CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepitisha uamuzi kuwa wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani sasa watakuwa wakipigiwa kura za maoni na kila mwanachama, badala ya utaratibu wa zamani uliokuwa ukiwaruhusu wajumbe wachache kushiriki kupitia mikutano mikuu ya majimbo.
Kwamba, utaratibu mpya unatoa nafasi kwa kila mwanachama wa chama hicho kupiga kura katika tawi lake na hivyo kuwa vigumu kwa wagombea kuwahonga wanachama katika matawi yote katika jimbo husika.
Sambamba na uamuzi huo, CCM pia imepitisha uamuzi wa kuongeza uwakilishi wa wanawake katika Bunge na Baraza la Wawakilishi, ili idadi ya wanawake katika vyombo hivyo iwe asilimia 50 ya wabunge au wawakilishi wote wanaochaguliwa.
Tunachukua fursa hii kupongeza uamuzi huo uliofanywa na Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kwa sababu ni njia mojawapo ya kuziba mianya ya rushwa ambayo ilikuwa ikitumiwa na baadhi ya wagombea kuwarubuni wapiga kura, kwa kuwa walikuwa wachache na walikuwa wakipatikana kwenye eneo mmoja.
Kitendo cha kuwakutanisha wanachama wachache wa CCM kwenye mkutano mmoja wa jimbo kilikuwa kinatoa fursa miongoni mwa wagombea kutoa fedha kwa urahisi na hivyo kuifinya demokrasia ya kupata viongozi bora na waadilifu.
Utaratibu huo mpya pia unapanua demokrasia kwa kuwashirikisha watu wengi zaidi katika kupiga kura za maoni na hivyo kupanua nafasi ya kila mwanachama kumchagua kiongozi anayemtaka, badala ya utaratibu wa kuwakilishwa kwenye mikutano ya majimbo, ambako wanachama wenye uchu na fedha walirubuniwa kwa urahisi.
Lakini pia tunachukua fursa hii kupongeza juhudi za kuongeza idadi ya uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya kutunga sheria kufikia asilimia 50 ya wabunge, wawakilishi na madiwani. Hii pia ni hatua nzuri ya kupanua demokrasia na kuongeza sauti za wanawake katika vyombo hivyo vya wananchi.
Jambo la msingi ni kwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kupokea mapendekezo ya CCM ili kurekebisha katiba za pande hizo mbili na sheria zake za uchaguzi, mapema iwezekanavyo, ili mabadiliko hayo yaweze kutumika katika uchaguzi mkuu ujao, tupate safu nzuri za viongozi.
Tunachukua nafasi hii pia kuvishauri vyama vingine vya siasa kuwa na taratibu za wazi za kupanua demokrasia kwa kushirikisha wanachama wao wengi zaidi katika michakato ya kupata viongozi wa vyama na hata wabunge, wawakilishi na madiwani.
Ni kwa njia hii sisi kama nchi tutakuwa na haki ya kujivunia mifumo yetu ya kupata wawakilishi wa wananchi na hata viongozi katika ngazi mbali mbali nchini.