Thursday, January 29, 2009

Richmond sasa ifikie mwisho


TANGU Bunge litoe mapendekezo yake kuhusu hatua za kisheria na kinidhamu dhidi ya wahusika katika kashfa ya zabuni ya kampuni ya Richmond Development, mwaka sasa unaelekea kutimia.

Katika mwaka huo mmoja, Bunge limekutana katika mikutano yake takriban mara tatu. Wabunge walikutana Aprili, mwaka jana, wakakutana katika Bunge la Bajeti na baadaye wakakutana katika mkutano wa Novemba, mwaka jana.

Kwa mara nyingine, Bunge limeanza mkutano wake mjini Dodoma. Huu ni mkutano wa 14 wa Bunge. Lakini pia ni mkutano wa nne wa Bunge, tangu Serikali iahidi kutekeleza mapendekezo kuhusu Richmond.

Tunatambua kuwa mbele ya Watanzania, Serikali na Bunge ni vyombo muhimu na ambavyo umma unaviheshimu sana. Ni vyombo vinavyogusa maisha ya kila siku ya raia wa Tanzania.

Pamoja na hayo tunadhani ni hatari kwa baadhi ya Watanzania kuamini kuwa Bunge au Serikali vinafanya mchezo wa kuigiza kuhusu Richmond kama ambavyo hisia miongoni mwa wanajamii zinavyoanza kujionyesha sasa.

Na hisia hizi si bure. Kwamba Richmond imegusa taasisi nyeti nchini kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni sababu tosha ya kuibuka kwa hisia hizi miongoni mwa umma.

Sisi tungependa kuona Bunge na Serikali vikitimiza majukumu yao barabara katika suala hili la Richmond ili wanaodhani ahadi ya Serikali kutekeleza mapendekezo ya Bunge ni mchezo wa kuigiza, wanatoka katika ulimwengu wa dhahania.

Ni busara sasa ahadi ya Serikali kuhusu Richmond ifikie mwisho ili mikutano ijayo ya Bunge iendelee na masuala na changamoto nyingine nyeti zilizoko mbele.

Hivyo ni imani yetu ya kuwa katika mkutano huu wa 14 wa Bunge, Serikali itawasilisha taarifa kamili bungeni, hasa ikizingatiwa kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alikwisha kuunda timu maalumu kufanikisha suala hili.

Hiyo ikifanyika itatoa nafasi kwa busara, raslimali, nguvu kazi na muda sasa kuwekezwa katika masuala mengine ndani ya mikutano ijayo ya Bunge huku Richmond ikiwekwa katika kaburi la sahau.

Source: Raia Mwema Januari 28,2009

No comments: