WIKI tatu zilizopita, tulifurahia mwaka mpya wa 2009. Furaha yetu iliambatana na matumaini mapya.
Wenye mipango iliyokwama mwaka uliopita, walifurahia mwaka mpya huku wakitafakari namna ya kukamilisha mipango hiyo.
Hakuna aliyejitabiria matatizo, wala aliyepanga kumsababishia mwenzake matatizo. Tulitakiana heri ya mwaka mpya kwa dhati. Tuliamini kuwa uzembe unaogharimu maisha yetu, hususan ajali zisizo za lazima, utapungua au kwisha.
Lakini dalili za awali mwanzoni mwa mwaka huu zinabainisha bado hatujawekeza vya kutosha katika matarajio yetu. Hususan matarajio ya kupunguza au kutokomeza ajali za barabarani.
Ndani ya wiki hizi takriban tatu, tumepoteza ndugu, jamaa na rafiki zetu ambao tulipeana heri ya Mwaka Mpya kwa furaha.
Tumewapoteza katika vifo vya wakina mama wajawazito na watoto,mauaji ya albino, ajali za barabarani, mkoani Tanga na katika maeneo mengine ya nchi. Wamekufa wakati wakiwa safarini kufanikisha juhudi zao za kusaka maendeleo binafsi na ya taifa.
Kutokana na hali hiyo, kikubwa tunachokiona sisi ni mauaji yameongezeka hasa ya albino na vikongwe, tumeingia mwaka mpya wakati fikra zetu katika kudhibiti ajali za barabarani tu peke yake.
Tupo ndani ya mwaka mpya bila kuwa na fikra mpya katika kujiepusha na mauaji ya albino na vikongwe pamoja na ajali za barabarani. Abiria na madereva wameendelea kuwa chanzo cha ajali za barabarani.
Sehemu kubwa ya ajali hizo chanzo chake ni mwendo kasi. Hii ni sababu iliyo ndani ya uwezo wa dereva pamoja na abiria.
Tunahimiza jamii, abiria, madereva na watendaji katika vyombo vya dola kukumbuka kuwa Taifa bila watu ni sifuri. Wakumbuke kuwa Taifa lenye maombelezo mfululilizo hususan yasiyo ya lazima, si taifa la kujivunia.
Katika mwaka 2009, abiria, madereva na vyombo vya dola tujitahidi kuhakikisha tunakuwa Taifa lenye kukomesha mauaji ya albino na vikongwe na pia kuwa na idadi ndogo ya ajali za barabarani Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika na hata barani Afrika.
Pamoja Tunaweza!
No comments:
Post a Comment