Friday, January 9, 2009

Chagueni uongozi, si fedha

HAKIKA inashangaza jinsi ambavyo Taifa hili linazidi kudidimia katika mambo ya hovyo ambayo huko nyuma hayakupata si tu kutendwa bali kusikika.

Na inaelekea huu ni ugonjwa unaotukeketa katika kila pembe ya maisha yetu na mbaya zaidi, sasa umeingia hadi kwenye siasa, ambako tunaona kila aina ya kituko.

Ni kana kwamba watu hawa wameagana. Tuanze na Mbeya. Kabla na baada ya kutangazwa kwa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini tulikuwa tukishuhudia kila aina uchafu kwa maana ya maneno yanayosemwa na wanasiasa wetu.

Bado tunashuhudia uchafu huo wakati huu wa kampeni. Bado badala ya kutuambia nini watakachofanya cha kuufanya umma uvutiwe nao, wengi wa wagombea wanalalamika. Lakini umma hauhitaji malalako haya.

Unaweza kusema labda haya yanayotokea yamekuwa hivyo kwa kuwa huu wa Mbeya Vijijini ni ushindani wa vyama na kila chama kinajitahidi kurubuni wapiga kura, ndiyo maana ahadi nyingine zinazotangazwa ni kichekesho.

Lakini yanapotokea katika chama hichohicho, katika kundi la watu wanaotakiwa kuwa na imani moja na mwelekeo mmoja, inatia shaka.

Wiki hii ni wiki ya uchaguzi katika moja ya jumuiya za Chama cha Mapinduzi (CCM). Umoja wa Wanawake (UWT) unafanya uchaguzi, kumpata, pamoja na wengine, Mwenyekiti.

Tumesikia tambo zisizoisha kutoka kambi zote zinazowania nafasi ya Mwenyekiti. Tambo hizi, mara kadhaa, zimetoka nje ya utaratibu wa kawaida wa kujinadi katika uchaguzi, zikawa matusi na kashfa kubwa!

Kuna habari za matumizi makubwa ya fedha katika uchaguzi huu kiasi kwamba mtu atajiuliza, kama alivyopata kujiuliza Baba wa Taifa, Julius Nyerere; kama mtu alikopa fedha hizi atazirudishaje?

Sisi bado ni waumini wa uchaguzi unaomtafuta mtu mwenye uwezo wa uongozi, si mwenye uwezo wa kugawa fedha nyingi kuliko mpinzani wake. Ikitokea wote ni wagawa fedha, hiyo ni bahati mbaya sana! Pamoja na hayo tuwaombe wajumbe UWT wajitahidi kuchagua uongozi badala ya fedha.

John Bwire
Raia Mwema, Januari 7, 2009