Tuesday, January 13, 2009

Nyuma ya uamuzi wa Rais


NJAA ya wadokozi ambao siku hizi ni maarufu kwa jina la mafisadi, imegharimu kwa kiasi kikubwa maisha ya raia wa kawaida nchini.

Kodi anayolipa raia huyo kwa mfano, wakati anaponunua chumvi au sukari dukani imekuwa ikidokolewa na mafisadi kwa kipindi kirefu sasa.

Kodi hiyo imekuwa ikidokolewa na kwa kutumia mbinu za kifisadi, imekuwa ikigharimia miradi ambayo mwishowe hunufaisha mafisadi.

Miradi kama ya kuzalisha umeme wa dharura, ununuzi wa rada ya kijeshi kwa bei ya juu na hata ununuzi wa ndege ya Rais.

Fedha za malipo kwa miradi au ununuzi wa mali hizo zimekuwa zikitoka katika fuko (hazina) lililokusanya kodi ya raia.

Raia huyo ni pamoja na mkulima aliyenunua kiberiti na mafuta ya taa dukani, kwa ajili ya kuwashia kibatari chake kijijini.

Ndiyo! Hapa nchini kila mmoja ni mlipa kodi hata mtoto mchanga. Mzazi analazimika kumlipia mtoto wake mchanga kodi, na hasa anaponunua mahitaji ya mtoto huyo.

Ukweli ni kwamba karibu kila bidhaa inayouzwa dukani nchini inatozwa kodi kabla ya kumfikia mlaji. Iwe bidhaa inayozalishwa nchini au inayoingizwa kutoka nje ya nchi.

Na bidhaa inapomfikia mlaji, kiwango cha awali cha kodi kilichotozwa humwangukia mlaji huyo. Hivyo unaweza kusema karibu kila mtu nchini ni mlipa kodi.

Na kwa maana hiyo kila mtu nchini anapaswa kuchukizwa na ufisadi wa aina yoyote. Huzuni au hasira ya raia wa Tanzania dhidi ya ufisadi haiwezi kutulizwa kwa nadharia bali kwa vitendo.

Matukio ya ufisadi yaliyokwisha kutokea awali ni majereha yanayoweza kuponywa lakini yakaacha makovu. Tunaweza kuyaponya majeraha hayo kwa kurejesha kilichoibwa na kuwachukulia hatua wahusika, lakini hatuwezi kusahau tabia yao hiyo ya udokozi katika historia ya nchi.

Tafakari yangu kuhusu safari ya vita dhidi ya ufisadi ililazimika kuingia katika ukurasa mpya baada ya kusikiliza hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya salamu za mwaka mpya.

Kati ya mambo aliyozungumzia Rais Kikwete katika hotuba yake ya Desemba 31, mwaka jana, ni kuhusu majukumu mapya kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.

Kwa mujibu wa Rais, Katibu Mkuu Kiongozi sasa atakuwa na majukumu mapya. Atakuwa akisikiliza malalamiko ya wawekezaji (bila shaka wale wa ughaibuni).

Rais ameeleza sababu za kufanya uamuzi huo. Akasema ni kutokana na kuwapo kwa dalili za wazi kuwa Tanzania imeanza kupoteza imani kwa wawekezaji.Uamuzi huo ni wa busara lakini pia umenifanya nijiulize maswali. Msingi wa kujiuliza maswali hayo ni kutokana na ukweli kwamba nchini kuna Kituo cha Uwekezaji (TIC). Kituo ambacho kimewahi kupewa tuzo kutokana na kile kilichowahi kuelezwa kuwa kufanya kazi yake kwa ufanisi, iweje basi leo hii Rais ambebeshe majukumu ya ziada Katibu Mkuu Kiongozi? Majukumu ambayo bila shaka yangeweza kubaki chini ya TIC?

Ni lazima kuna jambo halipo sawa, kuna kasoro. Lakini ni jambo gani hilo? Je, mambo si swari TIC? Au uaminifu umeota mbawa katika chombo hicho cha kuratibu uwekezaji na wawekezaji nchini? Je, chombo hiki hakina uwezo tena wa kusikiliza malalamiko ya wawekezaji? Katika hali ya kawaida na kama TIC ingekuwa na ufanisi usiotia shaka ni wazi kuwa Rais angeagiza jukumu la kusikiliza malalamiko ya wawekezaji kufanywa na chombo hicho, nilimsikiliza vizuri Rais Kikwete, alikuwa wazi zaidi katika hotuba yake, akasema wawekezaji wamekuwa na malalamiko mengi. Na kwa kuzingatia kukiri huko kwa Rais kuwa wawekezaji wamekuwa na malalamiko mengi ni wazi kuwa TIC imezembea kiutendaji,na kama si kuzembea basi ushauri wake kwa baadhi ya watendaji serikalini umekuwa ukipuuzwa. Lakini kama hali ni hiyo, ni nani hao wapuuzaji ndani ya Serikali? Ni makatibu wa wizara zipi, au mawaziri wa wizara gani?

Kwa nini malalamiko yawe mengi wakati chombo hicho (TIC) kikiendelea kuishi, tena kikiwa na watalaamu waliobobea? Watalaamu walioshiriki mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya uwezekazaji? Kwa nini malalamiko ya wawekezaji yawe mengi wakati mbali na kuwapo kwa TIC, kuna wizara mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya kisekta yanayogusa wawekezaji?

Kama utafanya tafakari ya kina utabaini kuwa uamuzi huu wa Rais unathibitisha kuwa kuna tatizo la msingi ndani ya mfumo wa kuratibu shughuli za wawekezaji,utabaini kuwa kuna tatizo ndani ya mfumo mzima wa kiutendaji serikalini. Na inawezekana hakuna mawasiliano mazuri ya kitaalamu kati ya baadhi ya taasisi na wizara.

Ni dhahiri kuwa kuna nguvu zinazopingana kimalengo ndani ya Serikali. Kwa mfano, ni wazi kuwa mantiki ya uwezekezaji nchini imeibua kambi mbili zenye mgongano, kuna kambi inayotumia mchakato wa kukaribisha wawekezaji nchini kwa maslahi binafsi, lakini pia kuna kambi inayohakikisha Taifa linanufaika wawekezaji kwa kiwango cha juu.

Na ukweli ni kwamba matokeo ya kambi hizi ni uamuzi wa Rais kutaka malalamiko ya wawekezaji yasikilizwe na Katibu Mkuu Kiongozi. Hakika uamuzi huu ni ishara kwamba kuna kasoro kubwa katika mfumo wa utendaji serikalini. Ni dhahiri kuwa uadilifu umekuwa bidhaa adimu serikalini.

Uamuzi huu wa Rais ni unazua maswali mengi zaidi kwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi sasa atakuwa akisikiliza malalamiko ya awali ya wawekezaji, na si rufaa za malalamiko ya wawekezaji.

Ningemwelewa zaidi Rais Kikwete kuhusu uamuzi wake huu kama angetangaza kuwa Katibu Mkuu Kiongozi atasikiliza rufaa za malalamiko ya wawekezaji.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Na Godfrey Dilunga
Raia Mwema, 9 Januari 2009