Friday, January 9, 2009

Waziri Chikawe awavaa wanaharakati


-Asema walishinikiza sheria mbaya ya kujamiiana mwaka 2002
-Afafanua kuwa inapingana na sheria ya ndoa ya mwaka 1970
-Atamka serikali kuifanyia mabadiliko haraka iwezekanavyo

Serikali inapitia sheria ya makosa ya kujamiiana (SOSPA) ya mwaka 2002 ili kupunguza adhabu kali zinazotolewa kwa watuhumiwa wanaotiwa hatiani kwa makosa ya kujamiiana, Rai limeelezwa.

Waziri wa katiba na sheria, Mathias Chikawe amesema pamoja na adhabu ya makosa hayo kuwa kali kwa adhabu ya chini kuwa kifungo cha chini ni miaka 30 na adhabu ya juu kuwa kifungo cha maisha gerezani, sheria hiyo pia inapingana na sheria ya ndoa ya mwaka 1970.

Alisema wakati sheria ya ndoa ya mwaka 1970 inaruhusu binti wa miaka 15 kuolewa, sheria ya makosa ya kujamiiana inatamka kuwa msichana wa miaka 18 na chini ya umri huo kwa kufanya tendo la ndoa kwa hiari au lazima ni kitendo cha kubakwa.

Waziri Chikawe alisema; "tunazitazama adhabu zinazotolewa kwa makosa ya ubakaji chini ya sheria ya makosa ya ubakaji ya mwaka 2002 ambazo ni mbaya kutokanana kutoa vifungo virefu na wakati huo ikipingana na sheria zingine halali za nchi".

Waziri Chikawe ambaye kitaaluma ni mwanasheria alisema sheria ya makosa ya kujamiiana ilipitishwa kwa shinikizo kubwa la wanaharakati waliokwenda kuweka kambi mjini Dodoma wakati muswada huo unawasilishwa imedhihirika kuwa na makosa mengi.

"Sheria ya SOSPA ilipitishwa wakati huo kukiwa kwenye wakati mgumu, wanaharakati walishinikiza ana kupitishwa kwa sheria hiyo na hali hiyo iliyofanya hata adhabu kuwa kali kutokana na mazingira yaliyotanda wakati huo lengo likiwa kulinda hadhi ya wanawake na watoto wa kike", anasema waziri Chikawe na kuongeza;

"Kutokana na upungufu huo, serikali sasa inapitia upya sheria hiyo kwa lengo la kurekebisha adhabu kwani zimebainika ni kali sana na hata mimi nakubaliana na wanaolia kwa adhabu hizo ambayo ni kifungo cha miaka 30 jela au kifungo cha maisha jela".

Kwa habari zaidi,
Gazeti la Rai, Januari 8-14, 2009
Ukurasa wa 1-3