WAKATI hali ya umeme nchini ikiwa bado tete, barua ya siri kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe kwenda kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kuhusiana na sakata la umeme na hali ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), imevuja.
Barua hiyo inagusia ushauri wa kamati ya POAC kwa Serikali kuhusiana na kukabiliana na hali ya umeme, ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali kuingilia kati na kuinusuru Tanesco kifedha, bila kugusia mitambo ya Dowans ambayo imekua gumzo kwa sasa.
Ndani ya barua hiyo ya mwishoni mwa mwezi uliopita, ambayo Raia Mwema imeiona, Zitto, kwa niaba ya kamati yake, ameishauri Serikali kuhakikisha kwamba kunakuwapo msaada wa dharura kwa Tanesco ili ijikwamue katika tatizo kubwa la kifedha na kuisaidia kununua mitambo ya kuzalishia umeme inayofaa bila kukiuka sheria za nchi.
“Kamati inawasilisha kwako ushauri wa kuiomba Serikali iiwezeshe Tanesco kununua mitambo ya umeme inayoona inafaa kulingana na mahitaji yake na bila kukiuka sheria za nchi ili kuliokoa Taifa kuingia kwenye giza na hivyo kuathiri uchumi wa taifa letu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo kutoka kwa Zitto.
Zitto, ambaye yuko mkoani Kilimanjaro kwa shughuli za chama chake, alikataa jana kuzungumzia kuhusiana na kuvuja kwa barua hiyo akisema: “…nilikuwa nje ya nchi na nimekuja moja kwa moja huku Machame kwa shughuli za chama.”
Kuvuja kwa barua hiyo kunakuja wakati Zitto anatajwa kama mmoja wa wanasiasa wanaoiunga mkono Tanesco katika mpango wake wa kununua mitambo ya Dowans, msimamo ambao umezua utata na kumuweka pabaya kisiasa, lakini alipoulizwa kuhusiana na msimamo wake kwa sasa alisema: “Msimamo wangu ni kuona nchi haipati giza na Watanzania wajifunze kuwa na viongozi ambao wana mawazo tofauti na wengi.”
Ndani ya barua hiyo, ambayo nakala yake imepelekwa kwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, kuna maelezo yanayoonyesha jinsi shirika hilo la umeme lilivyo na hali mbaya kifedha kutokana na sehemu kubwa ya mapato kutumika kununua umeme kutoka kampuni binafsi zinazozalisha umeme nchini.
Kuhusiana na ushauri wa serikali juu ya ununuzi wa mitambo barua hiyo inaeleza: “Kamati inapenda kuikumbusha Serikali kuwa maamuzi ya kununua mitambo ni maamuzi ya Serikali na si ya Kamati ya Bunge. Kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali na si utendaji wa kila siku. Kamati yangu imetoa ushauri huu kuisaidia Tanesco kupunguza gharama za kununua umeme na kuongeza mapato yake kwa kutekeleza mpango wake wa wateja 100,000 kwa mwaka. Tanesco hawataweza kuunganisha umeme kwa wateja 100,000 kwa mwaka kama hakuna umeme wa kuwapatia.”
Habari zaidi kutoka ndani ya Kamati ya Zitto zinaeleza kwamba baadhi ya wajumbe wameonyesha kuchanganywa na taarifa za vyombo vya habari zilizomnukuu Mwenyekiti wao akizungumzia Dowans wakati kamati haikuwa na maamuzi kuhusiana na kampuni hiyo.
Miongoni mwao ni Makamu Mwenyekiti wa Zitto, Mbunge wa Mbarali, Esterina Kilasi, ambaye alinukuliwa wiki hii akisema kwamba kamati haikuwa na maamuzi yoyote kuhusiana na Dowans.
Mjumbe mwingine wa kamati hiyo aliliambia Raia Mwema kwamba wajumbe wengi waliozungumzia suala la mitambo walibainisha kwamba Tanesco ni lazima inunue mitambo mipya na izingatie sheria.
“Baada ya Tanesco kuzungumzia dhamira yake ya kutaka kununua mitambo ya Dowans, tuliwaambia kwamba suala la kununua ama kutonunua ni suala la kiutendaji linalotakiwa kuzingatia sheria, ubora wa kitu kinachotakiwa kununuliwa na taratibu zifuatwe na tuliwasisitizia kwamba kazi ya Kamati na Bunge ni kusimamia,” alisema Mbunge huyo.
Mbunge huyo ambaye alikataa kutajwa jina kwa kuwa si msemaji wa Kamati, alisema waliwaeleza Tanesco waziwazi kwamba kitendo chao cha kufika katika Kamati kutaka mpango wao wa kununua mitambo upate baraka, hakikua sahihi.
“Tulisikiliza nia ya shirika dhidi ya mitambo hiyo lakini hatukubariki ununuzi huo. Uamuzi wa kamati ni kuishauri Serikali kununua mitambo mipya kwa ajili ya tahadhari na kukabiliana na tatizo la umeme linaloweza kujitokeza kama Tanesco walivyoonya, lakini kwa kuzingatia ubora, sheria, kanuni na taratibu za manunuzi,” alisema.
Mbali ya Zitto na Kilasi, wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Felister Bura, Diana Chilolo, Raphael Chegeni, Bahati Abeid, Emmanuel Luhahula, James Musalika, Peter Serukamba, Juma Njwayo, Tatu Ntimizi, Hafidh Ali Tahir, Elisa Mollel, Zaynab Vullu, Mwanawetu Zarafi, Mwadini Abass Jecha na Shally Raymond.
Mbali ya kutoa ushauri kwa Serikali, Kamati ya Zitto ilipendekeza kuwapo kwa kikao cha pamoja na kamati ya Nishati na Madini, maombi ambayo yalikataliwa na Spika Sitta, ambaye alibainisha wazi kwamba hakukuwa na sababu ya kikao hicho baada ya Kamati ya Nishati na Madini, inayoshughulikia sekta hiyo, uamuzi ambao unaelezwa kukubalika na kamati zote.
Tayari Tanesco wamekwishasitisha mpango wao wa kununua mitambo ya Dowans, lakini kwa taarifa ambayo ilitoa kitisho kwa wananchi kwamba kutakuwa na tatizo kubwa la umeme litakaloathiri sekta nyingi za huduma na uzalishaji.
Taarifa ya Tanesco iliyotolewa na Mkurugenzi wake Mkuu, Dk. Idris Rashid iliibua mjadala mpya wa kumtaka ajiuzulu kutokana na kutowajibika na kuutisha umma.
Katika tamko lake Dk. Rashid alisema: “Tanesco inatangaza rasmi kujitoa kwenye nia yake ya kununua mitambo hii. Ni imani yetu kwamba tumekwisha kujieleza na kujenga hoja za kutosha, na wananchi wa Tanzania, watafanya maamuzi yao hapo ambapo nchi itakapokuwa imegubikwa na kiza, hospitali hazitoi huduma, viwanda havizalishi, wanafunzi vyuoni wanashindwa kusoma kwa sababu tulishindwa kufanya maamuzi".
Sakata la Dowans limeibua mjadala mkali nap engine mgawanyiko wa wazi uliotokana na kauli za kukinzana kati ya wabunge wa kamati mbili ya POAC na ile ya Nishati na Madini inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli (CCM), William Shellukindo, anayesaidiwa na mwanasiasa machachari, Mbunge wa Kyela (CCM), Dk. Harrison Mwakyembe tofauti ambazo zimejitokeza zaidi katika vyombo vya habari.
Shellukindo na Mwakyembe wote walionyesha kushitushwa kwao na taarifa za kamati ya Zitto kujihusisha na masuala ya kisera badala ya kupitia hesabu huku wakihusisha hatua hiyo na mikakati ya kisiasa.
Dk. Mwakyembe ndiye aliyesema kwamba upo uwezekano wa suala hilo kutumika kama sehemu ya kampeni za kisiasa za Chadema ambako Zitto ni Naibu Katibu Mkuu wake, lakini Zitto akanukuliwa akisema suala hilo halina chembe ya siasa mbali ya maslahi ya Taifa.
Baada ya kauli za wabunge hao, Spika Sitta alifunga mjadala kwa kuishauri serikali kuachana na ununuzi wa mitambo ya Dowans kwa kuwa hauna maslahi kwa Taifa.
Raia Mwema, Machi 11,2009.