Thursday, January 15, 2009
Hatumchunguzi Mkapa - TAKUKURU
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema kwamba haimchunguzi rais msitaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kwa “ tuhuma yoyote ya kijinai”.
Taarifa ya TAKUKURU kwa vyombo vya habari, iliyosambazwa jana Jumanne, ilisema: “Katika siku za hivi karibuni kumekuwapo na uvumi ambao umekuwa ukitolewa katika baadhi ya vyombo vya habari mbalimbali vya habari ukibeba ujumbe kwamba rais msitaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, anachunguzwa na vyombo vya dola ikiwamo TAKUKURU.
“TAKUKURU inawafahamisha wananchi kwamba uvumi huu hauna ukweli wowote. TAKUKURU haimchunguzi kiongozi huyu kwa kosa au tuhuma yoyote ya kijinai kama inavyodaiwa”.
Taarifa hiyo ya TAKUKURU ilisema kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 46 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 haiwezi kumchunguza Mkapa.
Iliongeza taarifa hiyo ikinukuu Katiba: “Isipokuwa kama ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana na masharti ya ia ibara ya 46A(10), itakuwa ni marufuku kumshitaki au kufungua mahakamani shauri lolote la jinai au la kumdai mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo lolote alilolifanya yeye kama Rais wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya Rais kwa mujibu wa katiba hii.”
Ilisema kwa msingi huo wa Katiba, TAKUKURU “imeona ni vyema kuwafahamisha wananchi ukweli dhidi ya uvumi huu. Tukumbuke wakati wote kwamba Taifa letu lina Katiba ya nchi ambayo imeweka misingi mikuu ya kuendesha nchi, haki na wajibu wa kila Mtanzania”.
Raia Mwema Disemba 24, 2008