Tuesday, January 27, 2009

MUHTASARI WA SEMINA KUHUSU TATHMINI YA MIAKA 10 YA SHERIA YA MAKOSA YA KUJAMIIANA (SOSPA) YA MWAKA 1998

Tathmini ya miaka kumi (10) ya sheria ya makosa ya kujamiiana (SOSPA) 1998.

WATOA MADA:
Marie Shaba – (FemACT).
Ananilea Nkya – (TAMWA).
Scolastica Jullu – Kituo cha msaada wa sheria (WLAC).

MWEZESHAJI:- TGNP

MAHUDHURIO:-
Washiriki waliohudhuria GDSS hii walikuwa kama ifuatavyo:-
Wanawake 144
Wanaume 90
Jumla 234
KUHUSU WASHIRIKI:-
Washiriki wa semina hii walikuwa ni wanachama wa semina za jinsia na maendeleo (GDSS), vikundi shirikishi , wafanyakazi wa mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) na wananchi kwa jumla.

MJADALA KWA UFUPI:-
Baada ya salam,ufunguzi wa semina na kutakiana heri ya mwaka mpya kuliko fanywa na bi Marie Shaba, historia fupi ya msukumo wa kutaka kutungwa kwa sheria ya makosa ya kujamiiana (SOSPA) ilitolewa.
Mtoa mada bi Ananilea Nkya kutoka (TAMWA) alianza kwa kusema “Mfumo ama sera za nchi zilikuwa mbaya na kuwakandamiza watu wengi hasa katika nyanja za uchumi,siasa na uchangiaji huduma zilizopelekea watu wengi kukosa ajira na kupelekea kuibuka kwa matatizo mengi zaidi ya kijamii mwanzoni mwa miaka ya tisini (1990) .”

Aliyataja baadhi ya mambo yaliyopelekea msukumo wa kutaka sheria hii kutungwa kuwa ni:-

• Athari za utandawazi kuanza kuibuka.
• Madhara ya ukimwi kuanza kuonekana wazi zaidi.
• Kushamiri kwa vitendo vya kishirikina (Ramli).
• Kufichuka kwa vitendo vingi viovu katika jamii kama vile ubakaji,kunajisi n.k kupitia vyombo vya habari.
• Ukosefu wa haki hasa kwa wanawake na watoto.
• Mgawanyo mbaya wa rasilimali katika jamii.

Baada ya kubainisha hayo mtoa mada aliwataka washiriki wajiulize kama kitendo cha waziri kusema sheria hii imelenga kuwakandamiza wanaume zaidi…
Je mambo yaliopelekea kutungwa kwa sheria hii yamebadilika?

Aliendelea kwa kusema “tunaihitaji zaidi sheria hii kwa sasa zaidi kuliko wakati mwigine wowote, maana katika jamii yetu sasa kumezuka tabia mbaya zaidi za vitendo vya ubakaji katika ndoa na bado watu wameendelea kukosa ajira, hivyo kufikiria ,kupunguza ama kufuta sheria hii ni kuwaweka wanawake na watoto katika wakati mgumu zaidi”.

MJADALA KWA UREFU:-
Mafanikio na changamoto za sheria hii ndio yalijadiliwa katika hatua hii kuhusu sheria hii ya makosa ya kujamiina . Washiriki wakiongozwa na mtoa mada bi Scholastica Jullu kutoka kituo cha msaada wa sheria (WLAC).

Mafanikio ya sheria;
• Kutiwa hatiani kwa wahalifu wengi wa makosa ya kujamiiana toka kuanzishwa kwa sheria hii miaka kumi (10) iliyopita, ilielezwa karibu robo tatu (¾) ya wahalifu wanatumikia adhabu katika magerezani mbalimbali nchini.
• Sheria imetoa ulinzi kwa wanawake wengi zaidi na watoto nchini.
• Kupungua kwa vitendo vya ukeketaji. Ilielezwa kuwa mwaka 2006 vitendo hivyo viliripotiwa kupungua kwa asilimia ishirini (20).
• Kupungua kwa vitendo vya kidhalilishaji/bughudha dhidi ya wanawake.

Changamoto;
Kwa miaka kumi iliyopita ya utekelezaji wa sheria hii changamoto kadhaa zilibainishwa,miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na:-

• Kutokufahamika vizuri kwa sheria hii katika jamii.
• Kutokupelekwa/kuripotiwa kwa kesi nyingi za ubakaji katika vituo vya polisi kwa hofu ya aibu ya kutokuolewa na kwa wale wadogo mara nyingi maamuzi ya usuluhishi yanafanywa majumbani.
• Mara nyingi katika kesi za namna hii watoa ushahidi na wapelelezi huwa tofauti,kitu kinachopelekea kukosekana ushahidi madhubuti wa kuwatia hatiani wahalifu.
• Kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji ndani ya ndoa.
• Mkinzano wa kisheria kwenye ndoa, elimu na uchaguzi.Inatamkwa kuwa mtu mzia mwenye haki ya kushiriki uchaguzi lazime awe na miaka kunzia kumi na nane (18), lakini mtu huyo huyo anaruhusiwa kuingia katika ndoa akiwa na miaka kumi na tano (15) na kumnyima fursa ya kupata elimu.

Kifanyike nini;
• Elimu iendelee kutolewa kwa jamii ili kurahisisha uelewa na utekelezaji wa sheria hii.
• Kuwepo na utaratibu wa kufanya kazi kwa pamoja katika kufatilia mambo ili kupata ufanisi mapema.
• Kuondolewa kwa mfumo dume ambao tayari umeonekana kuwa ni tatizo.
• Tuwe na mbinu mpya za jando na unyago.
• Sheria ya makosa ya kujamiiana ifundishwe kuanzia ngazi za shule ya msingi kwa kuzingatia mtaala utakaokubaliwa.
• Kuongezwe kipengele cha ubakaji ndani ya ndoa katika sheria hii.
• Serikali ianzishe mahakama maalum,wanasheria na vifaa maalum kwa maswala ya ubakaji.

HITIMISHO:-
Wakati wa kufanya hitimisho la semina, mambo matano (5) yaliazimiwa:-

• Kabla ya muswada wa marekebisho ya sheria ya makosa ya kujamiiana (SOSPA) kupelekwa bungeni,rasimu ya mabadiliko ipitiwe kikamilifu na wadau wote au kuwe na mjadala wa kitaifa kuhusu mabadiliko hayo.
• Itolewe elimu ya kutosha kwa vyombo vya dola na jamii kwa ujumla kuhusu utekelezaji madhubuti wa sheria hii.
• Kutaka maboresho zaidi na kuzuia ufutwaji au kupunguzaji wa adhabu katika sheria hii.
• Kuwepo kwa shinikizo la kumtaka waziri mwenye dhamana ya sheria ajiuzulu.
• TGNP na wanaharakati wengine waendeleze vuguvugu la ukombozi wa mwanamke kimapinduzi kwa kuunganisha nguvu.

Mwisho ilikubaliwa kuwepo na muendelezo wa mjadala katika muendelezo wa semina za jinsia na maendeleo (GDSS) siku ya jumatano tarehe 28/1 kuhusu sheria hii ya makosa ya kujamiiana (SOSPA)-1998 ili kutoa fursa zaidi kwa washiriki kujadili kwa kina na kutoa maoni yao.

No comments: