusu utawala bora na uwajibikaji katika mchakato wa kupata katiba mpya.

Akichangia katika mdahalo huo Mratibu wa Mara Development Forum George Chibasa alisema lengo la kuandaa Mdahalo huo ambao umekuwa ukifanyika kila Wilaya katika Mkoa wa Mara ni kuwajengea uwezo Wananchi ili kuwa na umakini mkubwa wa kutoa maoni yao katika mchakato wa kupata katiba mpya mara Tume ya kukusanya maoni itakapoanza kukusanya maoni.

Mratibu huyo ameishukuru Taasisi isiyo ya kiserikali ya The Foundation For Civil Society ya Dar es salaam kwa kuendelea kuwapa ufadhiri ambao unawasaidia kuwafikia Wananchi na kutoa elimu mbalimbali juu ya umuhimu wa kutoa maoni yao katika kuelekea upatikanaji wa Katiba mpya.

Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete alitangaza majina ya wajumbe wa Tume ya kukusanya maoni juu ya upatikanaji wa Katiba mpya itakayokuwa chini ya Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Sinde Warioba ambayo bado haijaanza kazi ya kukusanya maoni

No comments: