Friday, January 9, 2009

Rais Kikwete aahidi kuzifanyia kazi sheria kandamizi


Hii ni sehemu tu ya hotuba ya Rais Jakaya Kikwete akihutubia mkutano wa uchaguzi wa UWT

Ndugu Mwenyekiti;
Pamoja na kuongeza uwakilishi wa wanawake kwenye vyombo vya maamuzi, yapo mambo ambayo yanahusu maendeleo ya wanawake ambayo inabidi yaendelee kufanywa sasa.
Sisi katika Serikali tumeweka vipaumbele katika mambo matano yahusuyo maendeleo ya mwanamke nchini:
La kwanza, ni lile nililolisemea hapo awali: la kuongeza uwakilishi wa wanawake kwenye vyombo vya maamuzi. Katika kufanikisha jambo hili muhimu, kuna mambo yanayohitaji mabadiliko ya sheria. Na kuna yale ambayo tunaweza kuyafanya kwa maamuzi yetu sisi tuliyo madarakani sasa. Mimi nimekuwa nafanya hivyo kwa nafasi zinazoangukia katika mamlaka yangu ya uteuzi. Ndio maana leo tunao wanawake wengi katika nafasi za Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Wakuu wa Wizara, Wakurugenzi Watendaji, Majaji, na kadhalika. Naahidi kuendelea kufanya hivyo kadri fursa zinapojitokeza. Nasema hivyo kwa sababu wale tuliowapa nafasi wanawawakilisha vizuri.
Kwa upande wa nafasi za kuchaguliwa, ni muhimu wanawake nao wakajitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi pindi fursa zinapopatikana. Kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za uongozi pia kutegemee ni kwa kiasi gani kinamama nao wanajitokeza kuomba nafasi hizo. Chama, na hasa UWT, mnalo jukumu kubwa la kuhamasisha wanawake kujitokeza.

Ndugu Mwenyekiti,
Sisi katika Chama cha Mapinduzi tuliwaahidi wanawake wa Tanzania, kupitia Ilani yetu ya Uchaguzi ya 2005, kwamba tutaanza kwa kuongeza uwakilishi wa wanawake Bungeni, ili angalau tufikie asilimia 50-50.
Mchakato wa kuelekea huko umeanza na unaenda vizuri. Si shughuli rahisi sana ndiyo maana imechukua muda. Hata hivyo, tumedhamiria kutimiza ahadi yetu.
Tulikwishaamua kuelekea huko na hakuna kitakachoturudisha nyuma katika kuanza mpango huo. Mawazo ya msingi yatakapokamilika yatawekwa hadharani kwa wadau wote kutoa maoni yao. UWT inao mchango na wajibu mkubwa katika kufanikisha azma hii. Uongozi wenu na mawazo yenu yatakuwa muhimu katika kusaidia kupatikana kwa utaratibu mzuri utakaopanua na kuimarisha demokrasia nchini kwa haraka.

Ndugu Mwenyekiti,
La pili katika kuhakikisha maendeleo na ustawi wa mwanamke wa Tanzania ni kuhakikisha mwanamke hanyimwi haki zake. Kuna msemo kwamba “haki za mwanamke ni haki za binadamu”. Nami nakubali. Kwa maana hiyo, sisi katika Serikali tumeendelea na mchakato wa kuzitazama upya Sheria zihusuzo ndoa, mirathi na watoto, sheria ambazo zinahusu haki na ustawi wa wanawake wa nchi yetu. Kwa kuwa Sheria hizi zinagusa kwa karibu maisha ya jamii nzima, tumeamua tutengeneze White Paper ili wananchi washiriki kwenye mjadala wa mabadiliko ya Sheria hizi. White Paper hii italetwa kwenye Baraza la Mawaziri wakati wowote kuanzia sasa. Na tutaweka utaratibu wa wananchi kujadili mapendekezo hayo. Dhamira yetu ni kuzirekebisha sheria hizo ili wanawake wasizidi kukandamizwa na kunyimwa haki zao za msingi. Ni matarajio yangu kuwa UWT itashiriki kwa ukamilifu kama mdau kiongozi katika mijadala itayohusu Sheria hizi. Sauti yenu lazima isikike na uongozi wenu lazima uonekane kwenye jambo hili muhimu.
Jambo la tatu tulilolipa msisitizo katika ukombozi wa mwanamke wa Tanzania ni elimu ya mtoto wa kike. Kama wengi mjuavyo, tunalo tatizo kubwa katika baadhi ya jamii zetu juu ya kutotiliwa maanani au hata kupuuzwa kabisa haki ya mtoto wa kike kupata elimu. Kwa maana hiyo, kwa miaka mingi sasa idadi ya wanafunzi wa kike kwenye mashule yetu, na hasa idadi ya wanafunzi wa kike wanaomaliza elimu katika ngazi zote, imekuwa ndogo kuliko ya wavulana.
Tumejitahidi sana kwa miaka ya hivi karibuni kubadilisha hali hii kwa upande wa elimu ya msingi na sekondari. Siku hizi idadi ya watoto wa kike wanaoingia darasa la kwanza na kidato cha kwanza, inalingana na wavulana. Lakini, bado kuna tatizo la watoto wa kike kutokumaliza shule kwa idadi inayolingana na wenzao wavulana. Jambo hili linarudisha nyuma maendeleo ya mtoto wa kike wa Kitanzania. Tunaendelea kukabiliana nalo, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua madhubuti za kupunguza tatizo la mimba za wanafunzi.
Ni muhimu kwa UWT nayo kuwa mstari mbele na inaonekana iko mstari wa mbele katika harakati za kukabiliana na tatizo la watoto wa kike kutokumaliza masomo kwa sababu za kuolewa au kupata mimba na mambo mengine yanayofanya watoto wa kike wasimalize masomo.
Jambo la nne ambalo tumelipa uzito mkubwa na tutaendelea kulipa umuhimu mkubwa ni uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake. Kama nilivyosema hapo awali, Watanzania ni maskini lakini wanawake ni maskini zaidi. Kwa maana hiyo, wanahitaji kuwekewa mazingira maalum na mahsusi kwa ajili ya kujikwamua katika hali duni za maisha. Serikali inatambua kuwa wanawake ni wajasiriamali wazuri, waaminifu na ni watu wenye bidii kubwa. Wanachohitaji ni umoja, mtaji na elimu ya ujasiriamali na biashara.

Chanzo cha habari,
mawasilianoikulu.blogspot.com