ZITTO AMTAKA PINDA ATAJE WAHUSIKA, WANANCHI WATAKA FEDHA ZIREJESHWE, MABILIONI ZAIDI YAIBWA MTANDAONIKUBAINIKA
kwa Sh303.7 bilioni zilizofichwa katika akaunti za vigogo wa Serikali
na wanasiasa nchini Uswisi, kumetikisa nchi huku shinikizo likitolewa
kwa vyombo vya dola kuchunguza haraka na kuchukua hatua za kisheria,
ikiwamo kurejesha fedha hizo.
Jana kutwa nzima, gazeti hili
lilipokea simu kadhaa kutoka kwa wasomaji wake wakiwamo wabunge na
mawaziri, huku baadhi wakichangia maoni kwenye tovuti na mtandao
mbalimbali ya kijamii, wakitaka kujua majina ya wamiliki wa akaunti
hizo.
Bungeni mjini Dodoma, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe aliitaka Serikali kuchunguza tuhuma hizo kisha kuwachukulia hatua
watu sita wanaotajwa kwamba wanamiliki akaunti zenye mabilioni hayo ya
shilingi chini Uswisi.
Fedha hizo zimebainishwa na ripoti ya
Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB), iliyotolewa hivi karibuni, ikitaja nchi
mbalimbali ikiwamo Tanzania, na kiwango cha fedha zilizohifadhiwa huko.
Tayari
Kitengo cha Polisi wa Kimataifa (Interpol) nchini kimeeleza kuwapo kwa
fedha hizo katika benki mbalimbali nchini Uswisi, zilizoingizwa na
kampuni za uchimbaji mafuta na madini.
Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) nayo imeweka bayana kuwa inafuatilia
suala hilo kwa mamlaka za Uswisi, ili kujua fedha hizo ziliko na nani
anazimiliki.
Mbali ya Tanzania, nchi nyingine ambazo zina fedha
nyingi katika benki za Uswisi ni Kenya (dola 857 milioni), Uganda (dola
159 milioni), Rwanda (dola 29.7 milioni) na Burundi dola 16.7 milioni.
Chanzo
cha habari hizo, kilieleza kuwa tangu akaunti hizo zifunguliwe,
wamiliki wake halali hawajawahi kuingiza hata shilingi moja.
Kauli ya ZittoZitto
ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, aliliambia Bunge jana
kuwa haiwezekani nchi ikaendelea ilhali watu wanakusanya fedha kutokana
na utafiti wa gesi na mafuta, ambao bado haujaanza kulinufaisha Taifa.
Akichangia
Bajeti ya Waziri Mkuu, Zitto alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (PCCB) ielekezwe ili ifanye uchunguzi utakaowezesha wamiliki wa
akaunti hizo kufahamika, ili wachukuliwe hatua mara moja bila kujali
nafasi wanazozishikilia ndani ya Serikali.
“Viongozi
wanaohamisha na kupeleka fedha za Watanzania nje ya nchi wanatakiwa
wachukuliwe hatua mara moja. Hili litatusadia katika siku zijazo, kwani
kama wapo wengine wanaodhani wanaweza kuficha fedha zao nje basi wajue
kwamba popote watakapozipeleka tutazifuata na kuzirejesha,” alisema
Zitto na kuongeza;
“Namuomba Waziri Mkuu aagize uchunguzi ufanyike, fedha hizi zirejeshwe na wahusika wachukuliwe hatua,” alisema Zitto.
Zitto
alitoa kauli hiyo akiyanukuu magazeti ya Mwananchi, The Citizen na The
East African ambayo kwa nyakati tofauti yameandika kuhusu kuwapo kwa
kiasi kikubwa cha fedha zinazotokana na rushwa, ambazo zimehifadhiwa
kwenye akaunti kadhaa nchini Uswisi.
Alisema kuachia suala hilo
kuendelea ni hatari, kwani uchumi wa nchi utahujumiwa hata kabla ya
miradi husika haijaanza kutekelezwa.
“Haiwezekani sisi tupo
tunahangaika kutafuta gesi na mafuta huko baharini Lindi na Mtwara,
halafu watu wengine tayari wameishawekewa hela kwenye akaunti, kwa
hakika lazima uchunguzi ufanyike na watu hawa wajue kwamba Serikali ina
uwezo wa kuwafahamu na kurejesha hizo fedha hizo nchini,” alisema Zitto.
Alitoa
mfano wa Serikali ya India ambayo iliwahi kupata taarifa za baadhi ya
watumishi wake kuficha fedha nchini Uswisi na kuchukua hatua za
kiuchunguzi zilizowezesha wahusika kutajwa hadharani, kisha fedha
zilizoibwa serikalini kurejeshwa.
Katika hatua nyingine, Zitto
alitaka mvutano baina ya Tanzania Bara na Visiwani kuhusu masuala ya
gesi umalizwe ili kuwezesha utafiti kuendelea kufanywa katika maeneo ya
bahari ya Hindi.
Alisema utafiti katika baadhi ya maeneo hasa
eneo la Bahari karibu na kisiwa cha Pemba umesimama kutokana na mvutano
wa iwapo suala la mafuta ni la Muungano au la.
“Kama visiwani
watavumbua gesi ni sawa, wavumbue kivyao, na sisi Tanzania bara
tumeshavumbua matrilioni ya gesi, basi tuendelee kivyetu lakini
tusisimamishe tafiti kutokana na mvutano usio na maslahi kwa nchi,”
alisema.
Lowassa atoa kauliMwenyekiti wa Kamati ya Mambo
ya Nje ya Bunge Edward Lowassa, alisema jana kuwa kamati yake imesikia
suala hilo kwenye vyombo vya habari na inajipanga kuzifanyia kazi
taarifa hizo mara moja.
"Tumesikia kupitia vyombo vya habari na
kama kamati tutahakikisha tunazifanyia kazi," alisema Lowassa alipokuwa
akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano aliouitisha
kuzungumzia safari ya kamati yake nje ya nchi.
Chadema yatoa tamkoKwa
upande wake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeonya kuwa
tatizo la ufisadi halitaisha nchini hadi pale Serikali itakapochukua
hatua za dhati za kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu wote ambao
wamehusika na ufisadi wa raslimali za nchi.
Chama hicho kimemtaka
Rais Jakaya Kikwete kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuagiza kukamatwa
kwa watuhumiwa wote wa ufisadi wa ununuzi wa rada na wale ambao
wanatuhumiwa kuhifadhi Sh 303.7 bilioni nchini Uswisi.
“Chadema
kinatambua kwamba kuachwa kwa mafisadi bila kuchukuliwa hatua kamili za
kisheria na mali zao kufilisiwa, kunafanya taifa kuendelea na ufisadi
ikiwemo ule wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Richmond na sasa tuhuma
mpya za ufisadi wa shilingi bilioni 303 kwenye akaunti Uswisi,” ilisema
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, kupitia taarifa
kwa
vyombo vya habari jana.
Wizi mwingie kupitia mtandaoNaibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Pereira Ame Silima alilieleza Bunge
jana kuwa hadi sasa kiasi kilichoripotiwa Polisi kuhusina na wizi kwa
njia ya mtandao nchini ni Sh2.2 bilioni.
Fedha hizo ni zimegawanywa katika makundi matatu, Sh1.3 bilioni, Euro 8,897 (Sh17,660, 545) na dola 551,777 (Sh882,843,200).
Kauli
hiyo ilitolewa wakati Waziri Silima akijibu swali la Hussein Mussa Mzee
(Jang’ombe-CCM) aliyetaka kujua ni kiasi gani cha fedha kimeripotiwa
Polisi kutokana na wizi kwa njia ya mtandao.
Mzee alihoji Serikali
imejipanga vipi kudhibiti wizi wa mtandao, idadi ya waharifu wa wizi huo
ambao wamekamatwa huku akitaka itungwe sheria maalumu kushughulikia
wizi huo.
Silima alisema kuwa Serikali imetunga sheria
inayoshughulikia uhalifu unaofanywa kwa njia ya mtandao, Electronic and
Posta Communication Act, 2010 na sheria ya kudhibiti fedha haramu (The
Anti – Money Laundering Act – 2006.
Aliongeza kuwa Serikali
kupitia vyombo mbalimbali vya dola kama vile Polisi, taasisi za fedha,
vyombo vya habari, TRA na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imejiwekea
mikakati ya kuelimisha wananchi kuhusu aina ya uharifu wa kimtandao na
jinsi ya kupambana nao.
Waziri alibainisha kuwa jeshi la Polisi
limeanzisha Kitengo cha Makosa ya Kimtandao (Cyber Crime Unit) ambacho
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kinafanya kazi kubwa ya kupambana
na majanga hayo.
Kilio cha wabunge
Wakati huohuo wabunge
wameendelea kumbana Pinda huku baadhi yao wakikataa kuunga mkono hotuba
yake hadi pale atakapojibu hoja walizotoa.
Mbunge wa Nkasi
Kaskazini (CCM), Ally Keissy akichangia hotuba ya hiyo jana, alisema
vita dhidi ya ufisadi haiwezi kufanikiwa kwani vyombo vya husika
wakiwamo Takukuru wanashindwa kuchukua hatua kwa makosa ambayo yako
wazi.
Keissy alisema mafisadi na walarushwa nchini wanalindwa na
Takukuru, kwani licha ya kuwapo kwa ushahidi na viashiria vya wazi,
chombo hicho hakichukui hatua zozote.
Alisema, kama wapo watu
wanaodiriki kuuza dawa ambazo zilipaswa kupelekwa katika hospitali na
matokeo yake wagonjwa wanakufa, mtu huyo hana budi kunyongwa.
“Sheria
za nchi hii zinawalinda wezi, ndiyo maana ufisadi hauwezi kuisha, mtu
ana majengo makubwa leo, wakati ni jana tu amepata ubunge, amepata wapi
utajiri huo wa haraka, aulizwe na akishindwa kutoa maelezo achukuliwe
hatua,” alisema Keissy na kuongeza:
“Sasa la ajabu ni kwamba eti
wanakwambia kwamba kama unamjua mla rushwa basi uwapelekee taarifa,
kwani wao hawawaoni watu wanaotajirika haraka haraka?” alihoji.
Keissy
ambaye aliipinga Bajeti ya Waziri Mkuu hadi pale atakapopewa majibu ya
kuridhisha, alisema sheria za nchi hii ni dhaifu, ndiyo maana mafisadi
wanaoiba mamilioni wanaendelea kudunda barabarani wakati mwizi anayeiba
simu hupigwa na kuchomwa moto hadi kufa.
Mbunge huyo alisisitiza
ujumbe wake, akisema kuwa, “hata ikitokea mafisadi hao wakafariki basi
pingu ziwekwe juu ya makaburini yao.”
Naye Mbunge wa Viti Maalum
(CCM), Riziki Lulida alisema kuna njama zinazofanyika za kudhoofisha
maendeleo mkoani Lindi kwa kuwapeleka viongozi wala rushwa katika mkoa
huo.
Alisema, uduni wa mkoa huo unasababisha wapinzani kuufanya
kuwa kichaka cha wapinzani, kuwadhalilisha na kuwasema kwamba wao ni
maskini.
“Viongozi wengi wa halmashauri wanaofanya ubadhirifu wa
fedha kutoka mikoa mingine hutupwa Lindi,” alisema Lulida kabla ya
kuanza kuwataja kwa majina wafanyakazi hao wa halmashauri:
“Joachim
Materu ameiba 577 milioni, akapelekwa Lindi, Eunice Maro ameiba 262
milioni na akapelekwa Lindi, baada ya kufanya wizi huo, Maro aliziweka
katika akaunti inayoshukiwa kuwa ni ya rafiki yake, yenye akaunti namba
206660017 NMB ambaye alihamishiwa Ofisi ya Kilimo Lindi,” alisema.
Aliwataja
wengine kuwa ni Macha anayetuhumiwa kuiba Sh6 bilioni ambaye
amehamishiwa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na kwamba kuhamishwa
kwao ni kusambaza ufisadi katika maeneo mengine.
Lulida
aliongeza kuwa, kama Waziri Mkuu anataka aiunge mkono bajeti yake, basi
aje na majibu sahihi kuhusu maendeleo mkoani Lindi pamoja na kurudisha
programu ya kilimo ya Kanda ya Kusini, (SAGCOT)
Habari hii imeandaliwa na Neville Meena, Florence Majani na Habel Chidawali, Dodoma na Leone Bahati Dar