Thursday, April 14, 2011

Zanzibar wataka Serikali ndogo

CHAMA cha Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) kimeonesha wasiwasi juu ya ukubwa wa muundo wa Serikali na kutopangiliwa kwa idara zake na kumwomba Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, kuupitia upya muundo huo.

Pia kimemwomba aangalie uwezekano wa kupunguza pengo kubwa la mshahara kati ya watendaji waandamizi na watumishi wa umma wanaoanza kazi, ili kuongeza ufanisi.

“Tunamwomba Rais aangalie ukubwa wa serikali yake, mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi kwa kuwa ni mzigo kwa walipa kodi. Tunahitaji kuwa na Serikali ndogo na kuokoa fedha kwa ajili ya mishahara bora kwa wote,” alisema Katibu Mkuu wa chama hicho, Khamis Mwinyi Mohamed.

Khamis alitoa ombi hilo kwa Rais Shein wakati akizungumza Jumatano na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, inayofanyika kila mwaka Mei Mosi huku akidai kuwa Serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa kwa sasa idara zake zimekaa vibaya.

“Mahakama ya Kazi iko chini ya Mahakama Kuu, idara zinazohusika na ajira kwa watoto, usalama kazini na malipo kwa wafanyakazi zipo chini ya Wizara ya Ustawi wa Jamii, hii si sawa, idara hizi zinapaswa kuwa chini ya Wizara ya Kazi kwa ufanisi zaidi,” alisema.

Alisema kutopangiliwa ipasavyo kwa idara zinazohusiana na ajira, pia kunawavunja moyo wafadhili kama vile Shirika la Kazi Duniani (ILO) katika kusaidia maendeleo ya ajira kwa kuwa wanadhani Serikali haiko makini.

Aidha, chama hicho pia kilionesha wasiwasi wake juu ya kupanda kwa bei ya bidhaa kutokana na kukosekana kwa chombo maalumu cha kudhibiti bei ambacho kinatakiwa kuboresha pia maslahi ya wafanyakazi na kuziba pengo la mishahara.

“Haikubaliki kwa mfano, baadhi ya wakurugenzi wanalipwa mshahara wa mwezi unaofikia Sh milioni 1.5 wakati mfanyakazi wa kawaida mwenye shahada, analipwa Sh 150,000 kwa mwezi na mshahara wa kima cha chini wa Serikali ni Sh 100,000,” alisema na kushauri kima cha chini kiwe Sh 350,000.

No comments: