MWAKA uliopita wa 2008 umekuwa ni mwaka wenye matukio mengi sana. Mbali ya matukio mengine, tumeshuhudia vita dhidi ya ufisadi ikipamba moto. Katika yote hayo,tusisahau umuhimu wa kuelekeza juhudi zetu katika kuujenga uchumi.
Hakika uchumi wetu bado ni duni. Wananchi wengi bado wanataabika kwa umasikini. Mwaka huu mpya wa 2009 uwe ni mwaka wa kuelekeza pia juhudi zetu kwenye kujenga na kuimarisha uchumi.
Itakumbukwa, kuwa kabla ya kuachia madaraka, rais mstaafu Benjamin Mkapa alipata kutamka; kuwa anaiacha nchi yenye uchumi ulio tayari kupaa. Ni miaka mitatu tangu Mkapa aondoke. Leo kuna baadhi wenye kuhoji uthabiti wa kauli ile ya Mkapa.
Kuna wanaodai, kuwa hali halisi katika utendaji wa awamu ya Mkapa nayo imechangia kutufikisha hapa tulipo leo, ugumu wa maisha uliochangiwa na ufisadi.
Ndege ya kiuchumi aliyoiacha Mkapa bado inaunguruma uwanjani, haionyeshi dalili za kuanza kupaa. Tusipoangalia, ndege hii itazimikia uwanjani kwa kukaukiwa mafuta kabla hata haijaanza kupaa. Na ieleweke, kuwa hata katika hali ya mvua ya manyunyu, rubani anaweza kuitayarisha ndege, akawasha injini, ndege ikawa tayari kuruka.
Lakini, ndege hiyo inaweza kubaki hapo uwanjani ikiunguruma bila kupaa. Hilo laweza kutokea kama mvua itaongezeka ghafla na barabara za udongo za uwanja huo zikajaa matope.
Kujenga uchumi wa kisasa ni sawa na kutengeneza mazingira mazuri ya ndege, si tu kuweza kupaa, bali kuvutia marubani wengine kutua na ndege zao kwa salama na amani. Katika nchi yeyote yenye dhamira ya kweli ya kwenda mbele kimaendeleo, usalama na amani ni vitu viwili muhimu kuwapo. Bila usalama na amani hakuna maendeleo. Na katika mazingira yenye kuruhusu kushamiri kwa rushwa, kubwa na ndogo, basi, haki na usawa katika nchi hiyo hukosekana. Na pasipo na haki na usawa, hakuna amani na usalama.
Unaweza kuwa na amani katika nchi lakini ukakosa usalama kwa maana ya kuwa, ingawa nchi haimo katika vita, lakini wananchi kwa kiwango kikubwa hawana hakika ya usalama wa maisha na mali zao. Hawana hakika ya maisha yao ya kila siku, chakula chao, afya yao, elimu yao na ya watoto wao. Nchi inaweza kuwa na amani lakini haina usalama kwa maana ya pili niliyoielezea. Na hilo la kukosekana kwa usalama huhatarisha kuvunjika kwa amani.
Kuwapo amani na usalama katika nchi hujengeka katika misingi ya haki na usawa, misingi ya kuaminiana. Misingi ya kuheshimu haki na uhuru wa raia kutoa mawazo yao. Ni lazima kuwapo misingi imara ya demokrasia. Wananchi ni vema wakawaamini viongozi wao, na viongozi pia ni vizuri wakawaamini wananchi wao. Na ili viongozi waaminike ni lazima wawe wakweli na wawazi. Wawe waadilifu.
Ni Mkapa pia aliyewahi kutamka; " Ni afadhali nichukiwe kwa kuwa mkweli, kuliko kupendwa kwa kuwa mwongo na mlaghai." Kisha akaongeza; kiongozi aliyejiridhisha kuwa jambo fulani ni la manufaa kwa wananchi wake hana sababu za kuogopa kuwa mkweli, na kuelezea kwa nguvu ya hoja, kwa nini sera, mikakati na mambo fulani ni ya lazima. Ni vema na haki, kuongoza walioelewa, kuliko kuongoza walioachwa gizani."
Wanadamu hatuna budi kufahamu, kuwa uaminifu ni biashara nzuri, ni biashara yenye tija. Tusipoaminiana na kibaya zaidi, tusipoaminiwa kama watu binafsi, tusipoaminiwa na wengine ndani na nje ya mipaka yetu, kwamba tusipoaminiwa na wanaotufadhili kiasi cha kutukatia misaada yao, basi, hilo ni jambo la hasara kwa mtu mmoja mmoja na kwa taifa.
Haya ni mambo ya msingi kabisa kuyatafakari tunapouanza mwaka mpya wa 2009. Ni ya muhimu kuyatafakari ili kuiwezesha ndege yetu ya kiuchumi iweze kupaa. Na zaidi ya yote, tunataka ndege nyingine zitue hapa kwetu.
Hivi ni nani atapenda kuja kuwekeza kwenye nchi ambayo mwenye haki mahakamani anageuka kuwa kichekesho pale mashtaka yanapoanza kusomwa? Nani atapenda kuja kuwekeza kwenye nchi ambayo hakimu anaonekana akinywa pombe na kula mishikaki na mtuhumiwa siku moja kabla ya kesi kusikilizwa mahakamani?
Tukubali kuwa, rushwa iliyopenya hata kwenye vyombo vya dola vyenye dhamana ya kulinda haki za raia ni sawa na saratani. Kuna wakati Mbunge Jackson Makwetta alizungumza kwa kirefu na kwa uchungu uliodhihiri juu ya tatizo la rushwa hususan katika vyombo vyenye kutoa haki kama polisi na mahakama.
"Mheshimiwa Spika, huko vijijini kesi nyingine zinaamuliwa na watendaji wa vijiji kutokana na kukosekana kwa mahakimu," alisema Makwetta .
Naam. Yawezekana ndege aliyotutayarishia Benjamin Mkapa iko tayari kupaa, lakini tunahofia, kuwa itabaki uwanjani ikiunguruma. Njia ya kurukia ina tope zito. Rubani tuliye naye sasa asijifungie chumba cha rubani, atoke nje kuongoza kazi ya kukwangua tope.
Tunazungumzia vita dhidi ya rushwa na ufisadi. Vinginevyo, ndege itabaki ikiunguruma, itaishiwa mafuta, itaharibikia uwanjani. Haitapaa. Heri ya Mwaka Mpya kwenu nyote.
Simu:
0754 678 252
Barua-pepe:
mjengwamaggid@gmail.com
Blogu:
mjengwa.blogspot.com