Tuesday, January 13, 2009

Mgongano wa kimaslahi na ufisadi unaoitesa nchi yetu

MARA kadhaa tumesikia viongozi wetu waandamizi na hata mkuu wa nchi Rais Jakaya Kikwete akielezea dhamira ya Serikali yake kupeleka mswada bungeni unaozuia kuchanganya siasa na biashara.

Hili pengine linaweza kuwa ni jibu muafaka kwa matatizo yanayolitesa Taifa; ulaji wa rushwa, matumizi mabaya ya ofisi za umma na ufisadi unaotishia amani, umoja na utulivu wa nchi.

Mara kadhaa mimi na wengine pia hupenda kusema nchi yetu ipo njia panda; yale yanayotokea sasa hayajawahi kushuhudiwa kwa muda mrefu au hayajawahi kutokea kabisa katika historia ya nchi. Ni njia panda, kabla hatujafika huko tunapotaka kufika katika Tanzania ile yenye neema na maisha bora kwa watu wake.

Kitafsiri mgongano wa kimaslahi ni ile hali inayojitokeza pale mtu aliye katika nafasi fulani ya kuaminiwa (mfano; mwanasiasa, mwanasheria, mhandisi n.k) anapokuwa na maslahi yanayokinzana, baina ya maslahi yake binafsi na nafasi aliyokuwa nayo.

Kukinzana huko kwa maslahi kunamuweka katika nafasi ngumu ya kufanya maamuzi bila ya kufanya upendeleo unaosukumwa na maslahi ya kibinafsi. Ikumbukwe mgongano wa kimaslahi unaweza kujitokeza hata pale ambapo hakuna uvunjwaji wa sheria au hata kukiukwa kwa maadili.

Mgongano wa kimaslahi unaweza kutengeneza picha ya upendeleo hata pale mhusika pengine hakuwa na nia ya upendeleo na hivyo basi kuiweka taaluma yake au cheo chake katika hali ya kutiliwa shaka.

Njia bora kabisa ya kupambana na mgongano wa kimaslahi ni kuuepuka moja kwa moja kwa kuepuka kujihusisha kabisa na biashara yoyote au taaluma yoyote baada ya kuteuliwa kushika ofisi ya umma.

Mfano, mwanasiasa aliyeteuliwa au kuchaguliwa kushika wadhifa fulani anaweza kuuza hisa zake zote katika mashirika au kampuni alizokuwa akishiriki. Au kwa namna nyigine anaweza kuzihamisha hisa hizo kwenda katika chombo cha udhamini kitakachokuwa kinaendelea na biashara bila ya ufahamu wake au yeye kuwa na ushawishi wa namna yeyote.

Wale wanaoona kwamba panaweza kutokea mgongano wa kimaslahi kwa wao kuwapo katika nafasi ya kimaamuzi au ushawishi inashauriwa ni bora wakakaa pembeni, na mtumishi muadilifu na mkweli ni yule ambaye pia atakuwa tayari kusema kwa uwazi kwa wenzake kuwa anajitoa katika kujadili suala husika kwa sababu kutakuwa na mgongano wa kimaslahi.

WANAHARAKATI WENZANGU MNALIONAJE HILI?