HALI ya uchumi nchini hivi sasa si nzuri, na inaelekea imeanza kumtikisa Rais Jakaya Kikwete ambaye sasa ameanza kuchukua hatua za makusudi kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kufuatilia kwa karibu utendaji wa sekta muhimu kiuchumi, Raia Mwema imebaini.
Kuanzia wiki iliyopita, Rais Kikwete amekuwa na vikao vyenye mwelekeo wa kuwabana watendaji na wafanyabiashara wa sekta zinazogusa uchumi, ikiwa ni pamoja na sekta ya miundombinu na fedha.
Katika kikao na sekta ya miundombinu, Rais Kikwete aliwahusisha pia watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambao walibanwa kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unaongezeka na unakwenda sambamba na ushirikiano na wadau wengine wakiwamo wafanyabiashara na kampuni binafsi.
Katika kikao hicho alitoa maelekezo kwa wadau wa sekta ya reli na bandari ambao walitakiwa kuboresha huduma zao ili kuwezesha waagizaji bidhaa nchini kutokimbilia kutumia bandari ya nchi jirani.
Mara baada ya kukutana na wadau wa sekta ya miundombinu, Rais Kikwete, wiki hii, alikutana na watendaji wa Wizara ya Fedha na Uchumi, na asasi zake, ikiwamo BoT.
Katika kikao hicho, Gavana Beno Ndullu alinukuriwa akisema kwamba mfumuko wa bei ulipanda ghafla mwaka jana, kwa sababu ya kupanda mno kwa bei za mafuta na vyakula (nafaka) katika soko la dunia, na kwamba utaanza kushuka katika siku za karibuni, na hivyo kuteremsha gharama za maisha.
Mfumuko wa bei nchini ulikuwa asilimia 13.5 kwa mwezi uliopita wa Desemba kutoka asilimia 8.6, kabla ya kuanza kupanda ghafla na kwa kiasi kikubwa kwa bei ya mafuta duniani na ile ya chakula.
Taarifa ya Ikulu ilieleza kwamba, BOT inabashiri kuwa lengo la ukuaji wa uchumi kwa asilimia 7.5 bado linaweza kufikiwa.
Tofauti na mikutano aliyoifanya mwanzoni mwa utawala wake ambako Rais alitembelea kila wizara na kutoa maelekezo yake, mikutano ya sasa inafanyika Ikulu kati ya Rais na viongozi wa juu wa wizara mbalimbali na asasi za wizara hizo.
Gavana Ndullu pia alieleza kuwa hazina ya fedha za kigeni katika BOT, hadi kufikia Desemba mwaka jana, ilikuwa ni dola za Marekani bilioni 2,894.42 ambazo zinatosha kuweza kuagiza bidhaa kutoka nje kwa kipindi cha miezi minne.
Kulikuwa na taarifa zisizo rasmi kwamba hali ya uchumi imekuwa mbaya; kiasi cha kuilazimu Serikali kuharakisha kuchapisha noti mpya, lakini Gavana Ndullu alisema kuwa hatua hiyo itakayochukuliwa mara baada ya kumpata mzabuni, haina uhusiano na hali hiyo.
Kwa sasa Serikali inamtafuta mzabuni wa kuchapisha fedha, baada ya wa awali kutoka nchini Ujerumani, kukamilisha mkataba wake, ingawa pia naye anakaribishwa kupigania zabuni hiyo.
Akizungumza na Raia Mwema jijini Dar es Salaaam, ingawa Profesa Ndullu amekiri kuwapo kwa mfumuko wa bei nchini, lakini akasisitiza kuwa hali si mbaya sana na kwamba kuchapwa kwa noti mpya ni utaratibu wa kawaida
“Kuna mambo mawili katika kuchapa noti mpya. Kwanza ni kuondoa noti zilizochakaa, lakini pia ni kukidhi mahitaji ya kibiashara na hasa hali ya biashara inapokua kwa kasi,”
“Nasi tunafikiria kubadili noti kwa malengo mbalimbali ambayo ni pamoja na kuziboresha lakini hii ni hatua ya baadaye, baada ya kumpata mzabuni.
“Tuliwahi kuwa na senti tano, senti 10 lakini tukaziacha…ni kweli kuna suala la mfumuko wa bei lakini hali si ya kutisha kama ilivyo Zimbabwe ,” alisema.
Alipoulizwa kama ni mambo gani yatazingatiwa katika noti mpya, Profesa Ndullu alisema kikao rasmi bado hakijafanyika cha uamuzi lakini mambo kadhaa yatazingatiwa, ikiwa ni pamoja na ukubwa wa noti za sasa, hususan za Sh 10,000.
Na alipoulizwa kuhusu noti zitakazoondolewa katika mzunguko, Profesa Ndullu hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa kuwa wakati wake haujafika.
Katika miaka ya nyuma, uchapishaji wa noti mpya umekuwa ukihusisha mchakato wa kufuta katika matumizi baadhi ya noti.
Noti ambazo zimewahi kufutwa katika mchakato wa kutumika ni pamoja na za shilingi 10 na shilingi 200. Noti ya shilingi 200 ilianzishwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye ni mtaalamu bingwa wa uchumi alisema kwamba kama Serikali inakusudia kuchapa noti mpya kwa ajili ya kuondoa zilizochakaa katika mzunguko, ni sahihi.
Hata hivyo, alionya kuwa kama Serikali inakusudia kuchapa noti mpya kwa lengo la kufidia matumizi yake hayo ni makosa makubwa yenye athari ya moja kwa moja kwa raia wa kawaida nchini. Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, athari hizo ni pamoja na ongezeko la mfumuko wa bei.
“Kwanza ni utaratibu wa kawaida kwa Benki Kuu kuchapisha fedha na hasa kama inakusudia kuondoa fedha chakavu katika mzunguko,” alisema na kuongeza kuwa kama lengo la sasa la hatua ya Serikali ni kuingiza fedha mpya na kuondoa za sasa basi athari pia zinaweza kuwa kubwa zaidi ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kupoteza imani na sarafu ya Tanzania.
Lakini pia alisema hatua hiyo inaweza kuwa na mantiki kama Serikali inakusudia kuanzisha noti mpya ya kiwango cha juu baada ya kubaini kuwa noti ya sasa ambayo ni Shilingi 10,000 haikidhi mahitaji kwa kulinganisha na sarafu za kimataifa na hususan dola ya Marekani.
Kwa upande wake, mtaalamu na mtafiti wa masuala ya uchumi kutoka Taasisi ya Utafiti katika masuala ya Uchumi na Jamii (ESRF), Dk. Oswald Mashindano, aliiambia Raia Mwema kuwa uamuzi wa kuchapisha fedha mpya una athari mbaya kwa Taifa.
“Unapochapisha noti mpya maana yake ni kwamba kuna matatizo katika vyanzo vya mapato au mfumo wa uchumi umekubwa na mtikisiko.
“Huko nyuma nafikiri katika miaka ya sabini tuliwahi kuchapisha noti. Lakini unapochapisha noti maana yake unaongeza fedha nyingine nje ya mfumo wa kawaida wa uzalishaji.
“Unaongeza fedha hizo katika mzunguko wa fedha na hapo utakuwa hauna mizania sawa na unaweza kufungulia mfumuko wa bei zaidi,” anasema.
Anazungumzia kauli ya Gavana Ndullu akisema; “Kama ni kweli kuna ukuaji wa shughuli za biashara kiasi cha kuhitajika kuongezwa kwa fedha zaidi hiyo ni ishara kwamba ujasiriamali na wajasiriamali wameongezeka.
Katika hali kama hiyo, fursa bora zaidi si kuchapisha fedha mpya na kuziingiza katika mzunguko bali ni kukopa fedha katika taasisi za kimataifa na kuwakopesha wajasiriamali.
Alitoa mfano wa uamuzi uliofanywa hivi karibuni na Serikali ya Marekani wa kukopesha fedha makampuni ya nchi hiyo yaliyoathiriwa na kuyumba kwa uchumi wa taifa hilo kubwa duniani.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu ugumu wa kupata mkopo katika asasi hizo kutokana na asasi hizo nazo kuathiriwa na anguko la uchumi duniani, Dk. Mashindano alisema kama mkopo unashindikana ipo njia nyingine ya tahadhari.
Alibainisha tahadhari hiyo kuwa ni kuchapisha fedha mpya na wakati huo huo kuwa makini zaidi katika matumizi hususan katika sekta kiongozi katika kuimarisha uchumi.
Raia Mwema, januari 21,2009
1 comment:
Tatizo kubwa ni bei ya mafuta nayo ipo juu sana, wangepunguza kodi na kudhibiti wafanyibiashara wa mafuta wasipandishe bei holela hapo bidhaa zitashuka bei na kipato kitakuwepo kwa wananchi hivyo watalipa kodi na wataongeza pato la taifa
Mwenda
Post a Comment