HAKUNA haja kwa Watanzania kusubiri nchi iingie gizani ndipo waamue kama alivyosema Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Dk. Idris Rashid. Kwa nini tusubiri giza ili tuamue wakati tunaweza kuamua sasa? Tufanye uamuzi mmojawapo kati ya mambo mawili.
Mosi, awajibishwe Dk. Rashid na wenzake kwa sababu walikwenda likizo (uzembe) na waliporejea ofisini ghafla wakabaini ni lazima wanunue mitambo ya Dowans. Pili, kama Rais Jakaya Kikwete hatawawajibisha hawa ambao wamepuuza ahadi yake ya Mei 9, 2006 kwa Watanzania, basi tuanze kujutia kura zetu zilizompa ushindi aongoze Ikulu.
Ni aibu kiongozi tuliyempa jukumu la kiutendaji kuratibu sekta ya umeme, akakosa kuwa na kile kinachoweza kuitwa “plan B.”
Tutakuwa watu wa ajabu kama tutakumbatia ushauri wa Dk. Rashid, wa kusubiri maisha ya giza, hospitali kukosa umeme, viwanda kushindwa kuzalisha na wanafunzi kushindwa kusoma.
Yapo maswali mengi yanayoibuka katika sakata la Dowans. Mosi, kwa nini Dk. Rashid na wenzake katika Tanesco wakose mbinu mbadala licha ya kuongoza shirika hilo kwa miaka kadhaa?
Kwa nini leo hii aibuke na kuonya kuwa kuna dharura ya umeme, na lazima inunuliwe mitambo ya Dowans?
Natambua kuwa Dk. Rashid ametoa sababu za kwa nini lazima anunue mitambo ya Dowans akisema ni kutokana na ufinyu wa muda na dharura.
Binafsi naamini kuwa sababu hii ni sehemu ya mpango wa kuhalalisha malengo ya muda mrefu ya kununua mitambo ya Dowans. Imani yangu hiyo inatokana na ukweli kwamba Tanesco imekuwa na wanasheria wake au ina uwezo wa kukodi wanasheria kama ilivyofanya wakati wa kuvunja mkataba kati yake na Dowans, Agosti mosi, mwaka 2008.
Je, Dk. Rashid alishindwa kuomba ushauri wa kisheria tangu mwaka jana kwamba anaweza au hawezi kununua mitambo ya Dowans bila kuvunja sheria za nchi?
Je, hakujua kuwa kuna zuio la Mahakama lililowekwa na Tanesco dhidi ya mitambo ya Dowans? Lakini pia je, hakujua kuwa Dowans imeshitaki katika Mahakama ya Usuluhishi, jijini Paris, Ufaransa?
Kubwa zaidi, tujiulize na kutafakari, je, Dk. Rashid na wenzake walikuwa katika likizo ya muda mrefu kiasi gani ? Likizo ambayo mara baada ya kwisha waliporejea ofisini ghafla wakabaini hakuna njia yoyote mbadala zaidi ya ununuzi wa mitambo ya Dowans hata kama ni kuvunja sheria, ikiwamo Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004?