WAKATI anguko la uchumi duniani likiwakutanisha nchini mawaziri na magavana wa Benki Kuu za nchi za Afrika pamoja na viongozi wengine wa kimataifa, akiwamo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Dominique Strauss-Kahn, mtaalamu wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Haji Semboja, amesema tayari Tanzania imeanza kuathirika mapema zaidi na anguko hilo kuliko ilivyotarajiwa.
Kauli hiyo ya Dk. Semboja inakuja wakati mkutano huo wa siku mbili ulionza jana (Machi 10) ukilenga kujadili jinsi ya kuliepusha Bara la Afrika na madhara ya mtikisiko wa uchumi unaondelea kutikisa nchi nyingi zikiwamo zile ambazo ni wafadhili wakuu wa Bajeti ya Tanzania.
Kwa mujibu wa gwiji huyo wa uchumi, athari za kiuchumi dhidi ya Tanzania zimeanza kujitokeza wazi wazi katika nyanja za uwekezaji, ajira, biashara na hata katika siasa na zaidi, athari hizo zinaonyesha dalili za kuzidi kumomonyoa maadili ya jamii.
Katika maelezo yake, yatakayochapishwa katika toleo la wiki ijayo la gazeti hili, Dk. Semboja anabainisha baadhi ya athari za mapema dhidi ya Tanzania kuwa ni pamoja na kupunguza wafanyakazi, viwango vya mishahara kwa watumishi wanaobaki na hata kupunguza gharama za uzalishaji.
Anasema athari za wazi zimeanza kujitokeza mwanzoni mwa mwaka huu ambazo zinajumuisha kupungua kwa ajira na kupungua kwa vipato.
Mbali na hali hiyo, anasema ya kuwa kutokana na mtikisiko huo wa kiuchumi duniani,
sekta isiyo rasmi nchini itaendelea kubabaika hasa ikizingatiwa kuwa watu wengi hukimbilia kuwekeza mitaji katika sekta isiyo rasmi, kama kinga au njia ya kujikwamua kiuchumi na kujinusuru katika migogoro hii.
Kwa mujibu wa Dk. Semboja, ingawa kuna dalili ya ukuaji wa sekta isiyo rasmi katika maeneo mengi ya mijini na vijijini, sekta ambayo kila mara ni wastaafu, wanawake na vijana ndiyo wanaothubutu kushiriki katika sekta, tatizo linalojidhihirisha ni kuwa waliomo katika sekta hiyo wengi wao hawana takwimu na taarifa kuhusu masoko yao, hawana ujuzi wala uzoefu wa mwenendo wa sekta hiyo na hali hiyo inawaweka katika hatari ya kushindwa na hatimaye kuanguka mara tu wanapoingia.
Kwa upande wa athari za kisiasa, mtaalamu huyo anasema mtikisiko wa uchumi duniani umeanza kuonyesha athari, ambazo zinaweza kuvuruga amani na usalama wa raia na Taifa.
Ndani ya hoja ya mtikisiko wa uchumi, Dk. Semboja anaamini kuwa yapo mambo kadhaa yanayoweza kuisukuma jamii ya Watanzania katika athari zaidi.
“Tuhuma za viongozi mafisadi, mauaji ya jamii ya albino, ongezeko la watu wasioajiriwa, umasikini na ufukara uliokithiri katika jamii ni dalili mojawapo zinazoashiria kuwa usalama wa raia na Taifa uko hatarini,” anasema Dk. Semboja akiongeza: “Dalili nyinginezo ni pamoja kuongezeka kwa kashfa kwa viongozi wa kisiasa katika rushwa.”
Lakini anaamini kuwa dalili nyingine ni udhaifu wa Serikali katika kutatua matatizo ya kikatiba na kimsingi, kama vile huduma duni za afya, elimu, maji, nishati na matusi, kejeli na chuki binafsi kati ya viongozi.
Anaonya Dk. Semboja: “Hali inaweza kutumika kama sababu za kimsingi za kidemokrasia kutaka mabadiliko ya utawala wa kisiasa katika mchakato wa upigaji kura wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwakani.”
Kwa mujibu wa Dk. Semboja, athari nyingine zitajitafsiri katika kuendelea kubomoka kwa maadili ndani ya jamii ikiwa ni pamoja na kuchochea zaidi umalaya, uhalifu, na tabia mbaya za ulevi na utamaduni wa kisasa.
Anasema pia kwamba kuongezeka kwa demokrasia, taarifa na takwimu, maarifa, na maendeleo ya Teknohama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) kumebadilisha mwono, mila na desturi za jamii. Jamii zinatambua haki zao za kimsingi na uhuru wao kisheria.
Hata hivyo, Dk. Semboja anasema kwa bahati mbaya wapo wengi ambao hawajui mipaka na wajibu wao, hivyo kufanya tabia na maadili kuporomoka.
“Kwa mfano imekuwa hakuna tofauti kati ya wazee na vijana katika masuala ya ngono zembe, ulevi, uvivu, na nia za kutaka kupata utajiri wa haraka haraka kwa taratibu zisizo za kisheria. Mitikisiko, migogoro na athari za kijamii na uchumi wa utandawazi huu unaweza kuchochea au kukuza athari hizi mbaya za kijamii,” anasema.
Lakini anasema wakati kwa upande wa kijamii na kisiasa hali ikiwa hivyo, athari kwa upande wa sekta nyeti za uchumi wa nchi kama kilimo, utalii na madini zimezidi kuwa kubwa tofauti na ilivyotarajiwa na watalaamu wa uchumi mwishoni mwa mwaka jana.
Katika kilimo, taarifa zinaonyesha kuwa bei ya kahawa aina ya arabika na kokoa zimeshuka katika soko la dunia. Arabika imeshuka kwa asilimia 24 wakati kokoa ikiporomoka kwa asilimia 27, kati ya Julai mwaka jana hadi mwanzoni mwa mwaka huu.
“Inaonekana kuwa bidhaa muhimu za kilimo cha biashara zitashuka katika kipindi cha mwaka 2009. Kushuka kwa bei za bidhaa hizi muhimu kutasababisha athari ya kushuka kwa mapato ya biashara za nje,” anasema Dk. Semboja.
Anasema kutokana na kushuka kwa bei na wingi wa uzalishaji wa bidhaa za kilimo cha biashara za nje ya nchi, ni wazi kuwa mapato ya Serikali, Pato la Taifa (GDP), kupungua kwa ajira na kuongezeka kwa umasikini ni mambo yatakayoiumiza Tanzania.
Anasema katika utafiti wake huo ya kuwa katika kipindi cha mwanzo wa mwaka huu, mtikisiko wa kiuchumi umepunguza kasi ya mahitaji ya watu wa nchi zilizoendelea kupanga safari na utalii Tanzania.
Hapa, Dk. Semboja anasema: “Ni vema kutambua kuwa pamoja na kuwa Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, kama vile Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama nyingi, pwani nzuri, kisiwa cha Zanzibar na Pemba, utalii wetu uko chini, mdogo na ukuaji wake ni dhaifu ukilinganisha na nchi kama vile Kenya na Afrika Kusini.
“Sababu kubwa ya utalii duni hapa nchini ni pamoja na kuwa na miundombinu mibaya, kodi kubwa, huduma na bei mbaya za hoteli na usafiri na gharama kubwa kwa watalii.
“Hivyo, mtikisiko wa kiuchumi utaweza kuwa na athari kubwa katika maeneo ambayo watalii wataona kuwa fedha zao hazitapata huduma bora wanazohitaji.”
Anasema katika sekta ya madini, hali si tofauti na katika sekta ya kilimo na utalii. Mtikisiko kiuchumi duniani umeshusha bei za madini na kupunguka kwa mahitaji ya madini katika masoko katika nchi zilizoendelea.
Hali ya kushuka kwa bei za madini na kupunguka kwa mahitaji vimeathiri shughuli za uchimbaji, biashara na uwekezaji katika sekta ya madini.
Hapa nchini, tayari baadhi ya kampuni za uchimbaji wa dhahabu zimeanza kupunguza shughuli na ajira kama mikakati ya kupunguza gharama za uendeshaji.
Inaelezwa kuwa hali ikiwa mbaya zaidi, Marekani, Ulaya, China na India zinaweza kusitisha uwekezaji wa moja kwa moja nchini kwa kuhofia kupotea kwa mitaji na kupata hasara, hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania haina mazingara endelevu ya uzalishaji na kibiashara.
Anasema hatari kubwa zaidi katika Bajeti ijayo ya Serikali ni kwamba misaada kutoka kwa wahisani inaweza kupungua na kwamba mambo yakiendelea kuharibika zaidi, wahisani wenye nia njema watakuwa na kipato kidogo cha kutoa kama msaada.
Anasema Dk. Semboja: “Imekuwa rahisi kwa nchi zilizoendelea kukata matumizi ya serikali zao kwa kupunguza misaada inayokwenda nchi zinazoendelea.
“Kuna wahisani wa aina nyingi. Wapo wale wanaosadia katika kutoa misaada na mikopo bila masharti na riba kubwa. Wako wale ambao wapo tayari kutoa misaada ya mikopo kwa masharti ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na kibiashara na riba kubwa. Hili kundi la pili, ndilo lilovuna katika migogoro na kuneemeka.”
Anasema kwa Watanzania wa kawaida, hasa wajasiriamali, hali inaweza kwenda kombo kwa upande wao na hasa kutokana na onyo lilitolewa kwa benki za biashara nchini.
“Mabenki ya biashara ya kigeni yaliyomo nchini yameanza kupata joto la kutakiwa kuwa makini katika kutoa mikopo midogo kwa ajili ya shughuli za biashara ndogondogo hapa Tanzania.
“Hapa awali walikuwa wepesi kutoa mikopo aina ya msaada kwa ajili ya sekta binafsi inayoendeshwa na wazalendo, tofauti na sasa. Hii itachangia kusimamisha uwekezaji wa wazalendo kwa ajili ya maendeleo yao.
Raia Mwema,Machi 11,2009.
No comments:
Post a Comment