-Wabunge wamsubiri Pinda
-Wataka wahusika washitakiwe kama kina Mramba
BAADHI ya wabunge, wanasiasa na wataalamu wa sheria wanautazama uamuzi wa kumburuza mahakamani Mkurugenzi wa Kampuni ya Richmond, Naeem Gire, kwa tahadhari kubwa wakiamini kuwa kuna malengo yaliyojificha.
Richmond Development LLC ni kampuni iliyopewa zabuni ya kuagiza mitambo ya kufua umeme wa dharura, mwaka juzi, na ndiyo chanzo cha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na mawaziri Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.
Itakumbukwa kuwa katika taarifa ya Kamati Teule iliyochunguza Richmond , ikiongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harisson Mwakyembe, mapendekezo 23, yakiwamo ya kuwachukulia hatua waliohusika kuibebea kampuni hiyo kinyume cha taratibu na hata sheria za nchini, yalitolewa.
Wakizungumza na Raia Mwema, jijini Dar es Salaam ambako wabunge wanakutana kwa ajili ya maandalizi ya mkutano ujao wa Bunge utakaoanza Januari 27, mwaka huu, wabunge na watalaamu hao walidai kuwa msingi wa wasiwasi wao ni aina ya mashitaka yanayomkabili Naeem Gire.
Kwa mujibu wa hati za mahakamani, Gire anakabiliwa na mashitaka ya kusema uongo pamoja na kughushi nyaraka.
Anakabiliwa na mashitaka matano, baadhi yakiwa ni kuwasilisha taarifa za uongo katika Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na katika Timu ya Majadiliano ya Serikali (GNT), iliyoundwa na baadhi ya makatibu wakuu wa wizara, akiwamo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hazina, Gray Mgonja.
“Gire ni mtu mdogo sana katika sakata hii nzima ya Richmond , ni kweli kwamba naye ana makosa na anastahili kuchukuliwa hatua za kufikishwa mahakamani.
“Lakini sisi wabunge hatupaswi kugota hapo kimtazamo. Upeo wetu unapaswa kwenda mbali zaidi na hasa katika kutafakari uwezekano wa kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu wote waliohusika katika sakata la Richmond ,” anasema mmoja wa wabunge, mwenye taaluma ya sheria.
Anasisitiza kuwa kwa kuzingatia aina ya mashitaka dhidi ya Gire, kuna uwezekano kuwa watendaji wengine wote na wanasiasa katika kashfa hiyo, wakaonekana hawana hatia wala makosa.
Kwa mujibu wa mbunge huyo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, mashitaka dhidi ya Gire ya kusema uongo na kuwasilisha nyaraka zisizofaa, kisiasa inaweza kutafsiriwa kuwa mawaziri na timu ya watalaamu wa Serikali walikuwa na nia njema katika mchakato mzima wa Richmond, na hawastahili lawama kwa kuwa walipewa taarifa za uongo na nyaraka za kughushi.
Mbunge mwingine ambaye pia hakutaka kutajwa jina kwa madai kuwa wanaisubiri taarifa ya Serikali bungeni, alisema; “Issue mama katika Richmond ni watendaji wa Serikali waliohusika kuitia hasara nchi, huyo Gire achukuliwe hatua lakini si kipaumbele cha mapendekezo ya Bunge.
“Kamati Teule ya Bunge imefanya kazi kubwa na yenye ushahidi wa kutosha namna ambavyo watendaji na wanasiasa walivyoibeba Richmond , licha ya kuonywa na baadhi ya watalaamu wa TANESCO na wengineo,” alisema.
Itakumbukwa kuwa katika taarifa yake ya kurasa 165 kuhusu Richmond , Kamati Teule ya Bunge iliwahoji mashahidi 75, kwa kuwauliza maswali 2,717.
Kamati hiyo pia ilipitia nyaraka 104, zilizotajwa bungeni na Dk. Mwakyembe kuwa zimebeba ushahidi usio na shaka kwamba Wizara ya Nishati na Madini, iliibeba Richmond Development Company LLC kutoka
mwanzo wa mchakato wa zabuni hadi mwisho.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, William Shelukindo, alisema pamoja na kufunguliwa kwa kesi dhidi ya Gire, wahusika wengine waliosalia katika sakata la Richmond hawana mwanya wa kusafishwa.
“Ni kweli kwamba huyo Gire amefikishwa mahakamani, lakini yeye anakabiliwa na makosa ya jinai na kughushi, wapo watendaji Serikali wanaostahili kuchukuliwa hatua zaidi,” alisema Shelukindo akiongeza:
“Kama watendaji na viongozi wa kisiasa walikubali kudanganywa na Richmond tangu awali, maana yake ni wazembe…ni dhahiri kuwa wamefanya kazi kizembe na hii ni hatari kama kiongozi unadanganywa kirahisi tu…eeh! Unaweza kuangusha nchi kiuchumi…tutazidi kufuatilia hadi mwisho wake.”
Alisema wanasubiri taarifa ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mapendekezo ya Bunge.
Kwa mujibu wa Shelukindo, wanataraji Waziri Mkuu atawasilisha taarifa yake kuhusu utekelezaji wa mapendekezo hayo katika mkutano ujao wa Bunge.
Waziri Mkuu Pinda alikwishawahi kuwasilisha taarifa yake ya awali bungeni kuhusu utekelezaji wa mapendekezo hayo na kuahidi kukamilisha utekelezaji huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema waliohusika na sakata la Richmond walitumia vibaya madaraka sawa na wanasiasa waliofikishwa mahakamani kuhusiana na suala la kampuni ya Alex Stewarts.
“Makosa ya Mramba (Basil) na Yona (Daniel) , ya kutumia vibaya madaraka yanafanana na watendaji waliohusika katika mkataba wa Richmond, hivyo wanatakiwa nao wafikishwe mahakamani,” alisema Lipumba.
Lakini kwa upande mwingine watalaamu wengine wa sheria wanabainisha kuwa hatua ya kumfikisha Gire mahakamani haiwezi kulifunga mdomo Bunge kuzungumzia kadhia ya Richmond .
Wanasema Bunge lina mwanya mkubwa kisheria na kikatiba kuhoji hatua iliyofikiwa na Serikali katika utekelezaji wa maazimio ya Bunge, bila kuingilia uhuru wa Mahakama (kesi ya Gire).
“Bunge linaweza kuendelea kujadili suala la Richmond bila kuingilia uhuru wa Mahakama. Suala la Gire ni la kijinai pekee. Lakini wapo watendaji waliozembea serikalini na yapo mapendekezo ya Bunge. Haya yote yanaweza kuhojiwa au kujadiliwa bila hata kuingilia Mahakama,” anafafanua mmoja wa wabunge wa muda mrefu bungeni.
Kamati Teule ya Bunge ililalamika kuwa katika kile kilichoelezwa kukidhi maslahi binafsi, Wizara ya Nishati na Madini ilikataa kuiruhusu kuona majalada ya wizara yenye mawasiliano kuhusu zabuni hiyo ya Richmond.
Ilibainika pia kuwa Wizara ya Nishati na Madini ilipindisha uamuzi wa Baraza la Mawaziri kwa kusitisha mpango uliokuwa umekaribia utekelezaji wa kuzalisha umeme kupitia mitambo ya kukodi ya kampuni ya CDC Globeleq.
Inadaiwa upuuziaji huo ulifanywa bila kuufikisha ujumbe wa Serikali kwa kampuni hiyo wa kurekebisha masharti yao ili mradi huo utekelezwe.
Inadaiwa pia kwamba hayo yalifanyika siku hiyo hiyo ambayo Baraza la Mawaziri lilitoa maagizo na siku nne baada ya kuanza mgawo wa umeme kwa mikoa yote ya Tanzania Bara inayounganishwa na Gridi ya Taifa.
Kamati Teule ya Bunge ilibaini pia kukiukwa kwa makusudi Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004, na Kanuni zake za mwaka 2005, licha ya Baraza la Mawaziri kusisitiza Sheria ya Ununuzi wa Umma na kanuni zake izingatiwe.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati Teule, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pia lilishinikizwa kutoheshimu ushauri wa kitaalamu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Kutokana na shinikizo hilo , Bodi ya Zabuni ya TANESCO iliwekwa pembeni na TANESCO ikaagizwa kuvunja sheria kwa kuwabadilisha wajumbe wa Bodi yake ya Zabuni.
Wizara ya Nishati na Madini pia ikafanya uamuzi wa
ununuzi kwa niaba ya TANESCO na kuulazimisha uongozi wake kusaini mkataba na kampuni ( Richmond ) ambayo TANESCO waliikataa mara tatu kwa vigezo vya kitaalamu kuwa haifai kwa kazi hiyo.
Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge zilizonukuu taarifa ya Mwakyembe “Huo ulikuwa udhalilishaji mkubwa wa viongozi na watendaji ndani ya TANESCO”.
Jambo jingine la kutilia shaka ni taarifa kwamba mwezi mmoja kabla ya zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura, Wizara ya Nishati na Madini iliiandikia Richmond Development Company LLC kuitaarifu kuwa imeshindwa kutekeleza mkataba baina yake na Wizara kuhusu mradi wa bomba la mafuta.
Kutokana na hali hiyo, kimya cha Wizara kuhusu udhaifu wa Richmond Development Company LLC, kuliipa Kamati Teule shaka kuhusu uadilifu wa viongozi wa Wizara.
Source: Raia Mwema 21, Januari 2009
No comments:
Post a Comment