TUNAPATA shida kuamini kwamba wawakilishi wetu bungeni wanaweza
kulidhalilisha Bunge kwa kuendesha malumbano yasiyo na tija na
kuporomosheana matusi badala ya kutumia muda huo kujikita katika
kujadili Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa bungeni humo wiki iliyopita.
Ni vigumu pia kuamini kwamba mporomoko wa maadili katika nchi yetu
umesambaa kila sehemu kiasi cha kujipenyeza pia katika chombo nyeti kama
Bunge.
Juzi na jana gumzo kubwa miongoni mwa wananchi na
katika mitandao ya kijamii lilihusu aibu iliyotokana na vioja vya
wabunge wengi walipokuwa wakichangia mjadala huo kuhusu Bajeti ya
Serikali ya 2012/13. Wakati wananchi wakitegemea kusikiliza hoja nzito
za wabunge na uchambuzi wa kina kuhusu vifungu mbalimbali vya bajeti
hiyo na namna ya kuondokana na na matatizo lukuki ya kiuchumi, walipigwa
butwaa kuona mijadala hiyo ikitawaliwa na vijembe, matusi na vitisho
vya kila aina, huku ikionekana dhahiri kwamba wabunge wengi walikuwa
wanapata shida kuweka kando tofauti zao za kiitikadi na kisiasa.
Lakini
tatizo linalojitokeza hapa ni utashi wa kisiasa kwa upande wa Spika,
Naibu Spika na wenyeviti wa Bunge ambao wanaendesha vikao vya Bunge.
Zimejitokeza kasoro za hapa na pale wakati Spika, Naibu Spika na
wenyeviti hao wanapoendesha vikao hivyo, kasoro ambazo zimeacha maswali
mengi siyo kuhusu uwezo wao wa kuendesha vikao hivyo, bali utashi wa
kisiasa wa kuhakikisha wanatenda haki kwa kila mbunge bila kujali
itikadi yake au chama cha siasa anachotoka. Tofauti na wanavyofanya kwa
wabunge wa upinzani, mara nyingi wameonyesha udhaifu wa kuhofia
kuwawajibisha wabunge wa chama tawala wanapovunja Kanuni za Bunge.
Hiki
ndicho chanzo cha kasheshe tunayoishuhudia bungeni hivi sasa. Ndiyo
maana badala ya wabunge kuijadili bajeti hiyo kwa lengo la kuiboresha
wamejipanga katika kambi mbili, moja ikiwa ya wabunge wa chama tawala
ambao wameunga mkono bajeti hiyo ya Serikali kwa asilimia mia moja na
nyingine ikiwa ya vyama vya upinzani ambayo imeikataa bajeti hiyo pia
kwa asilimia mia moja. Kwa mtindo uleule wa jino kwa jino, wabunge wa
chama tawala wameikataa katakata Bajeti mbadala iliyowasilishwa na Kambi
ya Upinzani Bungeni, huku kambi hiyo ya upinzani ikiiunga mkono bajeti
hiyo kwa asilimia moja.
Hivyo ndivyo vioja vya Bunge hili
linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma kujadili Bajeti ya Serikali ya
mwaka ujao wa fedha. Tusidanganyane, hakuna jambo la maana
linalofanyika kule Dodoma hivi sasa. Kama tumewatuma wabunge waijadili
Bajeti na kwa kauli moja kurekebisha pale panapohitaji kurekebishwa ili
hatimaye ipitishwe bajeti endelevu yenye kutilia maanani maendeleo ya
nchi na maslahi ya wananchi wote, wabunge hao wanakuwa wasaliti wakubwa
wanapofanya kinyume na matarajio ya wananchi ambao ndiyo hasa waliowapa
ridhaa ya kuwawakilisha bungeni.
Kama moja ya habari
tuliyochapisha katika toleo la gazeti hili leo inavyosema, wananchi
waliohojiwa jana walisema pasipo kutafuna maneno kwamba bajeti zote
mbili, yaani ya Serikali ya chama tawala na ya Kambi ya Upinzani Bungeni
zinafaa kutumika kwani zote zina vipengele vingi vinavyofaa kuingizwa
katika Bajeti ya pamoja. Kwa maneno mengine, wananchi wanasema
inahitajika Bajeti mwafaka yenye kutilia maanani michango ya wabunge wa
pande zote mbili.
Pamoja na wabunge wengi kufanya vituko
vilivyowafadhaisha wananchi, tunayo matumaini kwamba hali hiyo inaweza
kurekebishwa iwapo uongozi wa Bunge na wabunge watatimiza wajibu wao na
kuweka mbele maslahi ya taifa. Bado upo muda wa kutosha kufanya hivyo
kwa kujadili mambo ya msingi, ikiwa ni pamoja na kutafuta suluhisho la
kukua kwa deni la taifa, mfumuko wa bei, kupambana na umaskini,
kuboresha kilimo, ajira kwa vijana na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo
wa Miaka Mitano.
No comments:
Post a Comment