Thursday, January 8, 2009
Wajumbe UWT wamfitinisha JK na Sophia Simba
WAKATI Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) ukitarajia kupata mwenyekiti wake mpya wiki hii, kumekuwapo na hujuma dhidi ya demokrasia itakayofanikisha mchakato wa kumpata mwenyekiti huyo, Raia Mwema imebaini.
Miongoni mwa mambo yaliyoibuka ni kutajwa kwa Rais Jakaya Kikwete kumuunga mkono mmoja wa wagombea wa naasi hiyo, Waziri wake wa Utawala Bora, Sophia Simba, madai ambayo yameshindwa kuthibitishwa na uongozi wa juu wa CCM uliopelekewa.
Pamoja na kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Sophia Simba ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, nafasi ambayo inatafsiriwa kuwa imetokana na kuwa kwake karibu na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete.
Mbali ya kutajwa kwa Rais Kikwete ambaye ndiye atakayefungua rasmi mkutano wa UWT leo Jumatano, tuhuma za rushwa na kuchafuana kwa wagombea ni mambo yaliyotawala kampeni za kuelekea uchaguzi wa jumuiya hiyo yenye nguvu ndani ya chama tawala.
Baadhi ya wapambe wamefikia hatua ya kusambaza ujumbe wa maneno kupitia simu za mkononi za baadhi ya wajumbe wakitumia ugonjwa wa mmoja wa wagombea kama sababu ya kutaka asichaguliwe kushika nafasi hiyo ya uongozi wa UWT. Nafasi hiyo inawaniwa pia na wabunge wa Viti Maalumu Janet Bina Kahama na Joyce Masunga.
Wagombea kupitia wapambe wao inadaiwa wanahujumu mkondo wa demokrasia ya mmojawao kuchaguliwa kumrithi mwenyekiti anayemaliza muda wake, Anna Abdallah.
Inadaiwa kuwa baadhi ya washiriki wa kampeni za wagombea hao walilazimika kusafiri na baadhi ya wajumbe kuelekea Dodoma katika kile kilichoelezwa kuwa kuwathibiti wasibadili mawazo ya kumchagua mgombea wa kundi wanalounga mkono.
Wajumbe waliojikuta wakisafiri na wapambe wa wagombea hao ni pamoja na wanaotoka katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Wajumbe wengine kutoka mikoa ya Kusini walijikuta wakizuiwa kwa muda jijini Dar es Salaam katika kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni “kuwekwa sawa.”
Baadhi ya wajumbe wamejikuta wakigharimiwa huduma za malazi jijini Dar es Salaam, kabla ya kuelekea mjini Dodoma kupiga kura.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa wajumbe hao wamekuwa hodari katika kutoa ushirikiano ili kupewa rushwa na wapambe wa wagombea hao.
Habari kutoka mjini Dodoma zinaeleza kuwa wapambe wa baadhi ya wagombea waliwasili mjini hapo siku kadhaa, baadhi ya wagombea waliwasili mjini hapo siku kadhaa kwa ajili ya kuwapokea wajumbe wapiga kura.
Lakini wakati wapambe hao wakiwa wamewasili Dodoma kabla ya wajumbe kuwasili, washindani wao walilazimika kusafiri hadi katika mikoa wanakotoka wajumbe hao na kusafiri nao kuelekea Dodoma.
Kilele cha uchaguzi huo kinafikiwa wakati wagombea Sophia Simba na Mbunge wa Viti Maalumu, Janet Kahama wakiwa katika mvutano na mchuano mkali.
Kumekuwapo na malalamiko kutoka katika kila upande kuhusiana na kuchezeana ‘rafu’ na zaidi ni kambi mbili za Janet Kahama na ile ya Waziri Simba.
Janet Kahama kama ilivyo kwa Joyce Masunga ni wabunge wa Viti-Maalumu na ukweli ni kwamba mchakato wa kupata wabunge wa aina hiyo huhusisha ushindani ikiwa ni pamoja na kupigiwa kura na wajumbe maalumu katika mikoa wanakogombea.
Hata hivyo, madai kwamba Waziri Simba ametumwa na mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kugombea nafasi hiyo yamekwishakanushwa.
Madai hayo si mara ya kwanza kutajwa, yamewahi kujitokeza katika kinyang’anyiro cha viongozi wa juu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) pia.
Mara kadhaa, Rais Kikwete mwenyewe amesikika akikanusha madai hayo. Lakini wakati Waziri Simba akiwa katika mazingira hayo, mgombea Janet Kahama naye anadaiwa kuungwa mkono na mwenyekiti anayemaliza muda wake, Anna Abdallah.
Haijafahamika ni kwa nini Anna Abdallah amuunge mkono mgombea huyo, lakini inawezekana ni imani yake kuwa mama huyo aliyepishana naye miaka mitatu kiumri (Anna akiwa mkubwa zaidi) ataweza kuongoza umoja huo kwa tija zaidi.
Lakini licha ya kuwapo kwa madai hayo, Anna Abdallah hakuwahi kusikika hadharani akiyapinga, lakini pia hakuna ushahidi wowote unaothibitisha kuwa anamuunga mkono Janet Kahama.
Wakati wagombea hao wakiwa na mazingira hayo, mgombea mwingine Joyce Masunga naye anatajwa kuwa na kigogo anayemuunga mkono.
Baadhi ya wajumbe wa UWT wanadai kuwa anaungwa mkono na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.
Tofauti na wenzake hao wawili, Masunga amekuwa akiendesha kampeni za kimya kimya, na kwa wanasiasa wengine waliozoea mikikimiki ya kampeni wanadai kuwa mwenendo wa kampeni za mgombea huyo zinaweza kumwangusha.
Anna Abdallah anaondoka madarakani baada ya kuongoza UWT kwa miaka 14. Aliingia madarakani mwaka 1994, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Sophia Kawawa, aliyefariki dunia.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, endapo mmojawapo kati ya Sophia au Kahama atashinda kiti hicho, uongozi wake huenda ukakabiliwa na changamoto nyingine ndani ya umoja huo.
Kuna uwezekano mkubwa changamoto hizo zikawa zinaibuliwa na kundi la mshindani atakayeshindwa ili hatimaye kuthibitisha kuwa ilikuwa ni makosa kwa mhusika kuchaguliwa kutokana na uwezo duni kiutendaji.
Hali hiyo inatabiriwa kwa kuwa wito wa kuvunja makundi ndani ya CCM umekuwa ukipuuzwa licha ya wito huo kutolewa na viongozi wa juu, akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Rais Kikwete.
Nafasi ya Uenyekiti wa UWT kama ilivyo kwa jumuiya nyingine za chama hicho, ina umuhimu wa pekee kutokana na anayeshika nafasi hiyo kuingia moja kwa moja katika vikao vya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu.
Kuwa mjumbe wa Kamati Kuu CCM mwaka mmoja kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kuna umuhimu mkubwa kisiasa, si tu kwa mjumbe husika bali pia kwa wanasiasa wengine wakiwamo wagombea wa nafasi za kisiasa katika dola ikiwamo Urais na Ubunge.
Ni kwa ajili hii wanasiasa wengi makini wametupa karata zao katika uchaguzi wa UWT kama walivyofanya katika uchaguzi wa Umoja wa Vijana (UVCCM) uliokuwa na makeke mengi na ule wa Jumuiya ya Wazazi, ambao umeshindwa kufanyika kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo makundi ndani ya chama hicho tawala.
Uchaguzi huo umetanguliwa na mkutano wa Baraza Kuu la UWT lililoketi Jumanne, wiki hii.
Miongoni mwa mambo yaliyopitiwa katika mkutano huo wa Baraza Kuu ni pamoja na kupitia ripoti ya utendaji ya umoja huo katika kipindi kilichopita.